Mwaka 2021 ulivyokuwa mchungu kwa vijana Tanzania

December 8, 2021 5:54 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Wasema malengo yao hayajatimia kikamilifu.
  • Corona, tozo na gharama za maisha vyachangia.
  • Wana matumaini makubwa mwaka 2022.

Mwanza. Tukiwa tunaelekea kumaliza mwaka 2021, baadhi ya vijana mkoani Mwanza wamesema hawatausahau mwaka huu kwa sababu ulikuwa wenye maumivu huku wakitazamia mwaka ujao utakuwa wenye neema kuwawezesha kutimiza ndoto zao.

Vijana hao wa rika tofauti wanadai licha ya mipango mingi waliyojiwekea, hawakuweza kuitimiza kwa sababu ya changamoto mbalimbali ikiwemo janga la Corona (Uviko-19) na kupanda kwa gharama za maisha.

Nukta habari (www.nukta.co.tz) imezungumza na makundi ya waendesha bodaboda pamoja na wafanyabaishara ndogo maarufu kama machinga pamoja na mambo mengine wanasema malengo yao waliyojiwekea kwa mwaka huu hayajatimia.

Ibrahim George ni mwendesha bodaboda anayefanya shughuli zake katika kijiwe cha Kemondo jijini hapa, anasema mwaka 2021 ulipoingia alikuwa na lengo la kumalizia nyumba yake anayojenga, matokeo yake mwaka umekatika bila lengo hilo kutimia.

“Mzunguko wa fedha umekuwa mdogo, gharama za maisha zimepanda hali hii imesababisha nishindwe kutimiza malengo yangu, nina imani mwaka 2022 ninaweza kuzifikia ndoto zangu,” anasema George.

Baadhi ya bodaboda wanasema kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli na dizeli kumesababisha, madereva hao kutoboa zaidi mifuko yao kupata bidhaa hiyo.

Dereva wa bodaboda katika kijiwe hicho, Jamson Jackson anasema gharama za petroli pia zimechangia kutotimiza malengo yake.

“Kila kukicha bei ya petroli inapanda wakati huo bei ya kusafirishia abiria inabaki kuwa hapo hapo, hali hii inasababisha kushindwa kutimiza malengo yetu,” anasema Jackson.

Wajasiriamali wakionyesha bidhaa zao katika maonyesho ya wajasirimali wadogo na wakati ya Afrika Mashariki yanayoendelea katika viwanja vya Rock city mall jijini Mwanza. Picha | Mariam John.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), bei ya rejereja ya mafuta ya petroli yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi Desemba imepanda hadi Sh2,510 kwa lita moja kutoka Sh2,439 kwa lita moja iliyotumika mwezi uliopita wa Novemba.

Kwa Bandari ya Mtwara, petroli imepanda hadi Sh2,569 kwa lita kutoka Sh2,455 kwa lita iliyotumika Novemba 2021 ikiwa ni ongezeko la Sh114.

Ongezeko la bei ya petroli limeshuhudiwa pia katika Bandari ya Tanga (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara) ambapo mafuta hayo yamepanda hadi Sh2,525 kwa mwezi Desemba kutoka Sh2,478 kwa lita iliyotumika mwezi uliopita.

Hata hivyo, Ewura imeeleza kuwa kupanda kwa bei ya mafuta nchini Tanzania kumechangiwa na ongezeko la nishati hiyo katika soko la dunia na hivyo kuathiri bei za ndani.

Hata hivyo, bei ya mafuta inatarajia kushuka katika siku za hivi karibuni kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa duniani ikiwemo kuongeza kiasi cha mafuta kinachouzwa katika soko la dunia.

“Kulingana na mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia, bei za mwezi Novemba 2021 zimeanza kushuka. Kwa kuwa bei za soko la dunia zinaakisiwa katika soko la hapa nchini baada ya miezi miwili, unafuu wa bei za soko la dunia ulioanza kujitokeza katika mwezi Novemba 2021 unatarajiwa kuonekana katika soko la hapa nchini katika bei za mwezi Januari 2022,” imeeleza Ewura.

Jackson anaamini kuwa mwaka 2022 utakuwa mwaka wa mafanikio yake ambapo ana lengo la kuachana na bodaboda na kumiliki bajaji ya abiria.

 “Kwa sasa usafiri wa bajaji katika jiji hili la Mwanza ndiyo unashika kasi na pia unapendwa na watu wengi kwa usalama wao, ni mara chache kusikia ajali za bajaji lakini pikipiki kila siku zinaripotiwa,” anasema Jackson.


Zinazohusiana


Mbali na madereva hao, wajasiriamali wadogo maarufu kama machinga, wao wanasema mwaka 2021 wameshuhudia mabadiliko makubwa ya namna wanavyoendesha biashara zao.

Kutoka kuuza bidhaa barabarani mpaka katika masoko na maeneo maalum waliyopangiwa, jambo linalowafanya kuanza kufikiri upya namna ya kuwafikiwa wateja wao.

Hivi karibuni, Serikali iliendesha zoezi la kuwaondoa machinga wote katika hifadhi za barabara na kuwapangia katika maeneo maalum ili kuondoa usumbufu kwa watumiaji wa miundombinu hiyo.

Hata hivyo, mabadiliko hayo yamepokelewa kwa hisia tofauti, huku baadhi ya machinga wakisema mauzo yao yamepungua kwa sababu maeneo walikopelekwa bado biashara hazijachanganya hivyo kuwa katika hatari ya kupoteza mitaji yao.

Muuzaji wa nguo za watoto za mtumba jijini hapa, Abeid Salum anasema tangu mwaka ulipoingia alikuwa na lengo la kuwa anafungua belo tatu hadi nne kwa wiki kwa kuwa kulikuwa na mzunguko mkubwa wa biashara lakini hali imekuwa tofauti.

“Nilianza na mtaji mdogo wa kufungua bello 1 kwa wiki nikajiwekea mwaka huu nitakuwa nafungua bello 3 hadi 4 lakini nimeshindwa kutokana na misukosuko tuliyokutana nayo,” anasema Salum.

Baadhi ya bodaboda wanalalamika kupanda kwa bei ya mafuta kunawaumiza kibiashara. Picha| Mtandao.

Abeid na wafanyabiashara wengine wanakiri kuwa huu ni mwezi wa pili sasa toka walipohamishiwa maeneo mapya mwenendo wa biashara hauridhishi.

“Mwaka unaenda kuisha vibaya umekuwa mwaka mgumu, mwanzoni ilikuwa afadhali lakini mwishoni ndiyo umekuwa mbaya vijana hatuna hela tukifungua bello linakaa hata wiki mbili wateja hamna,” anasema Salum Salum,  muuzaji wa nguo jijini hapa.

Serikali imeendelea kueleza kuwa suala la kuwapanga upya wamachinga lina maana kubwa kwa sababu imewawekea wafanyabiashara maeneo sahihi ya kufanyia biashara ili wafaidike na fursa zinazokuja mbele yao ikiwemo kujengewa miundombinu ya kisasa na kuwawezesha kufanya biashara katika maeneo rasmi.

Tozo nazo bado mlima

Wakala za huduma za fedha mtandaoni, Kazimir Mussa anasema kabla ya Serikali kupitisha tozo za miamala ya simu, hali ya biashara ilikuwa nzuri lakini sasa upepo umebadilika.

“Ni kweli wamepunguza asilimia fulani lakini hali ya biashara bado ni mbaya watu hawajazoea kwa siku tunapokea wateja wasiozidi 10 tofauti na zamani ambapo biashara ilikuwa nzuri na tulipata wateja wengi,” anasema Mussa.

Malengo ya Mussa ilikuwa ni kufungua ofisi zingine za aina hiyo kama tatu lakini hadi sasa bado yuko na hiyo moja.

Tozo hizo zilianza kutumika katika mwaka wa fedha 2021/22 na Serikali ilibainisha kuwa zitatumika kuboresha miundombinu ya kijamii ikiwemo maji, umeme, elimu na afya.

Wewe unaonaje mwaka 2021? Umetimiza malengo yako? Umejipangaje kwa ajili ya mwaka ujao?

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW