Watahiniwa 572,378 wa kidato cha nne, kikaangoni leo
- Waonywa kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu.
- Wakuu wa shule, wamiliki, wapewa angalizo kuwaingilia wasimamizi.
- Wenye mahitaji maalumu kuongezewa muda zaidi.
Dar es Salaam. Jumla ya watahiniwa 572,378 waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Kuhitimu Elimu ya Sekondari (CSEE) wameanza kufanya mitihani hiyo leo Novemba 13, 2023 huku wakionywa kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu.
Mtihani wa kidato cha nne hupima umahiri wa wanafunzi kwa yale waliyojifunza kwa miaka minne kuanzia kidato cha kwanza, na matokeo yake hutumika kuchagua wanafunzi wanaojiunga na kidato cha tano au vyuo mbalimbali.
Soma zaidi : Shule 10 bora matokeo ya kidato cha nne 2022 hizi hapa
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dk. Said Mohamed, aliyekuwa akizungumza na wanahabari Novemba 12, 2023 amebainisha kuwa kati ya watahiniwa hao 543,386 ni wa shule.
“Kati ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa mwaka huu wavulana ni 250,237 sawa na asilimia 46 na wasichana ni 293,149 sawa na asilimia 54,” amesema Dk. Said.
Hata hivyo, pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wasichana waliosajiliwa kufanya mitihani wa jinsia ya kike, idadi ya wanaojiunga na kidato cha tano mpaka vyuo kikuu huwa inapungua ukilinganisha na ile ya shule ya msingi mpaka kidato cha nne.
Kamati za mitihani, wasimamizi waonywa
Dk. Said ametoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri, kuhakikisha usalama wa vituo vya mitihani unaimarishwa na vinatumika kwa mujibu wa kanuni zilizotolewa na NECTA.
“NECTA inatoa wito kwa wale wote walioteuliwa kusimamia mtihani huu, kufanya kazi yao kwa umakini, weledi, uadilifu wa hali ya juu na kwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mtahiniwa apate haki yake,” amesema Dk. Mohamed.
Aidha, Dk. Mohamed ameongeza kuwa wasimamizi wa mitihani wanatakiwa kuwaongezea muda wa dakika 20 kwa kila saa katika mtihani wa hesabu na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo megine watahiniwa wenye mahitaji maalumu ili nao wapate haki sawa na wengine.
Soma zaidi : Yakufikirisha shule ya Twibhoki matokeo kidato cha nne 2022
Angalizo kwa watahiniwa
Watahiniwa wa CSEE wamekumbushwa kuzingatia sheria na kanuni za mitihani na kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu wakati wote wa mitihani kwa kuwa NECTA itawachukulia hatua kali za kisheria.
“NECTA haitarajii kuona mtahiniwa anajihusisha na vitendo vya udanganyifu, kwani kwa kufanya hivyo matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mtihani,” amesems Dk. Mohammed.
Mwaka 2022, watahiniwa 333 walifutiwa matokeo ya kidato cha nne kwa kufanya vitendo vya udanganyifu ambapo kati yao mmoja alikuwa mtahiniwa wa mtihani wa maarifa.
Aidha, wamiliki na wakuu wa shule wametakiwa kutowaingilia wasimamizi wa mitihani wakati wote watakapokuwa wanatimiza majukumu yao, kwa kuwa kwa wakati huo shule zao ni vituo maalumu vya mitihani.