Barua yangu kwa George wa mwaka 2022
- Natumaini masikio yako yanafanya kazi kuliko mdomo wako.
- Pia umeitambua furaha yako na dhamira ya uhai wako.
- Bado najiuliza kama umejifunza kusamehe na kuacha watu wawe watu.
Dar es Salaam. Kwako George, ni matumaini yangu kuwa huko uliko bado unatabasamu kama awali. Nimesikia tu panaitwa 2022. Sina uhakika lakini bila shaka nitakuwa sahihi.
Huku 2021 mambo bado hakujabadilika sana. Bado sipati muda wa kuwa na wale wanaonijali na kunipatia muda wao hasa nikiwa kwenye bonde kimaisha.
Bado ninawapatia nafasi wasiojali muda wangu na kusahau kuwa wapo ambao wanaweza kupiga mbizi na kunifuata chini ya bahari endapo maji yatanizidi uzito na kunimeza.
Bado sijajifunza kusherehekea mafanikio madogo madogo ninayoyapata hata kama yalikuja kwa kumwaga jasho, damu na nguvu nyingi.
Maneno ya watu juu yangu bado yananinyima usingizi na muda mwingine natamani dunia inifunike na udongo wake ili nipate muda wa kuwa na kichwa kisichowaza maovu yanayosemwa, dhihaka ninazotumiwa na hukumu ninazosomewa.
Nilikuwa nawe wakati unaandika malengo yako ya huko uliko lakini yapo ambayo ningependa kuona unayaongeza.
Pata muda wa kufurahia kidogo ulichonacho
Kutafuta mafanikio ni kazi ngumu. Inachukua muda, nguvu na zaidi umakini. Napenda kukuona ukipata muda wa kufurahia kidogo ulichonacho kwani safari ya kuyafikia mafanikio hakuna aliyewahi kuimaliza.
Matumaini yangu ni kuwa unafahamu ya kuwa hatujaahidiwa milele na hakuna anayeijua siku wala saa ya kurudi kwa muumba wake.
Tafadhali jifunze kuwa, furaha yako inakuja kwanza kabla ya kutaka kufurahisha wengine kwani ni ajabu vile maisha huendelea kwa kasi hata baada ya wewe kuaga dunia.
Jifunze kujifunza zaidi
Matumaini yangu huko uliko ni kuwa umeanza kujenga mahusiano na vitabu kama ulivyoniambia wakati unafunga virago vyako. Natumaini kuwa kabati lako la vitabu lina uhai na siyo kama ulivyokuwa huku.
Tukionana, ningependa kusikia kuwa umejifunza kujibu watu kwa maarifa na kuwa majibu yako hayaumizi hisia zao ila tu kama ni kwa nia njema.
Nitapenda kukusikia ukisema, sasa mdomo wako hufunguka kutoa baraka kwa wenzako na maarifa.
Kuwa umeelewa wanadamu ni watu na siyo malaika hivyo kukosea kwao ni sehemu ya kuwa wanadamu. Makosa yao yasikupe jazba bali yakufunze kutokuwa kama wao.
Ninatamani tayari umejifunza uhariri wa sauti na video kama ulivyopanga lakini zaidi, umeshakuwa mbobevu wa hisia zako.
Soma zaidi:
Utulie sasa baba!
Ni kweli tulipokuwa huku 2021 mzee baba ulikuwa na heka heka.
Ulifosi kutafuta chaka lako lakini haukulipata. Huko uliko, napenda kusikia kuwa umejifunza kuwa baadhi ya mambo hayalazimishwi na yanakuja baada ya wewe kujifunza kujipenda na kuifahamu thamani yako.
Natumaini kuwa umetulia na kugundua ya kuwa kuna zaidi katika maisha kuliko pesa, anasa, uasherati na vitu.
Kuna amani, shukrani, familia na upendo wa dhati kutoka kwa watu. Natumaini utakuwa umeijua thamani yako kwa kujua kuwa mwili wako siyo wa kila mtu na huenda hakuna faida ya kuwa na mahusiano yasiyokujenga.
Twende na talanta moja baada ya nyingine
Mwaka 2021 ulijaribu baba. Ulifanya biashara, uliimba, uliandika na ulitengeneza vitu mbalimbali vya ubunifu. Najua uliongea na na kaka zako. Kina Samora, Feruzi na rafiki zako ambao walikushauri haya ninayokuandikia.
Natumaini umechagua cha kuanza nacho iwe ni muziki, kuandika au chochote, najua utafanya uchaguzi sahihi.
Katika lolote ulilochagua, natumaini linakuruhusu kupata muda wa kupumzika, linakupatia tabasamu na nafasi ya kuona kuwa kuna zaidi kwenye maisha kuliko kazi pekee.
Natumaini unawapatia nafasi wanayostahili wale wakuzungukao, natumaini bado unajiona mdogo unaposimama mbele ya bahari na unaimba kila unapopata nafasi.
Natumaini sikio lako linachukua nafasi kuliko mdomo wako na miguu yako haikupeleki kwenye majuto. Bila shaka unachangia maarifa yako na wengine na unafurahia mafanikio ya wenzako.
George, kasi ya wenzako isikutie kihumwe humwe. Kama akili yako ya jana ni ndogo kuliko ya leo, basi upo kwenye njia sahihi.
Fahamu kuwa mafanikio ya kishindo nayo hupotea kwa kishindo kile kile. Usisahau kuwa wahenga hawakuwa wajinga waliposema “haba ba haba hujaza kibaba”.
Mzee baba, nisikupotezee muda sana, huenda upo na washkaji zako, wale ambao dhati yao unaijua na upendo wao ni wa wazi. Huenda upo stejini ukiimba nyimbo unazozifurahia au huenda leo umelala mapema.
La mwisho ninalokusishi, ni kuhakikisha kuwa kila ulalapo, una tabasamu na hauna kinyongo na awaye yeyote na uamkapo, uanze na muziki uupendao.
Msalimie sana atakayekupatia barua hii kwani ameshiriki vyema katika kukufanya George ninayemtambua.