Wawili wakutwa na Ugonjwa wa Homa ya Nyani (M-Pox) Tanzania
- Mmoja ni dereva wa magari ya mizigo aliyetoka nchi jirani kwenda Dar es Salaam.
- Wizara ya Afya yawataka Watanzania kujikinga kwa kuepuka kugusana kwa kupeana mikono, kubusiana, kukumbatiana au kujamiiana na mtu mwenye dalili za Mpox.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imebainisha uwepo wa Ugonjwa wa Homa ya Nyani (M-Pox) mara baada ya wahisiwa wawili kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na matokeo ya vipimo kuthibitisha hilo.
Taarifa ya Wizara ya Afya kwa umma iliyotolewa leo Machi 10, 2025 na kusainiwa na Waziri wake Jenista Mhagama imeeleza kuwa wizara hiyo kupitia mifumo yake ya ukusanyaji wa taarifa na ufuatiliaji wa magonjwa ilipokea taarifa za uwepo wa wahisiwa wenye dalili za vipele usoni, mikononi, miguuni na sehemu nyingine za mwili.
Taarifa hiyo inaongeza kuwa dalili hizo ziliambatana na homa, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, maumivu ya viungo vya mwili ikiwemo misuli na mgongo ambapo kati ya wahisiwa hao mmoja ni dereva wa magari ya mizigo aliyetoka nchi jirani kwenda Dar es Salaam.
“Baada ya kupokea taarifa za wahisiwa, sampuli zilichukuliwa na kupelekwa maabara ya Taifa kwa uchunguzi. Mnamo tarehe 9 Machi, 2025 uchunguzi wa kimaabara umethibitisha kuwa wahisiwa wawili (2) wana maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox.
Hivyo, hadi kufikia sasa jumla ya wahisiwa wawili (2) wamethibitika kuwa na ugonjwa wa Mpox nchini,” imebainisha taarifa ya Mhagama.
Hata hivyo, wizara hiyo imeeleza kuwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi na vituo vyote vya kutolea huduma za afya, inaendelea na ufuatiliaji, uchunguzi na utambuzi ili kubaini kama kuna wahisiwa wengine ili waweze kupatiwa huduma stahiki.
Chanzo cha ugonjwa huu ni wanyama jamii ya nyani, ambapo binadamu huweza kuupata kutokana na shughuli zinazoweza kusababisha kugusana na wanyama, majimaji au nyama za wanyama wenye maambukizi.
Aidha, endapo binadamu akipata maambukizi hayo anaweza kumwambukiza mtu mwingine kwa kugusana moja kwa moja.
Wizara ya Afya, imewahakikishia wananchi kuwa imejipanga kudhibiti ugonjwa huo na kutokana na uzoefu wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko ambapo inaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa katika ngazi zote, upimaji wa watu wanaoingia na kutoka kupitia mipaka ya nchi, kuimarisha utoaji wa elimu ya afya na kuhamasisha jamii ili kuwawezesha wananchi kuchuka hatua za kujikinga.
Jinsi ya kujikinga na Ugonjwa wa M-Pox
Aidha, Wizara ya Afya imewasihi na kuwasisitiza wananchi wote kuzingatia na kutekeleza afua za kujikinga na ugonjwa huo kutokana na kuwa hauna kinga kwa kuwahi katika kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu unapoona mojawapo ya dalili za ugonjwa wa Mpox au kupiga simu nambari 199 bila malipo.
Hatua nyingine ni pamoja na kuepuka kuchangia vitu kama nguo na matandiko ambavyo vimetumiwa na mtu mwenye dalili za Mpox, kuepuka kugusana kwa kupeana mikono, kubusiana, kukumbatiana au kujamiiana na mtu mwenye dalili za Mpox.
Mbinu nyingine ni kuepuka kugusa majimaji ya mwili ya mtu mwenye dalili za Mpox, kuepuka kumuhudumia mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa Mpox bila kuchukua taharadhari, watumishi wa afya kuzingatia kanuni za kujikinga na magonjwa wakati wote wanapowahudumia wagonjwa ikiwemo wenye dalili za vipele na homa na kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.
Katika taarifa hiyo Wizara ya Afya imetoa mwenendo wa Ugonjwa wa Marburg uliotangazwa kuwepo nchini Januari 20, 2025 ambapo mpaka sasa mwenendo wa udhibiti wa ugonjwa huo unaendelea vizuri na hadi kufikia leo tarehe 10 Machi 2025, zimetimia siku 41 bila kuwa na mgonjwa mpya.
Latest



