Haya ndiyo masoko 10 ya kimataifa ya bidhaa za Tanzania

October 1, 2021 8:45 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Zaidi ya asilimia 50 ya bidhaa za Tanzania zinauzwa katika nchi sita tu.
  • Soko kubwa la bidhaa za Tanzania ni Afrika Kusini.
  • Tanzania inanunua zaidi bidhaa zake kutoka China.

Dar es Salaam. Kama ulikuwa hujapata jibu la Tanzania huuza wapi bidhaa zake nje ya nchi, basi jibu limepatikana. Tanzania huuza zaidi bidhaa zake nchini Afrika Kusini. 

Kitabu Cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020 kilichotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kimetaja orodha ya nchi 10 ambazo Tanzania huzitegemea zaidi kuuza bidhaa zake. 

Orodha hiyo inaoongozwa na Afrika Kusini ambapo asilimia 19.2 ya bidhaa zote zilizouzwa nje ya nchi mwaka 2020 zilienda katika nchi hiyo iliyopo kusini mwa bara la Afrika.

Hiyo ni sawa na kusema takriban bidhaa mbili ya 10 zilizouzwa nje ya nchi mwaka jana zilipelekwa Afrika Kusini. 

Afrika Kusini inachuana vikali na nchi ya Uswisi iliyopo bara la Ulaya iliyoshika nafasi ya pili kupokea bidhaa za Tanzania ikifuatiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (UEA). 

Bidhaa zinazouzwa zaidi nje ya nchi

Katika masoko hayo ambayo Tanzania inayategemea kujipatia kipato huuza zaidi bidhaa za kilimo na madini ya dhahabu. 

Kwa mujibu wa kitabu hicho, kwa  mwaka 2020, Tanzania ilisafirisha nje ya nchi zaidi mbegu za mafuta, tumbaku, kahawa korosho na dhahabu. 

Bidhaa nyingine ni mahindi, mchele na mazao ya mboga mboga ambayo yalienda zaidi Afrika Kusini, Uswisi, Umoja wa Falme za Kiarabu, India, China na Kenya.

Hii inaweza kuwa fursa kwa Watanzania hasa vijana kuwekeza nguvu zao katika sekta ya kilimo ili kufaidika na masoko hayo ambayo Tanzania imekuwa ikipeleka zaidi bidhaa zake. 

Wakati Tanzania ikiuza zaidi bidhaa za kilimo na madini nje ya nchi, mwaka 2020, iliagiza bidhaa zake kwa kiasi kikubwa kutoka ni China, India, Umoja wa Falme za Kiarabu, Japan, Afrika Kusini na Saudi Arabia.

“Nchi hizo sita ambazo kwa pamoja zilichangia asilimia 60.06 ya thamani ya bidhaa zote zilizoagizwa kutoka nje ya nchi,” imeeleza sehemu ya kitabu hicho ambacho kinapatikana kwenye tovuti ya NBS.

Bidhaa zilizoagizwa ni pamoja na mitambo, matrekta na bidhaa za kielektroniki kutoka China pamoja na mafuta ya petroli kutoka nchi za Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu. 

Aidha, magari na vyuma viliagizwa kutoka India na Afrika Kusini.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW