Kunani ujio wa simu mpya ya iPhone mwaka 2022?
- Inauzwa kwa gharama chini ya Sh1 milioni.
- Imesheheni baadhi ya sifa zilizopo kwenye toleo la iPhone 13 na pacha zake.
- Unaweza kuagiza simu hii kuanzia Machi13.
Dar es Salaam. Toleo la simu ya iPhone SE la mwaka 2022 limekuja na sifa zake. Lakini kubwa zaidi ya zote, ni ubora wake kuliko baadhi ya simu zinazouzwa juu ya Sh1 milioni.
Ikiwa ni miezi zaidi ya mitano tangu simu za iPhone toleo la “13” ziingie sokoni, Apple inatarajia kuliingiza sokoni toleo la SE na kwa wanaopenda kutoa oda za manunuzi ya simu hizo, wanaweza kufanya hivyo kuanzia Machi 13 mwaka huu.
Simu hiyo inakuja na uhifadhi kuanzia jigabaiti 64 (GB64), GB128 na GB256 huku ikitumia mfumo endeshi wa iOS 15 yenye mifumo ya Focus, share play na spatial audio.
Mbivu na mbichi za iPhone SE 2022
Simu hii inaambatana na uwezo wa kutumia mtandao wa 5G. Licha ya kuwa baadhi ya simu ikiwemo Samsung Galaxy S22 na nyingine zina uwezo huo SE inakuwa miongoni mwa simu zinazouzwa chini ya Sh1 milioni licha ya uwezo wake mkubwa wa utendaji.
Kwa mujibu wa Apple, kasi hiyo itamuwezesha mtumiaji kuendelea kutazama filamu huku akiwa kwenye simu za video (Face Time) bila kukatizwa burudani zake.
Pia, ili kutunza betri, simu hiyo ina uwezo wa kushusha kasi ya mtandao hadi 4G pale kunapokuwa hakuna haja ya kuwa na kasi kubwa ya mtandao.
“Mifumo inayokubali mtandao wa 5G duniani inazidi kuimarika. Ikiwa na wadau zaidi ya 200 katika masoko zaidi ya 70 yatakuwa yakiikubali mifumo hiyo mwisho wa mwaka huu,” imeeleza Apple katika taarifa yake kuhusu simu hiyo.

Apple Se yamwaka 2022, inaendelea kuwa na batani kama simu za matoleo ya iPhone 8 kushuka chini. Picha| Apple.
Kamera ya kufaa matumizi
Simu hii inakuja na megapikseli (MP) 12 kwa muundo wa kamera pana (wide) ikiwa na teknolojia ya potrait na Smart HDR 4 ambayo imetambulishwa kwenye simu za iPhone 13 na pacha wake.
Smart HDR 4 ni teknolojia inayohuisha rangi na kupunguza kelele/ uchafu kwenye picha huku ikimtofautisha fanani na sehemu ya nyuma yake (background).
“Hii inasaidia mwanga mzuri kwenye sura za fanani hata katika mazingira yenye mwanga hafifu,” imesema Apple ikiongeza kuwa teknolojia hiyo itasaidia kupata rangi halisi ya fanani.
iPhone SE na mazingira
Apple imesema simu ya Iphone SE imetengenezwa kwa kutumia malighafi zilizorejelewa ikiwa ni hatua ya Apple kutunza mazingira.
Kama toleo la 13, iPhone SE imetumia malighafi ya injini pamoja na sumaku za sauti ambazo zimerejelewa kwa asilimia 100.
Mfumo mpya wa ufungashaji unaondoa karatasi ya plastiki na hivyo kuisogeza Apple na lengo la kuondoa matumizi ya plastiki kwenye ufungashaji wake kwa asilimia 100 ifikapo 2025.
“Kufikia mwaka 2030, lengo la Apple ni kutokuwa na mchango katika uharibifu wa mazingira,” imeandika Apple yenye lengo la kuchangia katika kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa katika matengenezo ya bidhaa zake.
Soma zaidi:
- Kunani uzinduzi wa Samsung mwaka 2022?
- Mambo ya kuzingatia unapoanza kutumia simu ya iPhone
- Ufanye nini simu yako ikiingia maji?
Bei ya Mtanzania wa kawaida
Ni kawaida simu za iPhone, kuja na bei za mamilioni lakini kwa SE ya 2020, simu hiyo gharama yake ni Sh992,920 endapo utainunua moja kwa moja kutoka kiwandani au ukimwagizia mtu akununulie huko nje ya nchi.
Endapo ukiongeza na gharama za usafiri huenda ukahitaji nyongeza fedha kulingana na gharama za kampuni utakayoagizia.
Kazi kwako. Kama una mpango wa kufungua iPhone yako mwaka huu.
Latest