Unavyoweza kutengeneza amani, furaha mwaka 2021
- Baada ya malengo ya baadhi ya watu kushindwa kutimizwa mwaka huu, una kila sababu ya kujipanga kwa ajili ya mwaka ujao
- Unaweza kuweka akiba kufikia lengo fulani na kulikamilisha mara tu unapokuwa na uwezo.
- Pia, wakumbuke wazazi, ndugu, jamaa na rafiki kwa kujenga tabasamu katika sura zao.
Dar es Salaam. Nikiwa katika usafiri kuelekea kazini leo, niliamua kutokusikiliza muziki na badala yake, nilitumia muda wangu kufikiria safari yangu ya kimaisha nikitafakari malengo yangu ya mwaka 2020 yalivyoshindwa kutimia.
Sikuwa peke yangu kwani kondakta wa gari nililokuwa nimepanda naye ana ya moyoni kuhusu mwaka huu. Tofauti na mimi niliyekuwa nikiwaza kimoyo moyo, yeye alikuwa akijadiliana na mwenzake jinsi gani mwaka huu “umemtenda kiuchumi na kwa nyanja zote.”
“Nilipanga nihame pale nilipokua naishi matokeo yake michongo imefeli, madili hamna hata hicho kiwanja chenyewe sijui kama nitaanza kujenga.” aliongea kondakta huyo ambaye alionekana kuanza kukata imekata.
Sikuweza kumpa ushauri lakini, huenda wewe unayesoma kolamu hii ukawa katika hali kama ya kondakta huyo ambaye kwa ajili ya habari hii, nitamuita Michael.
Unahitaji nini kuepuka msongo wa mawazo kwa mwaka ujao?
1. Jenga tabia ya kukamilisha ndoto zako pale unapokuwa na uwezo
Baadhi ya watu nikiwemo mimi nilikuwa na nafasi ya kukamilisha baadhi ya malengo niliyokuwa nimejiwekea kwa mwaka 2020 lakini tabia ya kusema mwezi ujao, kesho au wiki ijayo imeniponza.
Nilipanga kujifunza kupiga gitaa na kinanda lakini hadi mwaka unamalizika sijatimiza ndoto hiyo licha ya kuwa na uwezo wa kufanya. Nimejifunza na waraka wangu wa mwaka 2021 majira kama haya, naahidi hautakuwa vilevile.

Unapoweza kukamilisha jambo fulani lifanye katika muda ambao umeufanya. Picha| freepik.com
2. Weka akiba kwani hauijui kesho yako
Kwa mwaka 2021, jitahidi kuweka akiba itakayokusaidia kufikia baadhi ya malengo yako. Sio kwamba ujinyime sana kiasi cha kushindwa kula ipasavyo au kuwasaidia ndugu na jamaa, bali jifunze kuweka akiba isiyokuumiza.
Yapo mashirika mengi ya bima ambayo yameibuka na mipango ya akiba za muda mrefu ambazo unaweza kulipia moja kwa moja kutoka benki. Unaweza kuangazia hayo na hata kununua kibubu ambacho utakifungua mwishoni mwa mwaka 2020.
Kwa mfano, kama wewe ni mtu mwenye uwezo kidogo ukiamua kuweka Sh7,000 tu kila siku, una uhakika wa kupata Sh2.5 milioni mwishoni mwa mwaka. Pesa inayotosha kununua walau kiwanja cha kutosha kujenga kwa baadhi ya maeneo ya nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
3. Jitahidi kuongeza maarifa na kujiendeleza kielimu
Mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanakua kwa kasi sana kiasi cha kitu unachojivunia kukijua leo, kinaweza kuwa na programu inayokifanya kwa uweledi na makini kesho tu. kwa mwaka ujao, jitahidi kuongeza ujuzi wa kiteknolojia ili uwe salama.
Pia, kama una nafasi ya kujiendeleza kimasomo, ni vyema ukaiangazia. Kama una malengo ya kuongeza kipato chako ni vizuri kujifua kielimu hasa kama umeajiriwa ili uwe katika nafasi nzuri.
Endapoutapatanafasi ya kujiendeleza kielimu, usiiache nafasi hiyo ikupite. Picha| freepik.com
4. Jifunze kufurahia mafanikio yako
Mwaka huu nimetimiza mwaka mmoja kama muuza juisi na mwandishi wa habari. Kusherehekea mwaka mmoja wa kazi hizo niliamua kutengeneza juisi ya bure kwa wateja wangu wa mara kwa mara, kufungua akaunti rasmi ya Instagram kwa ajili ya juisi zangu. Pia, kama mwandishi wa habari niliamua kujinunulia boksi la peni na vitabu vya kuandikia “note book” maalumu kwa mwakani.
Ni vitu vidogo sana nilivyofanya lakini inanipatia faraja kuona furaha ya wateja wangu na kila nikiona vitabu nilivyonunua, inanipa ari ya kuandika habari makini na kuweka juhudi katika uandishi wangu.
Kama wewe ni mwana muziki, mwajiriwa, mjasiriamali na hata mwanafunzi uliyemaliza darasa moja kwenda lingine, jipongeze kwani wapo watu walioshindwa kufikia nafasi hiyo.
Soma zaidi:
- Ndoa ndoano? Maswali lukuki kuhusu ndoa na jinsia
- Jinsi ya kujikinga na madhara ya ongezeko la joto Tanzania
- Mbinu zitakazowasaidia wahudumu kuvuta wateja wengi mgahawani
5. Wekeza katika furaha yako
Kwa kiasi chochote unachopata katika harakati zako, jifunze kuwekeza katika furaha yako. Endapo unafurahia kutazama filamu, nenda katazame. Kama wewe unafurahia kuogelea, nenda kaogelee kwani mara moja moja siyo mbaya.
Utajisikiaje pesa yako ikipotea baada ya kujibana kwa muda mrefu bila kufurahia kila sekunde ya maisha uliyo nayo? Jipende walau kidogo.
Pia, unaweza kuwakumbuka watu wasiojiweza kwa chochote ulicho jaaliwa. Mnunulie mwanafunzi peni nzuri au daftari, muagizie maji au chakula mama muuza matunda, mnunulie mama yako kitenge huku baba ukimbariki na shati au suruali. Usifurahie peke yako, jenga tabasamu kwa mtu mwingine.
Pamoja na hayo yote, muhimu ni kumshukuru mungu wako kwa kukujaalia kufikia huu mwisho wa mwaka na kuwa na matumaini chanya kwa mwaka ujao.
Wako katika ujenzi wa taifa, @rodjazzy
Latest