Watano mbaroni mauaji ya ndugu wa familia moja Mwanza

January 24, 2022 8:47 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhan Ng’anzi  akionyesha vielelezo vya mali ya marehemu ikiwemo simu zilizokamatwa nyumbani  kwa watuhumiwa. Picha| Mariam John.


  • Waliuawawa Januari 18 na kutupwa kando ya mtoto.
  • Polisi yawashilia watu watano kwa uchunguzi.
  • Mgogoro watajwa kuchangia mauaji hayo.

Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikiliwa watu watano wanaotuhumiwa kutekeleza mauaji ya wanawake watatu wa familia moja wakazi wa mtaa wa Mecco Kusini mkoani Mwanza huku chanjo cha vifo hivyo vikitajwa kuwa ni mgogoro wa biashara.

Marehemu hao ambao ni Marry Charles (42) mfanyabiashara mkazi wa mecco, Jenifa Fred (22) mkulima ambaye ni mtoto wa marehemu, pamoja na mfanyakazi wao wa ndani Monica Jonas (19) waliuawawa Januari 18, 2022 saa 5:30 usiku kisha miili yao kutupwa kando ya mto Jellys nyuma ya Kituo cha Afya Buzuruga.

Marry ameacha mtoto wa mwaka mmoja huku binti yake  Jenifa akiacha mtoto wa mwezi mmoja. Miili ya marehemu ilizikwa kijijini kwao Bomani, Wilaya ya Sengerema siku ya Ijumaa Januari 21, 2022.

Waliokamatwa kwa mauaji hayo ni Thomas Songay (26) mkazi mtaa wa Utemini-Buhongwa pamoja na mke wake Hajir Thomas (23) fundi cherehani ambaye alitekeleza mauaji hayo.

Wengine ni Deoglas Malengwa (31) muuza duka la vifaa vya umeme mkazi wa Buhongwa, Emmanuel Lugaila (36) mfanyakazi katika mgodi wa Mwandui mkazi wa Mecco Kusini na Emmanuel Mathew (19), mkazi wa Buhongwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhan Ng’anzi akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 24, 2022 amesema marehemu alikuwa akijishughulisha na biashara ya kuuza nafaka na kwamba alikuwa akitumia familia ya watuhumiwa kuagiza mzigo Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

“Inadaiwa mara ya mwisho marehemu alimpa mtuhumiwa kiasi cha fedha ambacho hakijajulikana kwa ajili ya kumuagizia mzigo, matokeo yake mzigo haukuletewa na katika kudaiana ndipo mtuhumiwa ambaye ni Hajir Thomas akishirikiana na wenzake aliweza kwenda kufanya mauaji hayo,” amesema Kamanda Ng’anzi.


Soma zaidi:


Pamoja na kutekeleza mauaji hayo, pia watuhumiwa waliweza kukutwa na vielelezo mbalimbali ambavyo ni mali ya marehemu zikiwemo simu janja mbili, televisheni mbili , Radio mbili, jiko la gesi aina ya Nikle, friji aina ya Kyoto na godoro.

Kamanda Ng’anzi amesema pia watuhumiwa hao walikutwa na silaha aina ya panga iliyotumika kwenye mauaji hayo ambayo ipo chini ya uangalizi wa jeshi la polisi. 

Amesema kwa sasa silaha hiyo imepelekwa kwa mkemia mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuoanisha vinasaba vya damu iliyopo kwenye panga na za marehemu.

“Baada ya kufanya mahojiano watuhumiwa walikiri kutekeleza mauaji hayo na kuchukua mali hizo huku simu wakizichimbia kwenye eneo walipokuwa wanaishi mtaa wa Buhongwa jijini Mwanza,” amesema Ng’anzi.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wanaohusika katika tukio hilo  ili wauanganishwe na wenzao huku likitoa onyo kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kuwa hawatoweza kukwepa mkono wa sheria.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW