ATCL yaripoti hasara ya Sh119.1 bilioni CAG aanika sababu

March 30, 2026 5:19 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Hii ni mara  ya tatu mfululizo kwa ATCL kutajwa kuwa miongoni mwa mashirika ya umma yanayotengeza hasara nchini tangu mwaka 2022/23.
  • CAG anika sababu na mapendekezo kuiboresha ATCL.

Arusha. Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini kuwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) lilipata hasara ya Sh119.1 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/25 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa gharama za uendeshaji.

CAG Charles Kichere aliyekuwa akiwasilisha ripoti ya ukaguzi wake leo Machi 30, 2026 mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan amesema hasara hiyo imeongezeka kwa asilimia 108 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja ikiongezeka maradufu tangu kuanzishwa kwake.

“ATCL imefikisha jumla ya hasara ya Sh 748 bilioni tangu  kuanzishwa kwake licha ya kuendelea kupata ruzuku za Serikali kwa ajili ya mishahara na gharama za uendeshaji,” amesema CAG Kichere.

Hii ni mara  ya tatu mfululizo kwa ATCL kutajwa kuwa miongoni mwa mashirika ya umma yanayotengeza hasara nchini suala linaloacha mjadala mpana wa mchango wa shirika hilo katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Mwaka 2022/23 ATCL lilitengeneza hasara ya Sh56.6 bilioni iliyoongezeka kutoka Sh35.2 bilioni mwaka 2021/22 kabla ya kupaa tena mwaka 2023/24 kufikia 91.7 bilioni licha ya uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali katika shirika hilo.

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa alisema Serikali  ina mpango wa kuiendeleza ATCL ikitarajia kununua ndege nane mpya, hivyo kuongeza idadi ya ndege kutoka 16 hadi 24 zitakazotumika katika safari za ndani na za kimataifa.

Msigwa aliyekuwa akizungumza na wanahabari Februari 6, 2026 amesema kuwa ATCL inaendelea kuimarika ikionesha ukuaji chanya ikikusanya jumla ya mapato ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 157 (sawa Sh404.5 bilioni) tangu kuimarishwa kwake upya.

Sababu zatajwa

CAG Kichere amemweleza Rais Samia kuwa hasara hiyo inayojirudia kila mwaka imechangiwa na sababu mbalimbali kiwemo ongezeko la gharama za uendeshaji kuzidi ukuaji wa mapato.

“Hasara hii imechangiwa na mambo yafuatayo ongezeko la gharama za uendeshaji kuzidi ukuaji wa mapato ambapo gharama ziliongezeka kwa Sh 134 bilioni  na kufikia Sh675 bilioni , pia shirika limefanya safari chini ya matarajio, huku njia 87 zikiwa na wastani wa ujazo wa abiria wa asilimia 55 pekee, hali inayopunguza mapato., amesema CAG Kichere.

Aidha, amesema matumizi yasiyo bora ya ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300F yamechangia hasara hiyo, ambapo asilimia 90.4 ya safari zilikuwa za masafa mafupi na ya kati badala ya safari ndefu zenye mapato makubwa.

Kutokana na Hali hiyo ndege ilisimamishwa huku ikiendelea kugharimu shirika takribani Sh bilioni 3.5 kwa ukodishaji na bima bila kuzalisha mapato.

Pia CAG ameeleza kuwa udhaifu wa mifumo ya udhibiti umepelekea malipo ya Sh20.61 bilioni  kwa mawakala bila kuthibitishwa kuwafikia abiria, pamoja na marejesho ya fedha kwa abiria ya Sh 31.7milioni  yaliyofanyika bila nyaraka za kuthibitisha uhalali wake.

Akizungumza mara baada ya kupokea ripoti hizo, Rais Samia amesema  Serikali itachukua hatua kwa mujibu wa sheria kulingana na mapendekezo yaliyotolewa ili kuondoa mapungufu yaliyobainishwa kwa lengo la kuimarisha usimamizi na uwajibikaji wa rasilimali za umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks