Uviko-19 kuendelea kuwa dharura ya afya duniani?

January 28, 2023 7:31 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link


  • Ni baada ya ugonja huo kudumu kwa miaka minne.
  • Visa na vifo vyaanza kuongezeka tena.

Dar es Salaam. Jumatatu ijayo Januari 30, 2023 itakuwa ni miaka mitatu tangu ugonjwa wa Uviko-19 utangazwe kuwa dharura ya afya ya umma duniani. 

Ugonjwa huo ulitangazwa kuwa ni dharura ya afya ya umma Januari 30, 2020 na mkutano wa pili wa kamati ya dharura ulioitishwa mjini Geneva Uswisi na Shirika la Afya Duniani (WHO), chini ya sheria za kimataifa za afya (IHR) (2015) kuhusiana na mlipuko wa virusi vya Corona (2019-nCoV) nchini China

Hata hivyo, swali linabaki kuwa ugonjwa huo utaendelea kuwa dharura ya afya? 

Kikao cha Kamati ya Kimataifa ya WHO kuhusu dharura za magonjwa ambacho kimekutana jana kwa mara ya 14 kutathmini iwapo bado Uviko-19  ni dharura ya afya ya umma au la, wakati huu ambapo wiki ijayo itakuwa gonjwa hilo linaingia mwaka wa nne.

Wakati tathmini hiyo ikiendelea, WHO imesema idadi ya vifo kutokana na ugonjwa huo imeanza kuongezeka duniani tangu mwishoni mwa mwezi uliopita wa Disemba 2022.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus amesema kuondolewa kwa vizuizi nchini China kumesababisha ongezeko la vifo kwenye taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani.

“Wiki iliyopita, vifo takriban 40,000 vya Uviko-19 viliripotiwa WHO na zaidi ya nusu ni kutoka China,”  amesema Dk Tedros mbele ya kamati hiyo.

Amesema wataongeza taarifa mpya kwenye dashibodi ya Uviko-19 ili kujumuisha wagonjwa wapya na vifo vilivyoripotiwa China katika wiki za karibuni.

Wiki nane zilizopita, zaidi ya watu 170,000 walikufa kwa ugonjwa huo duniani na idadi halisi inaweza kuwa kubwa.

Mkuu huyo wa WHO amesema chanjo, tiba na uchunguzi dhidi ya Uviko-19 vimesalia kama hatua muhimu katika kuzuia ugonjwa huo na kuokoa maisha ya watu. 

“Hata hivyo hatua za kimataifa bado zinasuasua kwa sababu katika nchi nyingi, hatua hizo muhimu za kuokoa maisha bado hazijafikia wale wanaohitaji zaidi, mathalani wazee na wahudumu wa afya,” amesema Dk Tedros.

Amefafanua kwa mifumo mingi ya afya duniani kote bado inahaha kukabiliana na Uviko-19, kando ya kuhudumia wagonjwa wenye matatizo mengine kama vile homa ya mafua makali, wakati huu ambapo kuna uhaba wa watumishi na hata walioko wamechoka.

Dk Tedros ametaja changamoto nyingine kuwa ni ufuatiliaji nao umezorota huku imáni ya wananchi kwa mbinu za kinga kama vile chanjo inaendelea kutikiswa na msururu wa taarifa potofu na za uongo.

Enable Notifications OK No thanks