Wafanyakazi wa Google, Facebook kufanyia kazi nyumbani hadi 2021
- Kwa wafanyakazi wanaolazimika kufanya kazi wakiwa ofisini wataruhusiwa kufika ofisini kati ya Juni 1 na Julai 6 mwaka 2020.
- Waliosalia ambao wanalazimika kutumia huduma za umma wataendelea kufanyia kazi wakiwa nyumbani hadi mwakani.
- Tahadhari juu ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 zitafuatiliwa vilivyo wakiwa ofisini.
Dar es Salaam. Kampuni za teknolojia za Google na Facebook zimeongeza siku za baadhi ya wafanyakazi wake kufanyia kazi wakiwa nyumbani hadi mwaka 2021 ili kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona.
Kampuni hizo mbili ambazo zina makao makuu yake nchini Marekani zimeeleza kuwa wafanyakazi watakaoendelea kufanyi kazi nyumbani ni wale ambao shughuli zao zinaruhusu kufanywa wakiwa nje ya ofisi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Google Sundar Pichai amewaambia wafanyakazi wake kuwa huenda muda wa kufanya kazi wakiwa nyumbani ukazidi kuongezeka hadi mwaka ujao wa 2021.
Pichai katika barua pepe kwa wafanyakazi wake amesema baadhi ya wafanyakazi wanaolazimika kufanya kazi ofisini, huenda wakaruhusiwa kurudi kwenye ofisi zao Juni 1, 2020 au Julai huku hatua za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 zikiendelea kutiliwa mkazo.
Zinazohusiana
- Google kutoa Sh15.1 bilioni kwa wathibitishaji habari za Corona
- Hivi ndivyo Google inavyoondoa upweke mtandaoni
- Google yatoa ahueni kwa wanunuzi wa bidhaa mtandaoni
Kampuni hiyo ambayo imekuwa msaada kwa kuwawezesha watu kufauta vitu mtandaoni, iliwazuia wafanyakazi wake kwenda ofisini tangu mwezi Machi mwaka huu.
Nayo kampuni ya Facebook imetoa tangazo la kuwarudisha baadhi ya wafanyakazi wake ofisini ifikapo Julai 6, 2020 huku wengine wakiendelea kufanya kazi wakiwa nyumbani hadi mwaka huu uishe.
Mwanzilishi wa mtandao huo wa kijamii Mark Zuckerberg amesema wafanyakazi wa kampuni hiyo wameweza kumudu utendaji kazi wao licha ya kufanyia kazi majumbani mwao.
“Tunapunguza kasi ya mipango yetu ya kurudi ofisini ili kuweka kipaumbele kwenye kusaidia jamii yetu na uchumi ili virudi kwenye hali ya kawaida kama awali.” imesomeka sehemu ya waraka wa Zuckerberg.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Sahara Ventures Jumanne Mtambalike amesema kwa upande wa kampuni za Tanzania zinatakiwa kuweka mpango mkakati kukabiliana na hali yoyote unayoweza kutokeoa kipindi hiki cha mlipuko wa Corona.
Mtambalike amesema zaidi ya asilimia 80 ya wafanyakazi wa Sahara ventures wanafanyia kazi nyumbani na wamejiwekea mipango mikakati ya kurudi ofisini hadi Julai pale hali itakapokuwa nzuri.
Amesema huu ni wakati sahihi kwa kampuni nchini kuwekeza katika matumizi ya mifumo ya teknolojia ili kuendelea na shughuli za uzalishaji, jambo litakalosaidia kupunguza athari za Corona.