Watu mashuhuri 34 wapanda mlima Kilimanjaro kuchagiza utoaji wa chanjo ya Uviko-19
- Wanatoka taasisi za kimataifa watafika kileleni Oktoba 24.
- Lengo ni kuelimisha kuhusu haja ya haraka ya kuwa na usawa wa usambazaji wa chanjo dhidi ya Uviko-19.
- Fedha zitakazopatikana katika shughuli hiyo zitaongeza kasi ya utoaji chanjo.
Dar es Salaam. Wapanda mlima 34 leo wameanza safari ya kupanda mlima Kilimanjaro nchini Tanzania kama sehemu ya juhudi za kimataifa za kuchagiza upatikanaji wa chanjo ya Corona (Uviko-19) kwa wote.
Kundi hilo linalojumuisha watu kutoka katika nyanja za biashara, serikali, wanamichezo mashuhuri na wawakilishi wa vijana linatarajiwa kuwasili kwenye kilele cha mlima huo Oktoba 24, siku ya Umoja wa Mataifa (UN).
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), wapanda mlima hao kupitia mradi wa Kilimanjaro Initiative (KI) wanawakilisha tamaduni, uchumi, mazingira na mabara tofauti wakiwemo vijana 10 waliofadhiliwa kutoka miradi tofauti ya kijamii na shule za Tanzania na Kenya.
Pia wapo wanawake wanariadha nyota wa mbio za milimani, viongozi wa kisiasa, maafisa wa UN, madaktari, wanasayansi na wawakilishi wa vijana.
Lengo lao kubwa kupanda mlima huo mrefu kuliko yote Afrika ni kuelimisha kuhusu haja ya haraka ya kuwa na usawa wa usambazaji wa chanjo dhidi ya Uviko-19.
Fedha zitakazopatikana wakati wa kupanda mlima zitakwenda kwenye mfuko wa Muungano wa Afrika (AU) wa kupambana na Uviko-19 na kampeni ya Go Give One inayosimamiwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa (WHO).
Fedha hizo zitatumika kutoa chanjo za Uviko-19, huku kipaumbele kikitolewa kwa wanaozihitaji zaidi katika nchi ambazo haziwezi kumudu chanjo hiyo.
Mwanzilishi wa Kilimanjaro Innitiative (KI) iliyoandaa upandaji mlima huo, Tim Challen akimkunuu Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Ghebreyesus amesema “Kuelimisha kuhusu changamoto ya kutokuwepo haki ya upatikanaji wa chanjo ni muhimu ili kuleta suluhusho lenye usawa.
“Lazima tushirikiane kama familia ya kimataifa kupambana na Uviko-19. The Big Climb inawakilisha mchango wetu katika juhudi hizi za pamoja.”
Madaktari wengine watatu kutoka India, Marekani na kundi la utafiti la ISGlobal wanashiriki katika kampeni hiyo sanjari na mwanariadha Mira Rai kutoka Nepal ambaye ni balozi mwema wa UN wa ushirikiano wa milima na Akinyi Obama-Manners akiwakilisha vijana kutoka wakfu wa Auma Obama Sauti Kuu nchini Kenya.
Wadau wengine katika kampeni hiyo ni FAO mountain partnership, mfuko wa Benki ya Umoja wa Mataifa (UNFCU), Kituo cha Afrika cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa (CDC) na Muungano wa Chanjo Duniani (GAVI).
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Latest
