Uchumi wa Tanzania watarajiwa kukua 6% 2025

June 12, 2025 11:54 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Prof Kitila Mkumbo asema uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.5 mwaka 2024, imara zaidi ya ukuaji wa asilimia 5.1% mwaka 2023.
  • Sekta tatu za kilimo, ujenzi na uchimbaji madini zilichangia zaidi ya nusu ya pato la taifa mwaka 2024

Dar es Salaam. Uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa kasi ya asilimia 6.0 mwaka 2025 kutoka kasi ya asilimia 5.5 mwaka 2024, hatua inayoashiria matarajio chanya ya kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini baada ya kuathiriwa vibaya na ugonjwa wa Uviko-19 miaka mitano iliyopita. 

Matarajio hayo chanya yanakuja wakati kuna presha katika soko la dunia kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kubadilika kwa sera za Serikali ya Marekani na migogoro ya kivita inayoendelea mashariki ya kati. 

Pato halisi la Taifa lilifikia Sh156.6 trilioni mwaka 2024 kutoka Sh148.5 trilioni mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 5.5.

Katika mwaka 2024, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof Kitila Mkumbo ameliambia Bunge kuwa uchumi uliimarika na kukua kwa kasi ya asilimia 5.5 kutoka asilimia 5.1 iliyorekodiwa mwaka 2023 ukichochewa zaidi na jitihada za Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo. 

Prof Kitila amesema miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja kuanza kwa uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere, kuendelea na utekelezaji endelevu wa miradi ya kimkakati na ya kielelezo inayohusisha miundombinu ya nishati na usafirishaji. 

“…kuongezeka kwa mikopo ya sekta binafsi, usimamizi madhubuti wa sera za fedha, kuimarika kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo, na uwekezaji wa Serikali katika huduma za jamii hususan elimu, afya, maji na hifadhi ya jamii,” amesema. 

Kwa mujibu wa hotuba hiyo ya hali ya uchumi iliyotolewa leo jijini Dodoma, Prof Kitila amesema sekta tano ziliongoza kwa ukuaji ni sanaa na burudani iliyokua kwa kasi ya asilimia 17.1%, uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme (asilimia 14.4), habari na mawasiliano (asilimia 14.3), fedha na bima (asilimia 13.8) na afya iliyoripoti ukuaji wa asilimia 10.1

Kilimo bado uti wa mgongo

Kilimo kimeendelea kutoa mchango mkubwa zaidi katika ukuaji wa uchumi nchini kikichangia zaidi ya robo ya pato la taifa. Kwa mujibu wa takwimu za hali ya uchumi, sekta tatu zilichangia takribani nusu ya pato la taifa ambazo ni kilimo kilichochangia kwa asilimia 26.3, ujenzi asilimia 12.8% na uchimbaji wa madini na mawe uliochangia kwa asilimia 10.1. 

“Tunachohitaji kwa siku za usoni ni kuongeza tija zaidi kwenye uzalishaji ili kilimo kiwainue Watanzania wengi zaidi kimapato,” amesema Prof Kitila. 

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unaendelea kuimarika kwa kasi duniani baada ya kuathiriwa vibaya mwaka 2020 baada ya maradhi ya Uviko-19 kutikisa uchumi wa dunia huku nchi zinazoendelea za Afrika zikiathirika zaidi. 

Taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili, 2025 inabainisha kuwa kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa kwa nchi za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kilikuwa asilimia 1.5 na asilimia 3.1 mwaka 2024. 

Matarajio ya ukuaji wa uchumi katika kanda hizo mbili ambazo Tanzania ni mwanachama ni chini ya wastani wa ukuaji wa asilimia 5.2 kwa SADC na asilimia 3.9 kwa EAC mwaka 2023.

Mwaka 2020 kasi ya ukuaji uchumi wa Tanzania ilishuka kidogo hadi asilimia 4.8 kutoka ukuaji wa wastani wa asilimia 7 kabla ya Uviko-19. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks