Serikali yajipanga kufikia asilimia 80 ya utoaji huduma kidijitali

December 12, 2025 3:09 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Yasema inampango wa kutoka katika mfumo wa karatasi na kuingia kikamilifu katika utoaji wa huduma za umma kidijitali kwa kwa asilimia 80 ifikapo 2025.
  • Ni kwa lengo la kurahisisha huduma kwa wananchi, kuongeza uwazi, na kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana kikamilifu.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema imejipanga kuwahudumia wananchi kidijitali hatua inayotajwa kurahisisha huduma, kuongeza uwazi na kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana kikamilifu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Desemba 12, 2025 amesema kuwa kwa sasa Serikali imefikia zaidi nusu ya lengo la kufikia asilimia 80 ya matumizi ya huduma za kigitali nchini.

“Kwa sasa tupo juu ya asilimia 55, lakini kama nilivyosema, mpaka kufikia 2050 huduma za Serikali kwa asilimia 80 zitatolewa kidijitali,” amesema Kikwete.

Ahadi hiyo ya Kikwete inakuja wakati Tanzania na dunia kwa ujumla ikishuhudia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yanayolazimisha baadhi ya huduma kutolewa kwa kutumia teknolojia hizo.

Ili kuitikia muelekeo wa dunia kiteknolojia, mwaka 2019 Tanzania ilianzisha Mamlaka ya Serikali Mtandao chini ya Sheria ya Serikali Mtandao Na.10 ya mwaka 2019.

Mamlaka hiyo ilianzishwa kwa malengo mbalimbali ikiwemo kuhakikisha usalama wa taarifa za Serikali, kuunganisha mifumo ya taasisi za umma, na kuwezesha utoaji wa huduma bora, rahisi na salama za Serikali kwa njia ya mtandao.

Huduma za kidigitali hadi vijijini

Kikwete piia amebainisha kuwa Serikali inaendelea kujipanga kufikisha huduma hizo za kidigitali hadi kwa wananchi wa vijijini kwa kujenga mifumo rahisi inayoweza kufanya kazi bila mtandao (offline).

“Mifumo hii hasa katika maeneo ambayo hayana mtandao tunayo ‘access’ ya ile ‘code’ yetu ambayo ni *152*00# yani hata kama ukiwa na simu ambayo sio simu janja, kama ambavyo unatuma pesa ndivyo ambavyo unaweza uka ‘access’ hizo taarifa,” amesema Kikwete.

Kikwete pia amesisitiza umuhimu wa mifumo ya Serikali na ile ya sekta binafsi kusomana, akirejerea msisitizo uliokuwa ukitolewa mara kwa mara na Rais Samia Suluhu ambaye alibainisha kuwa utekelezwaji wa agizo hilo ungepunguza uzembe na mianya ya rushwa.

“Mfanye ufuatiliaji kuhakikisha mifumo yote mipya iliyotengenezwa nayo inasomana na mifumo iliyopo… 

…Mifumo yetu ikisomana inapunguza gharama zisizo za lazima lakini pia inapunguza uzembe na kuziba mianya ya rushwa,” alisema Rais Samia akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa 15 wa Baraza la Biashara Tanzania (TNBC) Julai 29, 2024 jijini Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks