Waziri Masauni achaguliwa Makamu wa Rais UNEA

December 13, 2025 1:48 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Amechaguliwa kwa mujibu wa kanuni ya 18 ya kanuni za utendaji za UNEP.
  • Uchaguzi wake uliidhinishwa bila kupingwa na upande wowote.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA).

Masauni amechaguliwa katika nafasi hiyo Desemba 12, 2025, wakati wa Mkutano wa Saba wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA-7) uliofanyika jijini Nairobi, Kenya kwa siku saba.

Uchaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa kanuni za Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) zinazoruhusu uchaguzi wa viongozi wengine wa juu akiwemo rais na mwandishi katika mkutano wake mkuu.

Hii ni ni mara ya pili ndani ya mwaka 2025 kwa viongozi wa juu Serikalini kung’ara katika nafasi mbalimbali za uongozi Afrika na duniani, kuanzia kwa Profesa Mohammed Janabi aliyechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.

Prof Janabi alirithi nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkurugenzi Mteule, Dk Faustine Ndugulile, aliyefariki dunia kabla ya kuanza rasmi majukumu yake.

Mchakato wa uchaguzi wa Masauni UNEA

Mhandisi Masauni ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kikwajuni kuanzia Novemba 12, 2010 alipendekezwa na kundi la nchi za Afrika, ambalo kwa kuzingatia kanuni za mzunguko na uwakilishi wa kijiografia, limepewa nafasi mbili za Makamu wa Rais katika ofisi ya baraza hilo.

Baada ya kupendekezwa, jina la Masauni liliidhinishwa mara moja bila kupingwa, jambo linaloonesha imani na heshima kubwa ya jumuiya ya kimataifa kwa uongozi wa Tanzania katika masuala ya mazingira,.

Masauni anaenda kuwa miongoni mwa wajumbe 10, wanaounda baraza hilo pamoja na viongozi wengine wa juu akiwemo irais mmoja, makamu wa rais wanane na mwandishi mmoja katika ngazi ya uwaziri, huku wajumbe wawili wakiwakilisha kila moja ya maeneo matano ya Umoja wa Mataifa.

Waziri Masauni akiwa kwenye ziara ya kikazi Zanzibar, Desemba 18, 2024. Picha/VPO.

Mbali na Masauni viongozi wengine waliochaguliwa na baraza hilo ni pamoja na , Waziri wa Maji, Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi wa Jamaica, Matthew Samuda aliyechaguliwa kuwa Rais Baraza hilo baada ya kupendekezwa na kundi la nchi za Amerika ya Kusini na Karibiani.

Mwingine ni  Felix Wertli, Balozi wa Masuala ya Mazingira na Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kimataifa katika Shirika la Mazingira la Uswisi,.

Pamoja na uchaguzi huo, mkutano huo umepitisha maazimio 11, maamuzi matatu pamoja na tamko la mawaziri, yote yakilenga kuharakisha utekelezaji wa suluhisho kwa ajili ya kujenga dunia yenye ustahimilivu zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks