Fundi mkuu wa kivuko cha Mv Nyerere aokolewa akiwa hai

September 22, 2018 2:43 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link

Idadi ya waliofariki katika ya kivuko cha Mv Nyerere imepanda na kufikia 166 huku mtu mmoja akipatikana akiwa hai asubuhi ya leo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe ameiambia Nukta kwa simu kuwa kasi hiyo ya upatikanaji miili hiyo na mtu huyo aliyehai umechochewa zaidi na kuongezeka kwa timu ya waokoaji katika eneo hilo la ajali.

Kamwelwe amesema kuwa kwa sasa hawawezi kuzungumzia zaidi suala la aliyepatikana hai kwa kuwa yupo chini ya uangalizi maalumu wa madaktari.

Mtu huyo aliyepatikana leo anafanya idadi ya waliokolewa wakiwa hai kufikia 41. Jana jioni (Septemba 21, 2018) wakati akilihutubia taifa, Rais John Magufuli alisema waliokolewa wakiwa hai walikuwa 40.

Redio ya Serikali TBC Taifa imeeleza kuwa mtu huyo aliyeookolewa anaitwa Augustino Charahani ambaye ni Fundi mkuu wa kivuko hicho. Charahani alikuwa miongoni mwa wafanyakazi wanane waliokuwa katika kivuko hicho. 

“Waokoaji wameingia hadi ndani ya kivuko hicho ndiyo maana tumefanikiwa kumpata mtu huyo akiwa hadi. Wamefanikiwa kufika hadi kwenye ‘engine room’ (chumba cha injini),” amesema Kamwelwe.

Amesema waokoaji wengi wanazidi kufika hapa kuongeza nguvu wakiwemo waliotolewa na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.

“Watanzania wanazidi kujitolea kwa kuwa wapo waokoaji ambao wamefika hapa kwa kujilipia ili kuhakikisha tunawaokoa wenzetu. Huu ni moyo mzuri sana,” amesema.


Zinazohusiana:


Amesema kuwa ili kuongeza ufanisi katika uokoaji, Serikali inapeleka vifaa vingine vya kisasa vitakavyosaidia kukibinua kivuko hicho ili kusaidia upatikanaji zaidi ya watu walionasa ndani.

Vifaa hivyo, amesema, vinatarajiwa kufika Ukara Saa 10 jioni na tayari vimeshaondoka Mwanza muda mrefu.

Waziri huyo amesema wataendelea na uokoaji hadi watakapojiridhisha kuwa wameokoa wote kwa kuzingatia idadi ya watu watakaokuwa wameokolewa.

Kuhusu kuhifadhi miili, Kamwelwe amesema utambuzi wa waliofariki unaendelea na baadhi wameshachukua miili ya ndugu zao kwa ajili ya kwenda kuihifadhi.

Kamwelwe ameeleza kuwa Serikali imejipanga vilivyo katika kuhifadhi miili ambayo bado haijatambuliwa na kwamba itashughulikia masuala yote ya masuala ya mazishi.

Enable Notifications OK No thanks