Wataalamu: Haya yatasaidia wanawake wengi kujitokeza chanjo ya Uviko-19 Tanzania

September 1, 2021 1:37 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Takwimu zinaonyesha wanawake wapo nyuma kwenye zoezi la kupata chanjo.
  • Wataalamu waeleza kuwa wanawake wengi hawana taarifa sahihi kuhusu kinga hiyo. 
  • Wanawake washauriwa kutumia vyanzo rasmi kupata habair ili kukwepa habari potofu. 

Dar es Salaam. Licha ya Serikali na wadau wa afya kuhimiza Watanzania kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona (Uviko-19), watu waliopata chanjo hiyo Tanzania bado haijafikia hata nusu ya chanjo zilizoingizwa nchini huku wanaume wakijitokeza zaidi kuchanjwa. 

Mwishoni mwa Julai, Tanzania ilipokea dozi zaidi ya milioni moja za chanjo ya aina ya Johhson and Johnson inayotengeneza nchini Marekani. Rais Samia Suluhu Hassan alizindua chanjo hiyo mwishoni mwa mwezi huo na kufuatiwa na kampeni rasmi ya kuchanja mapema Agosti mwaka huu. 

Ndani ya mwezi mmoja tangu Rais Samia azindue chanjo hiyo, tathmini ya utoaji wa chanjo iliyotolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof Abel Makubi inaonyesha kuwa hadi Agosti 28, 2021, watu 304,603 walikuwa wamepatiwa chanjo. 

Kiwango hicho cha waliopatiwa chanjo ni sawa na asilimia 30 au takriban theluthi ya dozi zote zilizoingizwa Tanzania.

Watu waliochanjwa hadi Agosti 28 ni sawa na asilimia 0.5 tu ya idadi ya watu Tanzania inayokadiriwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuzidi watu milioni 59.4 mwaka huu. 

Serikali imepanga kutoa chanjo kwa asilimia 60 ya watu nchini. Hii ina maana kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha watu sita kwa kila 10 nchini wamepata chanjo ya Uviko-19. 

Baadhi waikwepa chanjo ya corona wakiihusisha na ugumba wa mbeleni, Picha| Cedars.

Wanawake wabaki nyuma chanjo ya Uviko-19

Katika takwimu mpya zilizotolewa na Prof Makubi, kati walengwa 304,603 waliopatiwa chanjo, wanaume wameonekana kuitikia wito zaidi na kuwaacha wanawake nyuma jambo ambalo wadau wa afya wanasema wanatakiwa kuhamasishwa zaidi ili kujikinga na Uviko-19. 

Kwa mujibu wa takwimu hizo, hadi Agosti 28 mwaka huu, wanawake 103,127 sawa na asilimia 33.9 ya watu wote waliochanjwa ndiyo wamejitokeza kupata kinga hiyo.  Idadi ya wanaume waliopata chanjo Tanzania ni takriban mara mbili ya wanawake. 

“Watoa huduma wote, waendelee kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo kwa kila mteja watakaye mhudumia kwa magonjwa mengine ili kumpa nafasi ya uelewa na baadae yeye kuchukua maamuzi sahihi juu ya chanjo,” amesema Prof Makubi.

Nini kinawakwamisha wanawake kupata chanjo ya Uviko-19

Baadhi ya wadau wana hofu kuwa mwitikio hafifu wa wanawake huenda ni matokeo ya habari za uzushi juu ya madhara ya chanjo ambayo yamechochea baadhi ya watu kuamini taarifa zisizo sahihi.

Mtaalamu wa Afya kutoka Hospitali ya Hindu Mandal Dar es Salaam, Dk Frank John ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa Tanzania ina wanaume wengi walioelimika ikilinganishwa na wanawake jambo linalowapatia wanaume uwezo wa kupata taarifa sahihi na hata wanapofikiwa na habari za uongo ni rahisi kufahamu mahali pa kuthibitisha. 

“Wengi waliaminishwa njia ambazo zilitumika awali kuwa suluhu ya Corona ikiwemo kujifukiza na tiba asilia ambazo zilitangazwa na kuuzwa. Kuwahamisha na kuwaeleza kuwa chanjo nayo inasaidia, inahitajika elimu kubwa sana kutolewa kwa sasa,” amesema Dk John.

Daktari huyo anasema kwa dozi zilizoingizwa nchini wengi walitarajia zingeisha mapema na kuletwa nyingine ili kuwakinga watu wengi zaidi “lakini hadi sasa ni watu wachache ndio wamejitokeza.”

Uzushi unawanyima wanawake fursa ya kinga

Wataalamu wanaeleza kuwa uzushi kuwa chanjo ya Uviko-19 zina madhara kwa afya ya uzazi kwa wanawake si za kweli kwa kuwa hadi sasa hakuna ushahidi wa kisayansi kuthibitisha na kuwataka wanawake kuondoa hofu. 

Mtaalamu wa masuala ya afya ya uzazi na Virusi Vya Ukimwi (VVU), Dk Lilian Benjamin amesema hadi sasa hazijaripotiwa taarifa zozote za kuwepo kwa mama mjamzito, mwanamke na hata mama anayenyonyesha kupata changamoto kutokana na chanjo ya Corona.  

Chanjo ya Corona haiathiri vinasaba wala uzazi

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Shadrack Mwaibambe ameiambia Nukta kuwa wanawake wengi walio kwenye umri wa kujifungua, wanaogopa kupata chanjo wakihofia kuwa chanjo itawapatia ugumba mbeleni, dhana isiyo ya kweli.

Mtaalamu huyo amesema chanjo dhidi ya Corona haina madhara yanayodhaniwa na wataalamu wa afya hawawezi kuruhusu itolewe kama itaathiri nguvu kazi ya taifa.

“Kama miaka mitatu iliyopita kuna chanjo dhidi ya Saratani ya shingo ya kizazi iliyokuwa ikitolewa nchini Kenya na ilikuwa na changamoto, ilipotaka kuja Tanzania “ilipigwa stop” na haikutolewa. Elimu inahitajika kuelimisha kuwa chanjo hii haina shida,” amesema Dk Mwaibambe.

Wanaume wachakarikaji zaidi

Baadhi ya wadau wameeleza kuwa Tanzania wanaume wana shughuli nyingi zikiwemo biashara za kuvuka mipaka huenda ni moja ya sababu zilizofanya wajitokeze zaidi kuchanja kuliko wanawake. 

“Mwanaume ndiye anayetoka kwenda kutafuta, huenda wengi wameona wachanje mapema ili kujikinga na Corona na kuzilinda familia. Wanawake huenda hawaoni sababu ya kufanya hivyo kwa kuwa wanafanya shughuli zao nyumbani au karibu na nyumbani,” amesema  Dk Brendavida Kaseko  daktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Tumbi mkoa wa Pwani.

Mtaalamu huyo wa afya anakiri kuwa hata kwenye kituo chake cha kazi wanaume wengi wamejitokeza kuchanja kuliko wanawake.

Elimu zaidi inatakiwakutolewa kwa wanawake ili wajitokeze kupata chanjo. Picha| CDC. 

Njia zitakazosaidia kuongeza mwitikio wanawake kupata chanjo

Ili kuhakikisha wanawake wengi zaidi wanapata chanjo hiyo ya Uviko-19, wadau wa afya wanashauri wanawake kupata taarifa sahihi zitakazofanya wafanye uamuzi sahihi badala ya kuzingatia uzushi. 

Mraghabishi wa masuala ya kijinsia, Innocent Grant ameiambia Nukta kuwa wanawake wanatabia ya kusimuliana mambo na kwa wengi hicho ni chanzo chao cha taarifa bila kuthibitisha ukweli wake hivyo elimu ya kupata habari sahihi itaongeza mwitikio. 

Grant amesema inabidi kuondoa mwanya wa upatikanji taarifa kati ya wanawake na wanaume na kukabiliana na vyanzo vinavyotoa taarifa zisizosahihi. 

“Wanawake ndio wahudhuriaji wazuri kanisani kuliko wanaume, endapo viongozi wa dini wataelimishwa kutoa elimu nzuri ya chanjo, itakuwa rahisi kwao kupata taarifa sahihi,” amesema Grant akiwashauri waandishi wa habari pia kuipatia elimu ya chanjo uzito kama iilivyo kwenye unyanyasaji wa kijinsia na mengineyo.

Dk John amesema, badala ya kufanya mtu anayekataa chanjo kama mtu anayekosea jamii, kuna umuhimu wa kuwepo midahalo ya wazi kwa ajili ya kujibu maswali yote waliyonayo wananchi na siyo kuishia kuwapa taarifa tu.

Serikali imeeleza kuwa inaendelea kutoa elimu kwa jamii hivyo inashauri wanawake kujitokeza kwa wingi kupata chanjo kwa kuwa ni salama.

“Wizara inaendelea kutoa elimu kwa jamii kwa kupitia majukwaa mbalimbali. Wanawake wahakikishe wanapata taarifa sahihi na wajitokeze kupata chanjo,” Catherine Sungura, Msemaji wa Wizara ya Afya ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz). 

Makala haya ni sehemu ya mfululizo ya ripoti maalum zinazoangazia namna ya kukabiliana na Uviko-19 nchini zinazofadhiliwa na Shirika la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV

Sakata bei ya mafuta kupanda latua BoT, Naibu Gavana atoa ufafanuzi

Sakata bei ya mafuta kupanda latua BoT, Naibu Gavana atoa ufafanuzi

Nukta TV

BoT yabakiza Riba ya Benki Kuu 5.75% kudhibiti mfumuko wa bei

BoT yabakiza Riba ya Benki Kuu 5.75% kudhibiti mfumuko wa bei

Nukta TV