Uuzaji wa mifugo nje ya nchi waiingizia Tanzania mabilioni
- Imepata tozo ya Sh5.5 bilioni ya kusafirisha mifugo nje ya nchi.
- Yaingiza Sh141.6 milioni ikiwa ni faini ya kutorosha mifugo bila kibali.
- Fedha hizo zimepatikana katika utekelezaji wa operesheni ya Nzagamba.
Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema Serikali imekusanya Sh5.5 bilioni hadi kufikia Aprili 30 mwaka huu kupitia operesheni Nzagamba ikiwa ni makusanyo ya tozo za kusafirisha mifugo nje ya nchi.
Mifugo hiyo, iliyosafirishwa nje kwa ajili shughuli mbalimbali ikiwemo biashara, inajumuisha ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Mpina ameliambia Bunge leo (Mei 14, 2020) wakati kiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2020/2021 kuwa kabla ya operesheni Nzagamba kulikuwa na ukwepaji mkubwa wa kulipa maduhuli ya Serikali yahusuyo biashara ya mifugo na mazao yake.
Amesema operesheni hiyo iliyoanza mwaka 2017/2018 imekuwa na mafanikio makubwa ambayo imesaidia kuipatia nchi Sh5.5 bilioni kama tozo za kusafirisha mifugo nje ya nchi.
Pia mifugo 3,363 (ngómbe, mbuzi na kondoo) iliyokuwa inatoroshwa kwenda nje ya nchi bila kulipiwa vibali na ushuru ilikamatwa na kutozwa faini yenye jumla ya Sh141.6 milioni.
“Udhibiti wa utoroshaji wa mifugo na mazao yake nje ya nchi umesaidia kuhamasisha ujenzi wa viwanda vipya vya nyama, maziwa na ngozi,” amesema Mpina jijini Dodoma.
Ng’ombe ni miongoni mwa mifugo inayoipataia Tanzania pesa hasa tozo na ushuru kwenye minada ya ndani. Picha| Mtandao.
Operesheni Nzagamba katika mwaka 2019/2020 ilitekelezwa katika maeneo matano ya kimkakati ya Nzega mkoani Tabora, Lamadi (Simiyu), Babati (Manyara), Longido (Arusha) na Handeni mkoani Tanga.
Aidha, Mpina amesema wamefanikiwa kudhibiti uingizaji wa mazao ya mifugo ambapo jumla lita za maziwa 5,621.3, kilo 303.69 za nyama na bidhaa zake, trei za mayai 1,012 zilikamatwa zikiwa zimeingizwa nchini kinyume cha sheria.
Katika mwaka 2020/2021, amesema wizara hiyo itaendelea kutathmini kodi, tozo na ada mbalimbali zitakazoonekana kuwa kero kwa wazalishaji na wafayabiashara ya mifugo na mazao yake ili kuzifuta au kuzifanyia marekebisho.
Soma zaidi:
- Bajeti ya Wizara ya Ulinzi yapaa kwa mara ya pili mfululizo.
- Bashungwa: Sijapewa fedha za maendeleo wizara ya viwanda, biashara 2019-2020
- Kamwelwe aomba matrilioni kugharamia ujenzi, uchukuzi Tanzania
Bajeti ya 2020/2021
Mpina ameliomba Bunge likubali kupitisha bajeti ya wizara yake Sh66.8 bilioni kwa mwaka 2020/2021 ambazo kati ya fedha hizo, Sh32.1 bilioni zitatumika ajili ya sekta ya mifugo na kiasi kilichobaki kitaenda sekta ya uvuvi.
Bajeti hiyo imeongezeka mara mbili kutoka Sh33.2 bilioni zilizotengwa mwaka 2019/2020.
Hata hivyo, hadi Aprili 30 mwaka huu wizara ilikuwa imepokea Sh13.34 bilioni za bajeti ya mwaka 2019/2020 ikiwa ni sawa na asilimia 40 tu ya bajeti yote huku ikiwa imesalia miezi miwili tu kukamilisha mwaka wa fedha.
Latest