WHO: Asilimia 95 ya vifo na wagonjwa wa malaria wako Afrika
- Kutokana na kuwa na rasilimali chache, WHO inapendekeza kuwa idadi ya watu walio hatarini zaidi kupewa kipaumbele.
- Lengo la WHO ni kupunguza idadi ya wagonjwa wa malaria na vifo kwa asilimia 90 ifikapo mwaka 2030.
Dar es Salaam. Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) limesema mwaka huu linajikita zaidi kuwafikiwa watu walio hatarini zaidi kupata ugonjwa wa Malaria kwa mikakati na nyenzo zilizopo ili kutokomeza ugonjwa huo unaokatili maisha ya maelfu ya watu kila mwaka.
Takwimu za shirika hilo zinaonyesha kuwa mwaka 2021 pekee watu 619,000 walipoteza maisha kutokana na malaria huku wagonjwa wapya wakifikia milioni 247 na asilimia 95 ya vifo na wagonjwa walikuwa katika ukanda wa Afrika.
Ripoti ya dunia ya malaria ya WHO kwa mwaka 2022 ilionyesha kuwa pengo la ufadhili kati ya kiasi kilichowekezwa katika kukabiliana na ugonjwa huo duniani na rasilimali zinazohitajika limeongezeka, hasa katika miaka mitatu iliyopita.
Wakati Dola za Marekani bilioni 7.3 (Sh17 trilioni) zingehitajika kudhibiti ugonjwa wa malaria, kiasi kilichowekezwa ni Dola za Marekani bilioni 3.5 sawa na Sh8.2 trilioni.
Kutokana na kuwa na rasilimali chache, WHO inapendekeza kuwa idadi ya watu walio hatarini zaidi kupewa kipaumbele.
Lengo la WHO ni kupunguza idadi ya wagonjwa wa malaria na vifo kwa asilimia 90 ifikapo mwaka 2030.
Licha ya vikwazo vya hivi karibuni katika udhibiti wa malaria, WHO imesema uwekezaji katika utafiti na maendeleo umekuwa na jukumu muhimu katika kupunguza mzigo wa kimataifa wa malaria tangu miaka ya 2000.
Mtoto mchanga akiwa amezungukwa na chandarua cha kujikinga na malaria nchini Ghana. Picha | Benki ya Dunia/Arne Hoel.
Vipimo vya uchunguzi wa haraka, vyandarua vilivyotiwa dawa na matibabu mseto yanayotokana na dawa ya ‘artemisinin’, ambayo ni dawa ya haraka dhidi ya ugonjwa huo, vimekuwa vya msingi katika kukabiliana na malaria.
Kwa mujibu wa WHO, kuendelea kuwekeza katika maendeleo na usambazaji wa zana za hali ya juu itakuwa muhimu katika kufikia malengo ya kimataifa ifikapo mwaka 2030.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linafichua kuwa kuna bidhaa kadhaa zinazofanyiwa utafiti ili zitumike katika kudhibiti mbu wanaoendeza malaria. Iwapo zana hizi zitakuwa na ufanisi, WHO itatayarisha mapendekezo mapya ya sera au kurekebisha zilizopo ili kusaidia utekelezaji wake katika nchi zilizoathiriwa zaidi na malaria.
Aidha, chanjo kadhaa za malaria zinatengenezwa. Shirika hilo linaeleza kuwa wengi hulenga vimelea vya malaria kabla ya kuingia kwenye ini, ambapo vinaweza kuongezeka kwa kasi.
Chanjo nyingine zinataka kukomesha maambukizi ya vimelea vya malaria au kuwalinda wanawake wakati wa ujauzito.
WHO inazihimiza nchi zilizoathirika zaidi na malaria kutumia zana na kutekeleza mikakati inayopendekezwa ambayo inapatikana.
Kadiri mchakato wa kimataifa wa kutokomeza malaria unavyoongezeka, nchi nyingi zaidi zimeanzisha mipango yao ya kutokomeza malaria.
#WorldMalariaDay2023
pic.twitter.com/rLVN3Qn5YA— Ofisi ya Waziri Mkuu (@TZWaziriMkuu) April 25, 2023
Kulingana na ripoti ya hivi karibuni zaidi ya dunia kuhusu malaria, kumekuwa na maendeleo katika kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma dhidi ya ugonjwa huo kwa makundi hatarishi zaidi.
Hata hivyo, watu wengi wenye uwezekano mkubwa wa kuambukizwa malaria bado hawana nyenzo za kuzuia, kugundua na kutibu.
Changamoto katika kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za malaria katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, zimechangiwa, hasa na janga la COVID-19, migogoro ya kibinadamu, ukosefu wa fedha, mifumo dhaifu ya ufuatiliaji na kupungua kwa ufanisi wa zana muhimu za kupambana na ugonjwa huo.
Latest