Mafuta ya kula: Tanzania yatafuna mfupa mdogo mdogo
- Yaanza kupunguza uagizaji wa mafuta nje ya nchi.
- Yasambaza mbegu bora, mbolea na viuatilifu kwa wakulima.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inakusudia kuongeza kasi na kiwango cha uzalishaji wa mbegu za mafuta ya kula ili kuviwezesha viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa hiyo itakayosaidia kuokoa fedha zinazotumika kuagiza mafuta nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, uzalishaji wa mafuta ya kula nchini ni wastani wa tani 300,000 ikilinganishwa na mahitaji ya tani 650,000 kwa mwaka.
Kutokana na upungufu huo, Tanzania huagiza tani zipatazo 350,000 za mafuta ya kula ambapo hugharimu zaidi ya Sh470 bilioni kwa mwaka.
Upungufu wa uzalishaji wa mafuta nchini kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe unatokana na tija ndogo ya uzalishaji ambayo inachangiwa na upatikanaji mdogo wa mbegu bora, mbolea, viuatilifu, matumizi ya mbinu duni za uzalishaji na mabadiliko ya tabianchi.
Mafuta ya kula yanayozalishwa Tanzania yanatoka katika mazao ya alizeti, karanga, pamba, soya, nazi, chikichi na ufuta ambapo, alizeti huchangia asilimia 90 ya uzalishaji wote.
Nini kinafanyika kuokoa fedha hizo?
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuongeza uzalishaji wa mbegu za mafuta ya kula kwa kusambaza tani 2,000 za mbegu bora za alizeti zenye thamani ya Sh5.8 bilioni kwa utaratibu wa ruzuku kwa wakulima wa mikoa ya Singida, Dodoma, Simiyu na Manyara.
“Mbegu hizo zitazalisha tani 400,000 za alizeti ya kukamua mafuta ya kula tani 100,000,” alisema Waziri Bashe Mei 17, 2022 katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2022/23.
Soma zaidi:
-
Fursa zilizojificha uzalishaji wa michikichi Tanzania
-
Fursa ya mabilioni kilimo cha alizeti kwa vijana Tanzania
- Wakulima washauriwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kilimo cha umwagiliaji
Ufufuaji wa zao la chikichi
Bashe amesema wizara yake imeendelea kutekeleza mpango wa muda mrefu wa kuzalisha miche bora ya chikichi na kuigawa bure kwa wakulima ambapo jumla ya miche 896,029 imesambazwa kwa wakulima katika mikoa ya Kigoma, Mbeya Mtwara, Kagera, Katavi na Tanga 191 katika mwaa huu wa fedha unaoisha Juni 30.
“Vilevile, Wizara imehamasisha kampuni za usindikaji kuingia mikataba na wakulima ya kununua mbegu za mafuta ya kula,” amesema.
Hadi Aprili, 2022 wakulima 7,588 wa zao la alizeti wameingia mikataba na kampuni za Pyxus Agriculture Tanzania Ltd, Qstec, na Mwenge Sunflower Oil kutoka katika mikoa ya Dodoma, Singida, na Manyara ili kuzalisha tani 28,000 ambazo watawauzia kwa bei ya Sh750 kwa kilo.
Pia Serikali imeratibu majukwaa 52 ya majidiliano na sekta binafsi kwa mazao asilia ya biashara, nafaka, mikunde, bustani na mbegu za mafuta ya kula kwa ajili ya kutatua changamoto za kikodi na kisera.
Utekelezaji wa mikakati hiyo umeanza kuonyesha matumaini kuelekea katika kupunguza kabisa uagizaji wa mafuta ya kula na kuwawezesha wakulima kuzalisha mbegu za mafuta zitakazokidhi mahitaji yote ya ndani.
Uzalishaji waongezeka
Katika mwaka 2021/22 uzalishaji wa mbegu za mafuta umefikia tani milioni 1.7 ikilinganishwa na tani milioni 1.5 mwaka 2020/21 na huenda uzalishaji ukaongezeka miaka inayofuata ikizingatiwa kuwa Serikali imeongeza bajeti ya kilimo.
Latest



