Vito vitano vyenye thamani zaidi duniani
- Kito chenye thamani zaidi ni almasi ya bluu.
- Vito vya almasi ndiyo vinatawala orodha hiyo.
- Vito hivyo ni adimu kupatikana duniani.
Dar es Salaam. Huenda umeona baadhi ya viganja vya wanawake vikiwa vimepambwa na vito mbalimbali vya thamani. Almasi, Tanzanite, Yakuti na Zumaridi.
Siyo wanawake tu, kwa watu wengine mashughuli pia ikiwemo wafalme, viongozi na wasanii wameonekana mara kadha wakiwa na vito vya kupendeza na kuvutia macho.
Umewahi kufahamu gharama ya vito hivyo? Kama jibu ni hapana, hii ndiyo orodha ya vito vyenye thamani zaidi duniani kwa kipimo cha karati.
Karati ni kipimo cha uzito wa vito vya thamani ambapo karati moja ni sawa na gramu 0.5. Uzito huo ni sawa na kusema, karati tano za kito cha thamani ni sawa na gramu moja.
05. Zumaridi (Emerald)
Tovuti ya masuala ya jiolojia (Geologypage) kupitia andiko la Agosti 6, 2020 imeainisha kuwa kito cha zumaridi kinashika nafasi ya tano duniani kwa gharama.
Vito hivi vinavyochimbwa sehemu mbalimbali duniani vinapatikana zaidi nchini Zambia, Colombia na Brazil.
Karati moja ya kito hiki ina thamani ya Dola za Marekani 305,000 ambayo ni sawa na Sh707.1 milioni.
Kwa mujibu wa tovuti ya Gemic, kwa upande wa kito cha Zumaridi, jiwe kubwa zaidi limechimbwa nchini Brazil likiwa na uzito wa karati milioni 1.7 sawa na kilogramu 340 na limepewa jina la “Bahia Emerald”.
Hata hivyo, changamoto ya vito hivi ni kuwa ikilinganishwa na vingine, vinaweza kuvunjika haraka.
Jiwe kubwa zaidi aina ya Zumaridilenye kilogramu 340 limepewa jina la “Bahia Emerald”. Picha Geology Page.
04. Almasi nyekundu (red diamond)
Ni kati ya vito nadra duniani na vinapatikana zaidi kwenye nchi chache barani Afrika, Australia na Brazil.
Geologypage imeandika kuwa, karati moja ya vito vya almasi nyekundu inauzwa kwa Dola za Marekani milioni 1 sawa na Sh2.3 bilioni.
Tovuti ya Shirika la Habari la nchini Marekani la CNN imeainisha kuwa, jiwe kubwa la kito hiki linaitwa “Moussaieff Red” likiwa na uzito wa karati 5.1 ambalo lilichimbwa nchini Brazil miaka ya 1990.
03. Almasi ya pinki (pink diamond)
Ndiyo, mbali na almasi zisizo na rangi, zipo almasi zenye rangi. Umeona almasi nyekundu na sasa, ipo almasi hii ya rangi ya pinki. Gologypage imeandika kuwa, ni asilimia 0.0001 ya almasi zote duniani ndio zina rangi hii. Maana halisi ya takwimu hiyo ikiwa ni adimu.
Kutokana na uadimu huo, almasi hii ina thamani ya Dola za Marekani milioni 1.2 milioni sawa na Sh4.4 bilioni.
Almasi kubwa ya pinki duniani kuwahi kuchimbwa ni ile yenye uzito wa karati 59.6 ambayo ilifanyiwa mnada mwaka 2017 na iliuzwa kwa gharama ya Sh165.1bilioni.
Jina la almasi hiyo ni “Pink Star” na ilichimbwa nchini Afrika Kusini.
02. Jadeite
Karat moja ya Jadeite ina gharama ya Dola za Marekani milioni 3 ambayo ni sawa na Sh6.9 bilioni.
Vito hivi vinapatikana zaidi nchini Burma na Japan na vinatajwa kupatikana kwa uchache.
Kwa mujibu wa Geologypage, Jadeite zina sifa ya ugumu ikilinganishwa na vito vingine.
Pete ya almasi ya bluu iliuzwa kwa gharama ya zaidi ya Sh130 bilioni. Picha| CBS New York.
01. Almasi ya bluu (blue diamond)
Almasi ya blue ndiyo kito chenye thamani zaidi duniani kulingana na kipimo cha uzito uliowahi kuuzwa yaani Karat.
Kwa mujibu wa Geologypage, karati moja ya almasi ya bluu inauzwa kwa Dola za Marekani milioni 3.9 sawa na Sh9 bilioni.
Almasi ya aina hii iliyopewa jina la “The Oppenheimer Blue” iliuzwa kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 57.5 sawa na Sh133.3 bilioni.
Almasi za rangi hii zinachimbwa zaidi nchini Afrika Kusini, Australia na India.
Vipi, unaweza kumiliki kito kipi kati ya hivyo? Endelea kufuatilia Nukta Habari (www.nukta.co.tz).
Latest
