Vipaumbele vitano bajeti ya Serikali Tanzania 2025/26
- Baadhi ya vipaumbele hivyo ni pamoja na kuchochea uchumi shindani na shirikishi na kukuza uwekezaji na biashara.
- Kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa bidhaa viwandani na utoaji huduma.
Dar es Salaam. Serikali imesema bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 itajikita katika kutekeleza maeneo matano ya vipaumbele ikiwemo kuchochea maendeleo ya watu kwa kuimarisha usimamizi na uendeshaji mifumo na miundombinu ya elimu, afya, maji na mazingira ya wananchi.
Utekelezaji wa vipaumbele hivyo ni sehemu ya kukamilisha utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof Kitila Mkumbo ameliambia Bunge jijini Dodoma kwamba katika bajeti inayoanza Julai mwaka huu itakuwa ni vipaumbele ambavyo ni kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa bidhaa viwandani na utoaji huduma.
Vipaumbele vingine ni kukuza uwekezaji na biashara, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.
Katika hotuba yake kuhusu hali ya uchumi wa taifa na mpango wa maendeleo wa Taifa wa mwaka 2025/26, Prof Kitila amesema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi itaweka mkazo kwenye miradi ya kimkakati yenye manufaa na matokeo makubwa.
Serikali imesema programu na miradi ya maendeleo itakayotekelezwa italenga kuimarisha usimamizi wa mifumo na miundombinu ya huduma za jamii, kuongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi, kukuza ujuzi kwa vijana, na kutoa mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wa elimu ya juu.
Ili kuchochea uchumi shindani na shirikishi, Serikali itajikita zaidi katika kutekeleza miradi na programu za maendeleo zinazolenga kuongeza uwezo wa nchi kikanda na kimataifa.

na Uwekezaji, Prof Kitila Mkumbo akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya uchumi wa Taifa kwa
mwaka 2024 na mpango wa maendeleo wa Taifa
2025/2026. Picha/ Bunge la Tanzania.
Kuboresha mazingira ya biashara
“Kuimarisha utulivu na uendelevu wa viashiria vya uchumi jumla kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara na kuendeleza miundombinu ya usafiri na usafirishaji, Tehama na nishati,” amesema Prof Mkumbo.
Serikali, amesema, itaimarisha uwezo wa uzalishaji wa bidhaa viwandani na utoaji huduma kwa kujielekeza katika programu na miradi ya maendeleo inayolenga kuimarisha uzalishaji viwandani.
Katika jitihada za kukuza uwekezaji na biashara, Prof huyo amesema itatekeleza programu na miradi itayoimarisha mifumo ya kitaasisi, sera na sheria za kodi ili kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji.
Bajeti hiyo ya mwisho ya awamu ya kwanza ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele cha kuendeleza rasilimali watu kwa kuwa na programu na mikakati inayolenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasilimali watu nchini, kuanzia ngazi za elimu ya awali hadi elimu ya juu ili kuwawezesha vijana kujiajiri.
“Eneo hili linajumuisha hatua za kuboresha viwango vya utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na ujuzi adimu ambavyo ni muhimu katika kuongeza tija na ushindani wa wananchi katika kutumia rasilimali zilizopo nchini ili kuleta maendeleo,” amesema Prof Mkumbo.
Miradi ya kielelezo na kimkakati
Ili kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kupitia matumizi ya mbegu bora, mbolea, kuongeza eneo la umwagiliaji na kukamilisha bandari ya uvuvi.
Katika sekta ya miundombinu, Serikali itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya usafiri na uchukuzi kama reli ya kisasa ya SGR, uboreshaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), upanuzi wa barabara, ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi na bomba la mafuta ghafi (EACOP).
Pia, juhudi za kupanua miundombinu ya kidigitali zitaimarishwa ili kuongeza matumizi ya Tehama katika uzalishaji, biashara na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Latest



