Wazee wanavyoweza kuyaepuka magonjwa ya akili
- Madarasa ya elimu ya watu wazima ni mbinu mojawapo ya kuepusha tatizo.
- Matatizo ya afya ya akili huwasababishia wazeevulemavu, utegemezi na hata vifo.
Dar es Salaam. Utimamu wa afya ya akili ni muhimu kwa ustawi wa watu wa rika zote. Watu wanapozeeka, baadhi ya mabadiliko hutokea kwenye maisha yao ikiwemo kupoteza kumbumbuku, magonjwa, vitu vinavyoweza kusababisha hisia mbaya, huzuni na upweke.
Mambo hayo na mengine yanaweza kuchangia mtu kupata ugonjwa wa akili.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, hadi Machi 2023, watu milioni 55 duniani kote wana magonjwa ya afya ya akili huku kila mwaka kesi mpya milioni 10 hutokea, kati ya wagonjwa hao, asilimia 60 wanaishi kwenye nchi za kipato cha chini na cha kati.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizungumza katika ufunguzi wa semina kwa wahariri wa vyombo vya habari katika maadhimisho ya wiki ya afya ya akili Oktoba 2022, alibainisha kuwa Tanzania ina watu takribani milioni saba wanaoishi na magonjwa ya akili.
Mwanasaikolojia wa kujitegemea, Jackline Kyambile ameiambia Nukta Habari kuwa magojwa ya afya ya akili ni matatizo ya ubongo ambayo humfanya mtu kuwa na hisia, fikra na matendo tofauti na yale yanayotarajiwa na jamii na kushindwa kukabiliana na changamoto za maisha.
Ugonjwa huu huchangiwa na sababu za kibaiolojia au kisaikolojia ambapo WHO wanabainisha kuwa magonjwa hayo huwaathiri zaidi wazee japo sio wote hupata athari zake kadri wanavyozeeka.
Sababu za magonjwa ya akili
WHO wanabainisha kuwa miongoni mwa sababu zinazoongeza hatari ya kupata magonjwa ya akili ni pamoja na umri mkubwa hususan zaidi ya miaka 65, shinikizo la damu, kisukari, kuwa na uzito mkubwa na unene kupita kiasi, uvutaji wa sigara, kunywa pombe kupita kiasi, kukosa mazoezi, mahusiano hasi na ya kijamii sambamba na huzuni.
“Ukiwa na mtazamo hasi wa kutopendwa, au kushindwa jambo fulani inasababisha kutojiamini, kutotambua umuhimu ulionao, ukatili, kutengwa na jamii au familia na kutoshiriki shughuli za uzalishaji,” amesema Kyambile
Kwa mujibu wa WHO magonjwa ya afya ya akili ni sababu ya saba ya vifo na moja ya sababu kuu za ulemavu na utegemezi kwa wazee ulimwenguni.
Soma zaidi
-
KANUNI YA 5: Mazoezi hayana mbadala kwa afya bora
-
Jinsi unavyoweza kuishinda sonona isiharibu maisha binafsi, kazi
Nini kifanyike?
Kulingana na utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Fronties in Aging Neurosience la nchini Switzerland umeonesha kuwa madarasa ya elimu kwa watu wazima yanaweza kuwa na manufaa katika kukabiliana na matatizo ya afya ya akili.
Utafiti huo umehusisha uchambuzi wa data za watu 282,421 ambao wameshiriki madarasa ya elimu ya watu wazima na kubaini wapo salama kwa asilimia 19 kutokupata magonjwa ya afya akili ikilinganishwa na ambao hawashiriki kabisa elimu hiyo.
Hii inaweza kuwa kwa sababu kujifunza mara zote kunachangamsha ubongo na kutoa fursa ya kushirikiana na wanajamii wengine na kuwawezesha wazee kuendelea kutoa mchango wa maendeleo kwenye jamii yao.
Hivyo elimu ya watu ya watu wazima inaweza kuwa njia nzuri ya kuwasaidia wazee kuepukana na magonjwa hayo.
Njia nyingine zinazoshauriwa na wataalamu wa afya ni uchunguzi wa mapema kwa mgonjwa ili kuanzishiwa mpango wa matibabu punde tatizo linapogundulika, dawa za hospitali na matibabu kwenye nyumba za upataji nafuu (sober house).
Pia kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na unywaji pombe kupita kiasi, kufanya mazoezi ya mwili, kushirikiana na wanajamii, kupata muda wa kupumzika na kufanya shughuli za kuingiza kipato.
Jackline Kyambile ameshauri Serikali na taasisi binafsi kutoa ushauri na mafunzo kwa watu wazima waliojiajiri au kuajiriwa juu ya namna ya kuishi maisha baada ya kustaafu ili wajiandae kiakili kukabiliana na chngamoto zinazoweza kujitokeza.

Kwa vijana wanaopitia sababu zinazoweza kusababisha matatizo haya wanatakiwa kuitambua thamani, uwezo na changamoto zao na kujitenga na watu au sehemu zinazowaweka kwenye hatari ya afya ya akili sambamba na kwenda kwa wataalamu wa saikolojia.
Latest
