Mpishi wa watalii Tanzania mwenye matumaini lukuki
Mariam Rashidi (42), mpishi wa chakula cha watalii mkoani Kilimanjaro ambaye ana matumaini makubwa katika biashara yake baada ya kuimarika kwa utalii. Picha| Daniel Mwingira.
- Amefanya biashara ya kundaa vyakula vya watalii mbugani kwa takribani miaka 17
- Amesema matumaini ya kufanya biashara kwa sasa ni makubwa kutokana na ujio wa chanjo.
Moshi. Ni miongoni mwa wajasiriamali wenye matumaini makubwa ya kufaidika na biashara yake siku zijazo.
Matumaini hayo ni kwa sababu ya kuanza kuimarika kwa sekta ya utalii Tanzania ambayo iliathiriwa na janga la Corona tangu ilipoingia nchini Machi 2020.
Huyo ni Mariam Rashidi (42) anayefanya kazi ya kuuza chakula cha watalii maarufu kama “lunch box” mkoani Kilimanjaro ambacho hutumiwa na watalii wanaotembelea hifadhi za Taifa zikiwemo za Serengeti, Kilimanjaro na Ngorongoro.
Mariam, ambaye biashara hiyo ameifanya kwa miaka 17 sasa, anasema baada ya hatua mbalimbali kuchukuliwa dhidi ya Uviko-19 ikiwemo utoaji chanjo na kulegezwa kwa masharti ya safari za kimataifa, ameanza kupata wateja katika biashara yake.
“Kwa sasa hivi na uko nyuma ni tofauti. Huko nyuma wakati Uviko-19 ilipoanza biashara ilikuwa ngumu sana ulikuwa huoni hata mgeni mmoja angalau sasa hivi kuna unafuu sana sikosi chakula cha wageni 50 au 70 nikikosa sana wageni 30,” anasema Mariam.
Anasema elimu ya kujikinga na ugonjwa huo pamoja na utoaji wa chanjo umesaidia watalii kuanza kuingia nchini hasa katika maeneo ya utalii, hivyo kuwajengea ujasiri wafanyabiashara wadogo wadogo wanaotegemea utalii kujiingizia kipato.
“Tulipata elimu kwa mkuu wa mkoa mara kwa mara na hata hili lilipokuja suala la chanjo tumeshaweka kikao tumekubaliana lazima kila ambaye yuko kwenye hii sekta lazima apate chanjo anayetaka,” anasema Mariam anayefanya biashara hiyo pembezoni mwa barabara ya kutoka Moshi kwenda Arusha.
Utalii ni miongoni mwa sekta ambazo ziliathiriwa zaidi na ugonjwa wa Uviko-19 na kusababisha watu kupoteza ajira na Serikali kupoteza mapato kutokana kuzuiliwa kwa safari za kimataifa.
Zinazohusiana
- Watalii waruhusiwa kuingia Italia, Ulaya ikiwaonya raia wake
- Sanamu zinazohusishwa na ubaguzi wa rangi zaendelea kung’olewa duniani
- Tanzania yazindua filamu kutangaza utalii kimataifa
Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii idadi ya watalii wanaoingia nchini ilishuka hadi watalii 620,867 mwaka 2020 ikilinganishwa na watalii milioni 1.5 wa mwaka 2019 sawa upungufu wa zaidi ya nusu ya watalii ndani ya mwaka mmoja.
Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO) limeeleza kuwa idadi ya watalii wa kimataifa ilipungua kwa asilimia 73 kwa mwaka 2020, huku kwa miezi mitano ya mwanzo ya mwaka 2021, watalii wamepungua hadi milioni 147 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2020.
Hata hivyo, UNWTO imesema sekta ya utalii duniani itaimarika kwa asilimia 60 ifikapo mwaka 2022, huku Afrika, sekta hiyo ikitarajiwa kuimarika kwa asilimia 73 kutokana hatua mbalimbali za kimataifa kupambana na ugonjwa huo.

Safari bado ndefu
Licha ya matumaini aliyonayo mwanamke huyo, bado biashara yake haijaimarika ikilinganishwa kabla ya Uviko-19 kuingia nchini ambapo alikuwa ana uwezo wa kuuza sahani chakula katika ya sahani 150 hadi 300.
Akisimulia hali ilivyokuwa mwaka jana alipofunga biashara yake, aliyeathirika siyo yeye peke yake bali hata wafanyakazi wake wapato 12 waliathirika kwa kuwa vipato vyao vilishuka kutokana na kutokuwepo biashara.
Hali hiyo ilimradhimu kupunguza kipato cha kuwalipa wafanyakazi wake na hata kumfanya abuni mbinu nyingine ya kusambaza vyakula kwenye maofisi wakati wa mchana ili mradi tu waaweze kupata kipato cha kujazia hadi sasa ambapo hali imenza kurejea kidogo.
Kwa sasa, anasema, anauza sahani anauza chakula cha wageni 70 au 50 na akikosa sana ni wageni 30 kiasi cha kumuingizia kipato kidogo tofauti alipokuwa hafanyi kabisa biashara.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Latest