Jenista kuzikwa Desemba 16, mkoani Ruvuma
- Mazishi yake kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Spika wa Bunge, Waziri Mkuu, na Makamu wa Rais.
Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama unatarajiwa kuzikwa Jumanne ya Desemba 16, 2025 katika kijiji cha Ruanda, Mbinga mkoani Ruvuma.
Jenista ambaye amekuwa Mbunge wa Peramiho kwa takribani miaka 25 kwa kuchaguliwa na wananchi na kuteuliwa kwa viti maalumu, amefariki dunia jana Desemba 11, 2025 jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge usiku wa Desemba 11, 2025, leo Desemba 12, 2025, mwili utawasili nyumbani kwa marehemu eneo la Itega, jijini Dodoma ambapo maombolezo yatakuwa yakiendelea.
Aidha, ratiba inaonesha kuwa Jumamosi Desemba 13, kutakuwa na ibada kwenye Kanisa Katoliki Kiwanja cha Ndege, ambapo pia salamu za rambirambi zitatolewa na wananchi watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu na baadaye alasiri safari ya kuelekea Songea itaanza.
Ratiba hiyo inafafanua kuwa, Desemba 14, 2025, mwili utapelekwa Kanisa Katoliki Matogoro, Songea Mjini ambako kutakuwa na ibada, kisha baadaye mwili kupelekwa nyumbani kwa marehemu Makambi, Songea Mjini.
Jumatatu Desemba 15, 2025 asubuhi safari ya kuelekea Peramiho itaanza ambapo ikifuatiwa na ibada, salamu za rambirambi na kuaga mwili, kabla ya siku inayoafuata kuelekea kijijini Ruanda, wilayani Mbinga kwa maziko.
Viongozi mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria shughuli hizo za mazishi akiwemo Spika wa Bunge, Mussa Zungu, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba na Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi.
Jenista atakumbukwa kwa bidii yake ya uongozi alipotumika katika nyadhifa mbalimbali ndani ya Serikali ya Tanzania tangu ajihusishe rasmi na masuala ya siasa mwaka 1987
Historia yake iliandikwa kwa kalamu ya wino na kuacha alama katika awamu tatu za Serikali za Tanzania kuanzia ile ya Jakaya Kikwete, John Magufuli hadi awamu ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kiongozi huyo mashuhuri ambaye pia ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe bungeni anafutika katika uso wa dunia wakati ambao bado jimbo la Peramiho linamuhitaji baada ya kumpa ridhaa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29 kuliongoza kwa miaka mitano ijayo.