Wawekezaji waanza kutumia bandari ya Mwanza Kusini kusafirisha mizigo
- Ni baada ya bandari hiyo kufanyiwa ukarabati mkubwa.
- Itasaidia kuongeza wigo wa biashara na mapato Serikalini.
- Wafanyabiashara wasema njia hiyo ni rahisi kuliko barabara.
Mwanza. Huenda mapato ya bandari ya Mwanza Kusini iliyopo Ziwa Victoria yakaongezeka katika siku za hivi karibuni baada ya wafanyabiashara kuitumia kusafirisha mizigo katika nchi jirani ikiwemo Uganda na Kenya.
Miongoni mwa wawekezaji hao ambao wameanza kutumia bandari ya Mwanza Kusini ni kampuni ya Bakhersa ambayo husafirisha shehena mbalimbali za mizigo kwenda nchini Uganda.
Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Nicodemus Mushi amesema hayo ni mafanikio makubwa kwa TPA kurejesha huduma ya usafirishaji mizigo kwenye bandari hiyo.
“Ahadi yetu kwa watumiaji wa bandari ni kuwa tutaendelea kutoa huduma nzuri kwa wateja wapya na wa zamani lakini pia TPA inampango wa kuongeza wateja wengine wanaosafirisha shehena zinazopita kwenye bandari ya Mwanza,” amesema Mushi.
Mushi alikuwa akizungumza jana Julai 22, 2022 wakati wa kushusha shehena ya shayiri zaidi ya Tani 4,000 zinazosafirishwa kupitia bandari hiyo kwenda bandari ya Portbery Uganda.
Amesema wamefanikiwa kuboresha miundombinu ya bandari, vitendea kazi na wanafanya kazi kwa weledi hatua ambayo itaongeza mapato kwenye bandari hiyo.
Bandari kuu katika Ziwa Victoria ni pamoja na bandari ya Mwanza Kusini na Bandari ya Mwanza Kaskazini zilizounganishwa na barabara ya reli nchini na nchi za jirani.
Bandari hizo zina vifaa vingi vikiwemo mizani ya magari, matanki ya mafuta, karakana na mahali pa abiria na kusaidia shughuli mbalimbali ndani ya ziwa. Pia ziwa hilo lina bandari nyingine nyingi zinazoshirikiana kuwezesha huduma mbalimbali ndani ya Ziwa Victoria.
Zinazohusiana:
- Zanzibar, kitovu utengenezaji wa meli Afrika Mashariki
- Fundi mkuu wa kivuko cha Mv Nyerere aokolewa akiwa hai
- Meli mpya Ziwa Victoria kuchochea biashara Afrika Mashariki
Kaimu Meneja wa Bandari ya Ziwa Victoria, Vicent Suleiman amesema baada ya Serikali kuondoa kero ndogo ndogo ikiwemo kodi, hivi sasa wanapokea shehena nyingi za kusafirisha kwenda nje ya nchi.
Pia wamefanikiwa kukarabati magati na kuimarisha njia za bandari pamoja na kufanyia ukarabati na usimamizi umeimaarishwa.
“Baada ya kufanyia kazi changamoto ikiwemo kufunguliwa kwa milango na mahusiano baina ya nchi na nchi, hivi sasa usafirishaji wa mizigo kwa njia ya bandari umefikia asilimia 31 huku mapato yakipanda kwa asilimia 26 ukilinganisha na miaka ya nyuma,” amesema Suleiman.
Afisa Masoko kutoka kampuni ya Bakhresa, Hassan Mohamed amesema wameamua kutumia bandari hiyo baada ya baadhi ya changamoto kurekebishwa.
Amesema hiyo ni mara ya pili kwa kampuni hiyo kutumia bandari ya Mwanza Kusini kusafirisha bidhaa hizo ambapo kwa mara ya kwanza ilitumia kusafirisha tani 10,000 za sukari.
Latest