Air Tanzania inavyopoteza mabilioni kila mwaka
- CAG aanika visababishi vya hasara kwa ATCL ndani ya miaka mitano mfululizo.
- Ni pamoja na kutotumika kwa ndege za ATCL pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya fedha.
- Ashauri kutatuliwa kwa tatizo la malipo ya matengenezo ya ndege kwani yanaongeza hasara.
Dar es Salaam. Shirika la ndege Tanzania (ATCL) limeendelea kujiendesha kwa hasara kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo licha ya juhudi za Serikali kulikwamua ikiwemo kulipunguzia mzigo wa madeni na kutoa ruzuku.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 imebainisha kuwa miongoni mwa sababu zinazochochea shirika hilo kupata hasara ya mabilioni kila mwaka ni matumizi yasiyorishisha ya ndege, kuchelewa kuondoka kwa ndege za ATCL pamoja na kufutwa kwa tiketi.
CAG katika ripoti yake ya mashirika ya umma ya mwaka 2021/22 amebainisha kuwa licha ya ATCL kupewa ruzuku ya Sh30.63 bilioni shirika hilo limeripoti hasara ya Sh35.23 bilioni ambayo ingeongezeka kama Serikali isingetoa ruzuku.
“Serikali isingetoa ruzuku hiyo, kampuni ingepata hasara ya Sh65.86 bilioni. Hii inaonesha changamoto ambazo kampuni ya Ndege Tanzania inakabiliana nazo katika soko kwa sasa,” amesema CAG.
Ingawa hasara ya mwaka 2021/22 imepungua kwa bilioni moja kulinganisha na hasara ya Sh36.2 iliyoripotiwa mwaka 2020/21, huenda ATCL haitazalisha faida hivi karibuni iwapo menejimenti haitafanyia kazi changamoto zinazokabili shirika hilo.
Tangu mwaka 2016 Serikali imekuwa ikiwekeza mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuifufua ATCL iliyokuwa imeyumba vibaya sokoni kwa kuiongezea ndege na wafanyakazi. Hadi mwishoni mwa Machi 2023 ATCL ilikuwa ina ndege 12 zikiwemo Boeing B787-8 Dreamliner mbili zenye uwezo wa kubeba abiria 262 kila moja.
Shirika hilo linatarajia kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2023 litakuwa limeshapokea ndege nyingine tano De Havilland Dash 8 Q400, Boeing 737 Max-9 mbili, Boeing 787-8 Dreamliner moja na Boeing 767 ya mzingo inayotarajiwa kuingia nchini hivi karibuni.
Kutotumika kwa ndege za ATCL
Ripoti ya CAG imebaini kuwa ndege mbili za Airbus A220-300 na Bombardier (De Havilland) Q400 zilikuwa hazifanyi kazi kwa muda wa siku 2 mpaka 220 kati ya 1 Julai 2021 hadi 30 Juni 2022 kutokana na utendaji duni wa ndege hizo pamoja na kutofanyiwa matengenezo yanayostahili.
Uchambuzi wa kifedha umeonesha kuwa ndege zisizotumika zimesababisha shirika kuingia gharama zisizobadilika kutokana na kukodi na bima jumla ya Sh5.27 bilioni na kukosa mapato ya Sh20.35 bilioni ambayo yangepatikana endapo ndege ingefanya kazi kwa mwaka mmoja.
“Hali hii imeathiri sana ukwasi na sifa ya kampuni, pia kuongezeka kwa idadi ya ratiba za safari za ndege zilizofutwa kunaathiri uaminifu wa wateja juu ya usafiri wa Kampuni ya Ndege Tanzania,” amesema CAG.
Zinazohusiana
-
Hasara ya ATCL yapungua, Rais Samia aanika madudu mapya
-
Ripoti ya CAG: ATCL ilipata hasara ya Sh60 bilioni 2019-20
Dreamliner yazalisha Sh45.67 bilioni, yatumia Sh70.57 bilioni
Kutokuwepo usimamizi makini kati ya mapato na matumizi ya ATCL kumelisababishia shirika hilo hasara ya Sh29.4 bilioni pamoja na gharama za kudumu za matengenezo ambazo ni Sh5.06 bilioni.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG ndege ya Boeing 787-8 ilizalisha mapato ya jumla ya Sh45.67 bilioni na kutumia Sh70.57 bilioni na kusababisha hasara ya Sh24.9 bilioni.
Hata hivyo, CAG amebaini kuwa kukosekana kwa ufanisi wa uendeshaji kulisababishwa na idadi ndogo ya abiria na idadi ndogo ya safari za kimataifa, kwa kuwa ni safari tisa kati ya 18 za kimataifa zilifanyika kutokana na kusimamishwa kwa baadhi ya safari kwa sababu ya vikwazo vya udhibiti wa ugonjwa wa UVIKO-19.
Kuchelewa kuondoka kwa ndege na kubatilishwa kwa tiketi za ATCL
Licha ya ATCL kuweka lengo la kufikia asilimia 92 ya ndege kuondoka kwa wakati mwaka 2021/22 ripoti ya CAG imebaini safari 3,990 kati ya 15,820 zilichelewa kuondoka kwa wastani wa dakika 11 hadi masaa manne na dakika 33.
Hiyo ni sawa na kusema asilimia 25 ya safari zilizofanywa na ATCL yaani safari 25 kati ya 100 zilianza kwa kuchelewa jambo ambalo husababisha wateja kupunguza imani na wakati mwingine shirika hulazimika kurudisha fedha kwa wateja.
Pamoja na kutokuwa na wastani mzuri wa kuondoka kwa wakati ambao haishauriwi kuwa zaidi ya asilimia nane kwa viwango vya kimataifa, ATCL inakabiliwa na changamoto ya tiketi za ndege zinazonunuliwa kupitia mawakala kubatilishwa ambapo mwaka 2021/22 tiketi 38,455 zilifutwa.
Ripoti ya CAG imebaini kuwa ni asilimia nne tu ya tiketi hizo zilibatilishwa na ATCL huku asilimia 96 ikifanywa na mawakala jambo ambalo limesababisha hasara kwa kuwa mteja hulazimika kurudishiwa pesa yake na wakati mwingine mfumo kuonesha ndege imejaa wakati bado ina nafasi.
“Ili kuepukana na hilo ninapendekeza ATCL iboreshe mifumo ya udhibiti ya ndani kuhusu utaratibu wa kufuta tiketi ikiwa ni pamoja na kuweka masharti na ukomo wa kufuta tiketi kwa mawakala wa safari,” amesema CAG.
Abiria wakishuka kwenye ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Mbeya Oktoba 2022. CAG ameeleza kuwa ucheleweshaji wa safari na usitishaji wa tiketi ni miongoni mwa mambo yanayosababishia hasara shirika hilo. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta.
Gharama za ziada za matengenezo
Kwa mujibu wa CAG hasara ya Sh19.1 bilioni imetokea katika shirika hilo kutokana na tatizo la malipo mara mbili kwa huduma za matengenezo, ambazo huongeza gharama na madeni kwa Air Tanzania.
ATCL ilimlipa wakala wa ndege wa Serikali jumla ya Sh25.39 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya ndege ambacho kimeongezeka kutoka Sh18.56 zilizotozwa mwaka 2020/21.
Wakati wakala wa ndege wa Serikali akilipwa Sh25.39 bilioni, ATCL iliingia gharama ya Sh19.11 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya ndege katika mwaka huo,ambayo ni sehemu ya akiba ya matengenezo chini ya mkataba wa Wakala wa Ndege wa Serikali ya Tanzania.
Hata hivyo, CAG amebainisha kuwa kama kungekuwa na utaratibu mzuri wa kushughulikia malipo ya matengenezo ya ndege hizo hasara ingepungua.
“Gharama hizi zilizoingiwa mara mbili zimesababishia kuongezeka kwa hasara kwa ATCL. Ulipaji mara mbili wa gharama ambazo ni Sh19.11 bilioni kwa watoa huduma na Sh25.39 bilioni kwa Wakala wa Ndege wa Serikali ya Tanzania.
Ni maoni yangu kuwa gharama hizi na hasara iliyotokea mwaka huu ingeweza kupungua kutoka Sh35.24 bilioni mpaka Sh9.85 bilioni,” amebainisha CAG katika ripoti yake.
Latest