Watahiniwa milioni 1.3 darasa la saba kikaangoni kesho
- Watafanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi Septemba 13 na 14, 2023.
- Wanafunzi waonywa kujihusisha na vitendo vya udanganyifu.
Dar es Salaam. Watahiniwa milioni 1.3 wa Tanzania Bara wanatarajia kuanza mtihani wa kumaliza elimu ya msingi waliyoianza miaka saba iliyopita huku wakionywa kuepuka udanganyifu.
Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limesema mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi (Primary School Leaving Examination PSLE) itafanyika kwa siku mbili kati ya Septemba 13 na 14, 2023.
Katibu Mtendaji wa Necta Dk Said Ally Mohamed amesema kati ya watahiniwa hao, 742,718 sawa na asilimia 53.15 ya waliosajiliwa ni wasichana.
“Watahiniwa 1,334,269 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 63,101 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia,” amesema Dk Mohamed katika taarifa iliyotolewa leo Septemba 12, 2023.
Dk Mohamed amesema kuwa watahiniwa wenye mahitaji maalum waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni 4,583, ambapo kati yao, 101 ni wasioona, 1,321 wenye uoni hafifu, 1,125 wenye uziwi, 549 ni wenye ulemavu wa akili na 1,487 ni wenye ulemavu wa viungo.
Soma zaidi
-
Miongozo mipya elimu maalum kuongeza ujumuishi Tanzania
-
Wazee wanavyoweza kuyaepuka magonjwa ya akili
-
KANUNI YA 5: Mazoezi hayana mbadala kwa afya bora
Watahiniwa hao watafanya mtihani huo katika masomo sita ambayo ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Teknolojia (Science and Technology), Hisabati (Mathematics), Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi (Social Studies and Vocational Skills) pamoja na Uraia na Maadili (Civics).
Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ni muhimu kwa wanafunzi kwa kuwa hupima maarifa na umahiri wa wanafunzi kwa yale waliyosoma katika ngazi hiyo. Pia ni daraja muhimu la kujiunga na elimu ya sekondari.
Weledi uzingatiwe
Aidha, Necta imewataka wasimamizi wa mtihani huo kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa kuzingatia weledi na miongozo iliyowekwa ili kila mtahiniwa kupata matokeo anayostahili.
Itakumbukwa mwaka 2022, Serikali iliifungia shule ya Chalinze baada ya kuripotiwa vitendo vya ubadhirifu ambapo watahiniwa saba walibadilishiwa namba za mitihani yao kinyume na taratibu.
“Wasimamizi wahakikishe watahiniwa wenye mahitaji maalum wanafanya mitihani yao ipasavyo ili wapate haki yao ya msingi, haki hizo ni pamoja na kuwapa mitihani yenye maandishi ya nukta nundu kwa watahiniwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa watahiniwa wenye uoni hafifu,” imeeleza taarifa ya Necta.
Necta wamewataka wasimamizi kuwaongezea muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la Hisabati na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine kwa watahiniwa wenye mahitaji maalum.
Hata hivyo, jamii imetakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kuheshimu na kuhakikisha utulivu katika maeneo yote ambayo mitihani itafanyika huku wanafunzi wakitakiwa kuepuka vitendo vya udanganyifu kwa kuwa vinaweza kusababisha wao kufutiwa matokeo yao yote.
Mwaka 2022 watahiniwa 2,194 wa shule ya msingi walifutiwa matokeo yao huku shule 24 zikifungiwa kuwa vituo vya mitihani kutokana na kubainika kufanya vitendo vya udanganyifu.