Rais Samia aongoza mamia kuaga mwili wa Jenista Mhagama Dodoma
- Asema Jenista ni kiongozi aliyevaa kofis nyingi, awataka viongozi kumuenzi.
- Atazikwa Desemba 16, 2025 Mbinga, Songea.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama akieleza kuwa kiongozi huyo alikuwa jasiri na mlezi wa wengi bungeni na serikalini.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika ibada ya kuaga mwili wa Mhagama iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Kiwanja cha Ndege mkoani Dodoma leo Desemba 13, 2025 amesema kiongozi huyo alikuwa mwadilifu akisimamia na kutetetea haki za Watanzania.
“ Katika maisha yake ya utumishi, alisimama imara kutetea haki, maendeleo na ustawi wa watu aliowaongoza…
….Alikuwa nguzo ya matumaini kwa wanawake na vijana na mfano wa uongozi uliotawaliwa na nidhamu, uadilifu na hofu ya Mungu,’ amesema Rais Samia.
Rais Samia pia amemuelezea Jenista kuwa miongoni mwa viongozi wachache walioshika nyadhifa nyingi ndani ya wakati mmoja suala lililoongeza ufanisi wa shughuli mbalimbali Serikalini.
“Yeye ndiye mtu pekee katika historia ya nchi yetu aliyewahi kuvaa kofia mbili za Katibu wa Kamati ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi na mnadhimu wa Serikali bungeni, na kofia hizo zilimtosha na kumuenea sawasawa,” amesema Rais Samia akielezea baadhi ya nyadhifa alizoshika Jenista.
Jenista aliyefariiki kwa maradhi ya moyo Desemba 11, 2025 anaacha pengo kubwa Serikalini, bungeni na kwa wananchi wa jimbo la Peramiho ambao tayari walimpa ridhaa ya kuwaongoza kwa miaka mitano.
Miaka 25 ya uongozi wake iliacha alama na historia isiyofutika kwa wabunge na viongozi wa Serikali katika awamu tofauti tofauti za uongozi alizozitumikia kama alivyoeleza Spika wa Bunge Azzan Zungu.
“Jenista ameondoka lakini malaika wake wapo, na sisi tupo tutaendelea kushirikiana kuendelea kusaidia maskini na wasio jiweza, Mungu amjalie amuweke pema na safari ya kwenda peponi iwe nyepesi,” amesema Zungu.
Kwa upande wake Makamu wa Rais Dk Emmanuel Nchimbi amemtuelezea Jenista kuwa ni kiongozi mnyenyekevu aliyejitoa kwa wananchi kwa moyo wote akiwataka viongozi waliosalia kufuata nyayo zake.
‘Kama Mungu angeniambia niombe kitu kimoja tu, ningeomba kwamba wabunge wote wa CCM, wabunge wote wa nchi hii, madiwani wote, wapende na watumikie watu wao kwa kiwango cha Jenista,” ameongeza Nchimbi.
Buriani Mhagama
Baada ya ratiba ya leo, kesho Desemba 14, 2025 kutakuwa na ibada nyingine ya kumuaga itakayofanyika katika Kanisa Katoliki Matogoro, Songea Mjini na baadae mwili wake utapelekwa nyumbani kwake Makambi, Songea Mjini.
Jumatatu, Desemba 15, 2025 asubuhi safari ya kuelekea Peramiho itaanza ikifuatiwa na ibada, salamu za rambirambi na kuaga mwili, kabla ya Desemba 16, 2025 kuelekea kijijini Ruanda, wilayani Mbinga kwa ajili ya maziko.
Latest