Ujio meli za mizigo kuchochea biashara Kanda ya Ziwa

February 6, 2023 8:20 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Wananchi waiomba Serikali ijenge meli kuwarahisishia usafiri wa mizigo ziwani.
  • Itasaidia kuokoa muda, kukuza biashara na mapato ya Serikali. 

Mwanza. Licha ya huduma za uchukuzi ndani ya Ziwa Victoria kuendelea kuimarika, suala la usafirishaji wa mizigo kwa njia ya meli bado ni changamoto.

Wakati Bandari ya Kanda ya Ziwa ilipoanzishwa mwaka 2006, ilikuwa na lengo la kuhudumia abiria milioni 1 kwa mwaka. Kiwango hicho pia kiliwekwa katika kusafirisha tani za mizigo.

Takwimu za Kampuni ya Huduma za meli mkoani Mwanza zinaonyesha kuwa hivi sasa ni meli nne zinafanya kazi ya kusafirisha abiria na mizigo ndani ya Ziwa Victoria ambazo zinaenda Bukoba (Kagera)  na Ukerewe mkoani Mwanza.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya uchukuzi, shehena za usafirishaji zimepungua licha ya usafiri huo kuwa nafuu kuliko barabara na ndege.

Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanasema iwapo hali hiyo itaendelea itasababisha kushuka kwa biashara na kuikosesha Serikali mapato kutoka katika kanda hiyo muhimu inayounganisha mataifa jirani ya Uganda na Kenya.

Hivi sasa, bandari za Ziwa Victoria zinategemea zaidi huduma za meli binafsi na zile zinazotoka nje ya nchi ambazo hata hivyo, idadi yake ni ndogo kulinganisha na mahitaji halisi.

Vyombo vya usafiri majini vyenye uwezo wa kubeba mzigo kuanzia tani 50 na kuendelea vilivyosajiliwa kutoa huduma ndani ya Ziwa Victoria kwa kipindi cha miaka 16 iliyopita ni 38 tu.

Leticia Lusato ni mfanyabiashara anayesafirisha bidhaa zake kutoka Mwanza kwenda Kampala Uganda na Bukoba mkoani Kagera amesema ukosefu wa usafiri wa uhakika ndani ya ziwa hilo siyo tu kunafifisha uchumi, bali pia ni kikwazo kwa huduma za dharura za afya kwa wakazi ukanda huo.

“Kwa mfano, kuna safari tatu pekee kwa siku kutoka Mwanza kwenda Bukoba huku safari za kwenda Uganda zipo mara moja moja hadi meli za kutoka huko zije Mwanza,” amesema Leticia.

Amesema usafirishaji wa mizigo imekuwa changamoto wakati mwingine shehena zinakuwa nyingi hivyo meli kushindwa kubeba mingine hali inayosababisha kutafuta usafiri mwingine wa anga au barabara ambao ni ghali.

Mwonekano wa meli ya Mv Butiama inayofanya safari zake kati ya Mwanza na Ukerewe. Hata hivyo, kukosekana kwa meli ya mizigo kumekuwa kukififisha biashara katika Kanda ya Ziwa. Picha| Mariam John/Nukta.

Tani moja ya mzigo husafirishwa kwa gharama za sh27,000 pekee.

Mfanyabiashara wa ndizi kati ya Bukoba na Mwanza, Christina Mshomi amesema hivi sasa anauza mkungu mmoja wa ndizi kati Sh35,000 hadi Sh50, 000 ili kumudu gharama na kupata faida kutokana na kulazimika kusafirisha mizigo yao kwa njia ya barabara.

“Wakati tukitumia usafiri wa meli kusafirisha mizigo tulikuwa tukiuza mkungu mmoja ndizi kati Sh15,000 hadi Sh20, 000,” amesema Mshomi.

Fabian Kaijage ambaye pia ni mfanyabiashara wa duka la rejareja mjini Bukoba amesema bei kubwa ya nauli na gharama ya usafirishaji inawalazimu kuuza bidhaa kwa bei ya juu kulinganisha na wanapotumia njia ya maji kuagiza bidhaa hizo.


Soma zaidi:

  • Wananchi waomba meli ya mwendo kasi Ziwa Victoria


Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi Edwin Soko amesema bandari za Ziwa Victoria zinakabiliwa na changamoto ya kupoteza mapato hali ambayo imechochewa na kushuka kwa shehena ya mizigo.

“Kutokana na changamoto hiyo, bandari bubu zinazotoza gharama kulingana na makubaliano kati yao na wasafirishaji badala ya viwango elekezi  siyo tu zinapunguza ufanisi wa bandari Kanda ya Ziwa, bali pia mapato ya Serikali,” amesema Soko.

Amesema bandari bubu hizo pia ni tishio kiusalama kwa sababu zinaweza kutumiwa kusafirisha au kuingiza bidhaa haramu zikiwemo zana haramu za uvuvi, wahamiaji na silaha.

Soko ameiomba Serikali kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa meli za mizigo ili kutoa unafuu kwa usafirishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Edmund Lutta amesema Serikali imetenga zaidi ya Sh113 bilioni katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya utekelezaji miradi 12.

Amesema kati ya miradi hiyo, minne ni mipya, mitano ni ya kufanyiwa ukarabati na mitatu inaendelea kutekelezwa.

“Katika miradi hiyo kiasi cha Sh53 bilioni zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi saba iliyoko katika Ziwa Tanganyika na Sh57 bilioni ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mitano ya utekelezaji wa miradi mitano iliyopo ndani ya Ziwa Victoria,” amesema Lutta

Ameainisha miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa meli ya mizigo ya Mv Umoja ambayo kwa sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 62 na Machi mwaka huu itaanza kufanya kazi.

Ujio wa meli hiyo utapunguza changamoto ya usafiri hasa wa mizigo na kuchochea ukuaji wa uchumi Kanda ya Ziwa.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV