Tanzania yatangaza kumalizika kwa ugonjwa wa Marburg 

March 13, 2025 4:08 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya siku 50 tangu kuripotiwa kwa mgonjwa wa kwanza Januari 20 mwaka huu.
  • Serikali yatawataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.

Arusha. Wizara ya Afya Tanzania imeutangazia umma kumalizika kwa ugonjwa wa Marburg nchini ikiwa ni siku 50 tangu mgonjwa wa kwanza kuripotiwa mkoani Kagera, Magharibi mwa Tanzania.

Januari 20 mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg katika Mkoa wa Kagera, akibainisha mgonjwa mmoja kuathirika na ugonjwa huo.

Taarifa ya Jenista Mhagama, Waziri wa Afya iliyotolewa leo Machi 13, 2025 inabainisha kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kukidhi vigezo vya kitaalamu ikiwemo kutoripoti visa vipya ndani ya kipindi kirefu.

“Kitaalamu na kulingana na kanuni na taratibu za Shirika la Afya Duniani {WHO} tumekidhi vigezo vya kutangaza rasmi kumalizika kwa mlipuko wa MVD. Hivyo basi, leo tarehe 13 Machi, 2025, ninatangaza rasmi kumalizika kwa mlipuko wa MVD nchini,”amesema Mhagama.

Ugonjwa huo unamalizika nchini Tanzania kukiwa na jumla ya vifo 10, ikiwemo vifo nane vilivyoripotiwa na WHO na vifo viwili vilivyoripotiwa na Wizara ya Afya ingawa taarifa za Serikali hazikukubaliana na ile ya WHO kuhusu idadi ya vifo.

Mara ya kwanza ugonjwa huo uliripotiwa Machi, 2023 na kudumu kwa miezi miwili ukisababisha vifo vya watu sita kati ya tisa waliogundulika kuwa na virusi hivyo.

Hata hivyo, bado Tanzania ipo katika hatari ya magonjwa mengine ya mlipuko ikiwemo  Mpox  ambao tayari wizara hiyo imeshatangaza watu waili kuathirika pamoja na ugonjwa wa Ebola ulioripotiwa katika nchi jirani ambao bado unahitaji wananchi kuchukua tahadhari.

Kutokana na suala hilo, Mhagama amesisitiza jamii kuendelea kuwa makini hata baada ya kutangazwa kumalizika kwa mlipuko huu, kwa kuzingatia hatua zote za kujikinga, ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono (sanitizer), kutoa taarifa kwa wakati za uvumi au tukio lolote lisilo la kawaida katika jamii kupitia namba ya dharura 199 au kituo cha afya kilicho karibu.

Pamoja na hayo, Mhagama amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha wananchi wake na jumuiya ya kimataifa wanabaki salama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks