Uviko-19 yachangia ATCL kupata hasara ya Sh60.24 bilioni
- Serikali yasema ugonjwa uliathiri sekta ya anga duniani mwaka 2019/20.
- Yasema imeanza kuchukua hatua kutatua changamoto ya hasara.
- PAC yaonya ongezeko la deni.
Dar es Salaam. Serikali imesema ugonjwa wa Corona (Uviko-19) ulichangia Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kupata hasara ya Sh60.24 bilioni katika mwaka 2019/20 huku ikisema itaiimarisha shirika hilo kujiendesha kibiashara.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Uchukuzi), Dk Ally Possi aliyekuwa akizungumza leo Februari 23, 2022 katika ofisi za ATCL jijini Dar es Salaam amesema athari za Uviko-19 zimechangia hasara hiyo.
“Hasara ile imetengenezwa na sababu nyingi, kama utakumbuka ugonjwa wa Uviko ulikuwa umeathiri sekta ya usafirishaji wa anga siyo kwetu tu ila mashirika mengi ya ndege duniani tukiwamo sisi pia,” amesema Dk Possi.
Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea na mikakati ya kutatua changamoto hiyo ya hasara ikiwemo kuboresha viwanja vya ndege nchini na kuongeza ndege mpya ili kuongeza ushindani katika sekta ya anga.
Kauli ya Dk Possi imekuja wakati kukiwa na mjadala mpana kwenye jamii kuhusu uendeshaji wa shirika hilo ambapo baadhi ya watu wanasema ni vema Serikali ijitoe katika uendeshaji wake.
Licha ya hasara ya Sh60.24 bilioni ya 2019/20, ATCL ina hasara jumuishi ya Sh152.96 bilioni tangu mwaka 2015/16 kwa mujibu wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kwa sasa, ATCL ina vituo 23 vya safari ndani na nje nchi ambapo imeingia katika ushirikiano wa huduma za usafiri na mashirika ya ndege ya Rwanda, Qatar, Ethiopia.
Pia inaendelea kusaka za masoko ya kimataifa ikiwemo India na Marekani ili kuongeza ushindani.
“Uwepo wa madeni ya muda mrefu ni kihatarishi cha uendelevu wa kampuni kwa siku zijazo,” alisema Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka wakati akiwasilisha taarifa ya kamati yake hivi karibuni.