Watalaam wa sekta wavyoweza kuitumia tathmini mpya ya mabadiliko ya hali ya hewa

March 3, 2022 1:26 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • TMA: Wataalam wa sekta fuatilieni tathmini mpya ya hali ya hewa
  • Ni tathmini inayoangazia mambo muhimu ya hali ya hewa kwa mwaka 2022.
  • Tathmini hiyo hutolewa na jopo la Kiserikali la Tathmini ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC).  
  • Inasaidia kufanya maamuzi ikiwemo kukabiliana na athari za hali mbaya ya hewa.

Dar es Salaam. Wataalam katika sekta mbalimbali wameshauriwa kufuatilia taarifa mpya ya tathmini ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani iliyotolewa wiki hii itakayowasaidia kuchukua hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame na mvua kubwa.

Tathmini ya mabadiliko ya hali ya hewa kuhusiana na athari na uhimilivu wa mabadiliko ya hali ya hewa ilitolewa Februari 28, 2022 na jopo la Kiserikali la Tathmini ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC).  

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk Agnes Kijazi akitoa  taarifa ya klimatolojia ya hali ya hewa kwa mwaka 2021 leo jijini Dar es Salaam amesema  tathmini hiyo ina mambo muhimu ambayo yakiwafanyiwa kazi yatasaidia kupunguza athari za hali mbaya ya hewa inayoweza kujitokeza mwaa huu.

“Mabadiliko ya hali ya hewa yanayojumuisha kuongezeka kwa idadi na ukubwa wa matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo ukame na mvua kubwa yameendelea kusababisha athari na madhara makubwa ikiwemo vifo, uharibifu wa miundombinu na upotevu wa mali,” amesema Dk Kijazi.

Amesema ongezeko la joto ambalo linatarajiwa kufikia nyuzi joto 1.50C hivi karibuni (2021 – 2040) litazidi kusababisha athari na madhara makubwa zaidi  kwa jamii,  viumbe hai na mfumo mzima wa ikolojia. 

Pia uwezo wa kuhimili changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa utakuwa mashakani zaidi endapo ongezeko la joto litazidi nyuzijoto 1.50C.


Soma zaidi: 


Aidha, amesema ipo mikakati mbalimbali inayoweza kutumika ili kupunguza athari na kuimairisha uwezo wa kuhimili changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.  

“Kwa hapa Tanzania baadhi ya Mikakati hiyo ni pamoja kuimarisha miundombinu (SGR), ujenzi wa bwawa la Nyerere kwa ajili ya kufua umeme (Megawatt 2,115), upandaji miti na utunzaji mazingira, elimu na kuimarishwa kwa huduma za hali ya hewa,” amesema Dk Kijazi.

Amesema wananchi wapatiwe taarifa na elimu ya matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa zinazotolewa na mamlaka hiyo ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli zao na pia kusaidia kupunguza majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa.

Taarifa ya Klimatolojia huandaliwa kila mwaka ambapo imekuwa na mchango mkubwa kwa jamii na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa ajili ya kuweka mipango na vipaumbele dhabiti vya kukabiliana na athari za  matukio ya hali mbaya ya hewa. 

Mwaka wa 2021, Tanzania ilikumbwa na matukio ya hali mbaya ya hewa hususan mvua kubwa zilizoambatana na mafuriko na upungufu wa mvua katika baadhi ya maeneo, joto pamoja na upepo mkali na kuathiri maisha ya watu, mimea na wanyama.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

Nukta TV

Top 10 ya magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Top 10 ya magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Nukta TV

SGR yaingizia Serikali Sh169.37 bilioni tangu kuanza kwa safari Juni 2024

SGR yaingizia Serikali Sh169.37 bilioni tangu kuanza kwa safari Juni 2024

Nukta TV