Yakufikirisha shule ya Twibhoki matokeo kidato cha nne 2022

February 2, 2023 1:08 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Yashika nafasi ya saba kitaifa katika matokeo hayo.
  • Wanafunzi 66 kati ya 67 wafutiwa matokeo.
  • Mwanafunzi mwenye matokeo amepata daraja la kwanza la pointi nane.
  • Necta yasema udangajifu umeiponza shule hiyo. 

Dar es Salaam. Wakati uongozi wa Shule ya Sekondari Twibhoki ya mkoani Mara ikishingilia kutokana na matokeo mazuri ya kidato cha nne iliyopata, wazazi na wanafunzi 66 wa shule hiyo kwao ni huzuni. 

Shule hiyo imefanya maajabu baada ya kushika nafasi ya saba kitaifa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka 2022. Licha ya ushindi huo, shule hiyo inaacha maswali mengi yasiyo na majibu.

Katika matokeo ya shule hiyo  yaliyochapishwa katika tovuti ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) yanaonyesha wanafunzi 67 ndiyo waliosajiliwa na kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka jana.

Athumani Amas ambaye ni Kaimu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), ameiambia  Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kati ya wanafunzi hao, 66 wamefutiwa matokeo kwa sababu wamefanya udanganyifu.

Kwa mujibu wa Necta, ni mwanafunzi mmoja tu mwenye matokeo aliyepata daraja la kwanza la pointi nane na kuivusha shule hiyo.

“Matokeo yao yamefutwa sio yamezuiliwa, yamefutwa kwa sababu wamefanya udanganyifu,” amesema Amas.


Zinazohusiana: 


Wanafunzi hao 66 waliofutiwa matokeo ni sawa na asilimia 20 ya wanafunzi 333 ambao wamefutiwa matokeo katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022. 

Hiyo ni sawa na kusema kwa kila wanafunzi 10 waliofutiwa matokeo, wawili wanatoka katika shule hiyo iliyopo Kanda ya Ziwa. 

Itakumbukwa alipokuwa akitangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka 2022, Amas aliwaambia wanahabari kuwa Necta imefuta matokeo ya watahiniwa 333 ambao walibainika kufanya udanganyifu katika mtihani.

Watahiniwa hao waliofutiwa matokeo kutokana na udanganyifu wanaweza kufanya tena mtihani wa kidato cha nne kama watahiniwa binafsi kwa kutumia namba zao walizopata mwaka 2022.

Kinachoweza kuwashangaza wengi ni kuwa licha ya watahiniwa 66 wa shule hiyo kufutiwa matokeo yao, Twibhoki imeingia katika orodha ya shule 10 zilizofanya vizuri kitaifa kwa kushika namba saba kwa kuzingatia kigezo cha wastani wa ufaulu (GPA). 

Licha ya shule hiyo kupata majanga mwaka 2022, imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne ambapo mwaka juzi ilishika nafasi ya 49 kitaifa. Kati ya wanafunzi 80 waliofanya mtihani huo mwaka huo, 69 walipata daraja na kwanza na 11 walipata daraja la pili.

Mwaka 2020 ilishika nafasi ya 33 ambapo ilipanda kutoka nafasi ya 45 kitaifa mwaka 2019.

Enable Notifications OK No thanks