Ripoti ya CAG: ATCL ilipata hasara ya Sh60 bilioni 2019-20
- CAG Charles Kichere amebaini pia kwa miaka mitano shirika hilo lilikuwa likipata hasara.
Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini kuwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) lilipata hasara ya Sh60 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2019/20 na kwamba kwa miaka mitano iliyopita pia halikuweza kupata faida yeyote.
Taarifa hiyo ya CAG inakuja katika kipindi ambacho ATCL imekuwa ikiwezeshwa kwa kiwango kikubwa katika kufanya biashara ikiwemo kupatiwa ndege mpya ili kuongeza wigo wa maeneo ya kuruka kupanua soko lake.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) Charles Kichere ameeleza leo Machi 28, 2021 wakati akiwasilisha ripoti za ukaguzi kwa mwaka 2019/20 kuwa hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya ATCL ili kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma na biashara.
“Katika ukaguzi wetu mwaka 2019/20 shirika letu la ndege tumegundua hasara mwaka huu ya Sh60 bilioni lakini kwa miaka mitano pia limekuwa likitengeneza hasara,” amesema Kichere.
“Kuna changamoto mbalimbali ambazo Serikali inabidi iziangalie ili Shirika letu liweze kutekeleza majukumu ipasavyo,” ameongeza Kicheere wakati akiwasilisha ripoti hizo kwa Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
ATCL ni moja ya mashirika ya ndege Afrika Mashariki ambayo yamekua kwa kasi zaidi katika upanuzi wa idadi yake ya ndege na safari tangu Serikali ya hayati John Magufuli iingie madarakani mwaka 2015.
Ndani ya miaka mitano, ATCL iliongeza ndege nane na inatarajia kuongezewa nyingi ambazo Serikali imeshazinunua.
Katika masuala mengine ya ukaguzi, Kichere amesema wamebaini kuwa baadhi ya mifumo “haiongei” na mianya ya kiusalama jambo linaloweza kufanikisha upotevu wa fedha za umma iwapo itaendelea kutumika kwa hali ilivyo.