Kutana na wanakijiji wanaojiweka hatarini kwa kuamini “hakuna Uviko-19”

October 23, 2021 6:04 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni wananchi wa Kijiji cha  Makangalawe mkoani Njombe.
  • Ukosefu wa elimu, uzushi na mila potofu vyachangia kutokuchukua tahadhari.
  • Serikali yasema itawafikia kwa elimu ya kujikinga ikiwemo  kuchanja chanjo.

Njombe. Ndani ya chumba kidogo chenye ukubwa wa mita mbili kwa mbili, watu wasiopungua 10 wamekaa kwa kutazamana huku wakiendelea kupokezana kikombe cha lita tatu chenye pombe ya kienyeji aina ya ‘ugimbi’.

Kikombe hicho hupita kwa kila mtu ili kunywa pombe hiyo huku mazungumzo yakiendelea.

Chumba hicho ambacho kina kuta za matofali ya udongo na bati lililochakaa ni klabu ya pombe za kienyeji iliyopo Kijiji cha Makangalawe mkoani Njombe.Baadhi ya wakulima wa kijiji hicho kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Makete hukusanyika nyakati za jioni kupiga soga huku wakipata kinywaji hicho ambacho hutengenezwa kwa mahindi, ulezi na mtama

Vicheko vimetawala ndani na nje ya klabu hiyo huku wengine wakiendelea kucheza muziki wakiwa wamesogeleana.

Hiyo ni sehemu ya hali ilivyo katika kijiji hicho ambacho suala la kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona (Uviko-19) halipewi kipaumbele na wakazi wake.

Uvaaji wa barakoa, kunawa mikono, matumizi ya vitakasa mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima halizingatiwi kabisa licha ya kuwa ni miongoni mwa afua muhimu dhidi ya Uviko-19.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi kufikia Oktoba 21, 2021, Tanzania ilikuwa na wagonjwa wa Corona 26,034 na imeripoti vifo 724 vilivyotokana na ugonjwa huo.

Hali ya wanakijiji hao kutokujali kuhusu Uviko-19, haiishi vilabuni pekee. Katika vitongoji vya kijiji hicho ambacho Nukta Habari (www.nukta.co.tz) ilitembelea nako hali siyo tofauti kama ilivyo kwenye vijiwe ambavyo huwakutanishwa watu wakiwemo wazee baada ya kumaliza majukumu yao.

Mmoja wa wamiliki wa klabu kijijini hapo, Benjamin Chengula anadai kuwa kwa sasa wameambiwa Corona imepungua japo hakusema ni nani hasa aliyewaambia jambo hilo kiasi cha kuendelea kuwaweka hatarini kupata maambukizi.

Anasema kuwa hiyo imewafanya watu waache kuchukua tahadhari kama ilivyokuwa wakati ugonjwa huo umeingia nchi mwaka jana.

“Hapa kwenye kilabu chetu wateja wanakuwa wengi tu kama unavyoona…najikinga na Corona kwa kuvaa barakoa ila huwa tunavaa barakoa tunapokwenda Ikonda (hospitali) tu,” anasema Benisia Chengula, mmoja wa wahudumu klabuni hapo huku akicheka.

Baadhi ya wanachi wa Wilaya ya Makete wakipata kinywaji aina ya ugimbi katika moja ya klabu ya pombe iliyopo Kijiji cha Makangalawe. Picha| Imani Henrick.

‘Huu ndiyo mzizi wa tatizo’

Licha ya wakazi wa kijiji hicho kufahamu uwepo wa Uviko-19, wengi bado hawana elimu na taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huo, jambo linalowafanya wasione umuhimu wa kuchukua tahadhari ikiwemo kupata chanjo.

“Yaani hapa elimu haijatufikia kabisa, na hata kuhusu chanjo hatujaelimishwa ila tunasikia kwenye redio na televisheni. Naiomba  Serikali itufikie na sisi wa huku vijijini, ikiwezekana elimu ipite hata kaya kwa kaya ili watu waelewe,” anasema Mohamad Studio, mkazi wa kijiji cha Makangalawe.

Hata hivyo, uongozi wa kijiji unakiri kutoa elimu kwa mtu mmoja mmoja tu kuhusu kujikinga lakini hakujawahi kufanyika mkutano mkubwa wa kutoa elimu hiyo.

Kaimu Mtendaji wa kijiji cha Makangalawe, Grace Sanga anasema wanawaelimisha wakazi hao, ambao sehemu kubwa ni wakulima na wafugaji, kunawa mikono na maji tiririka na sabuni na kutogusana mikono. 

Wakazi wa mkoa huu wana utamaduni wa kusalimiana kwa mikono na hata kubusiana wakati mwingine jambo ambalo wasipopatiwa elimu ya kutosha linaweza kusababisha wao kupata maambukizi.

“Kuhusu kujikinga na corona tunazidi kuwahamasisha wananchi wachukue tahadhari  kwa kuvaa barakoa na kutokugusana kwenye mikono,” anasema Sanga.

Imani ya wananchi wa kijiji hiki ni kuwa ugonjwa huo haupo, jambo linalowafanya wasione umuhimu pia wa kuchanja chanjo ya Uviko-19 ili kujihakikishia usalama zaidi.

Hatua zinazochukuliwa

Mganga Mkuu Halmashauri ya mji Njombe, Dk Yesaya Mwasubila anakiri wazi kuwa ugonjwa wa Uviko-19 upo na ni tishio kwa watu wasiochukua tahadhari. 

Anasema kuwa matibabu yake ni magumu na gharama zake ni kubwa hivyo watu wanatakiwa kuchukua tahadhari na kujikinga ili wasiupate. 

Aidha ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kujitokeza kuchanja kwani chanjo hupunguza makali ya Corona.

“Mpaka kufikia mwezi wa 9 wagonjwa wa corona wamepungua, siwezi jua kwa idadi gani ila wagonjwa wa kwenye oksijeni wamepungua. Hii haimaanishi kwamba Corona haipo, corona ipo na watu waendelee kuchukua tahadhari,” anasema Dk Mwasubila 

Aidha ameongeza kuwa, mpaka sasa Halmashauri yake imechanja watu zaidi ya 1,500 na bado wanaendelea na kampeni ya kuelimisha jamii  kupitia mikutano ya hadhara na nyumba za ibada juu ya ugonjwa huu pamoja na chanjo yake ili wajikinge.

Mratibu wa chanjo Mkoa wa Njombe, Linda Chatilla anasema jitihada mbalimbali zimekua zikichukuliwa kuhakikisha jamii inaelimishwa kuhusu Corona na chanjo.

Hata hivyo, anasema wamekuwa wakipata changamoto katika utoaji wa elimu hiyo ikiwemo baadhi ya watu kukataa chanjo kutokana na imani potofu na uzushi unaonea kwenye jamii.

Anasema wameongeza vituo vitakavyokuwa vinatoa chanjo hiyo kutoka 39 hadi 224, wanafanya uhamasishaji kwa kushirikisha wadau mbalimbali kama viongozi wa dini, wanahabari, viongozi wa siasa na watendaji ngazi mbalimbali.

“Tunahakikisha huduma ya chanjo ya Uviko-19 inaendelea kuwa sehemu ya huduma za chanjo zinazotolewa kila siku katika vituo vya kutolea huduma za afya,” anasema Chatilla. 

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW