Wabunge walia bajeti ya kilimo, wakitaka mageuzi
- Wasisitiza umuhimu wa teknolojia, utafiti na sera madhubuti kuinua tija ya kilimo nchini.
- Sekta ya kilimo yakua kwa 4.1% licha ya ongezeko la bajeti kwa zaidi ya asilimia 380.
Dar es Salaam. Licha ya Serikali kuongeza bajeti ya sekta ya kilimo wabunge wameelezea wasiwasi wao kuhusu ufanisi wa uwekezaji huo, wakitaka mabadiliko ya dhati yatakayoongeza tija, ushindani na masoko ya uhakika kwa wakulima.
Sekta ya kilimo inaongoza kwa kuchangia kiwango kikubwa cha pato la taifa (GDP) ikichangia kwa asilimia 26 ya Sh156 trilioni zilizoripotiwa mwaka 2024, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mipango na Uwekezaji.
Wakichangia bajeti kuu ya Serikali bungeni jijini Dodoma leo Juni 16,2025, wabunge wamesema kilimo bado kinakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo matumizi duni ya teknolojia, ukosefu wa utafiti wa kisasa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mbunge wa kuteuliwa, Prof Shukrani Manya amesema kuna haja ya kuongeza utafiti wa masuala ya kilimo hususan katika uzalishaji mazao ili yaweze kuuzika ndani na nje ya soko la Tanzania.
“Tanzania ukichukua mti wa mwembe au mchungwa mti huo huo unatoa matunda yaliyoiva mengine machachu mengine matamu ukichukua zabibu ukasema kwamba ni zabibu zilizoiva zingine ni chachu zingine ni tamu, sasa unavuna matunda ya jinsi hiyo uyauzie nani?” amesema.
Kenneth Nollo, Mbunge wa Bahi ameeleza kuwa bado zaidi ya theluthi mbili au asilimia 70 ya wakulima nchini wanategemea jembe la mkono, hali inayokwamisha uzalishaji mkubwa na wa kisasa.
Mbunge ataka majembe ya ng’ombe
Licha ya teknolojia ya sasa kujikita zaidi kwenye mashine za kisasa za kilimo, Nollo yeye anataika Serikali kuanzisha kiwanda cha kuzalisha majembe yanayokokotwa na ng’ombe ili kuchochea matumizi ya teknolojia rahisi vijijini.
“Tunahitaji kampeni mahususi ya kutoka kwenye jembe la mkono twende kwenye jembe la kukokotwa na ng’ombe kama ambavyo tulifanya kampeni mahususi ya kumtuat mama ndoo kichwani na kampeni mahususi ifanyike ya kuachana na jembe la mkono ,” amesema Nollo.
Mbali na changamoto za kiteknolojia, baadhi ya wabunge wanasema upatikanaji wa ardhi ni miongoni mwa masuala yanayopunguza kasi ya ukuaji kilimo cha kibiashara nchini.

Mbunge wa wa Jimbo la Kalenga Jackson Kiswaga amebainisha kuwa changamoto ya upatikanaji wa ardhi kwa wawekezaji ni kikwazo kikubwa katika kukuza kilimo.
Hivyo, amependekeza kuanzishwa kwa benki ya ardhi ili kurahisisha uwekezaji mkubwa wenye manufaa kwa wakulima wa ndani.
“Tanzania tunayo ardhi kubwa yenye rutuba lakini hatuna akiba ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji. Tukianzisha benki ya ardhi, tutaweza kuwavuta wawekezaji wakubwa na kupata masoko na teknolojia kwa wakulima wetu,” ameeleza Kiswaga.
‘Maisha ya wakulima ni duni’
Baadhi ya wabunge wanaona kuwa maisha ya wakulima na wavuvi hayaendani na uhalisia wa ukuaji wa uchumi, jambo linaloowaacha katika lindi la umaskini.
Prof Patrick Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, amesema Serikali inapaswa kuweka kipaumbele katika uwekezaji wa kilimo kwa watu wa vijijini ili kuinua maisha yao.
“Tunaambiwa pato la mtu mmoja ni linakadiliwa kuwa Dola za Marekani 1,090 (Sh2.78 milioni ) kwa mwaka, lakini ukweli kule vijijini kuna watu hawafikii hata Dola (za Marekani) 100 kwa mwaka. Hayo ni mahesabu ya makaratasi tu,” amesema Prof Ndakidemi.
Kamati ya kudumu ya Bunge ya bajeti inaeleza kuwa licha ya Serikali kuongeza bajeti bado sekta ya kilimo inakabiliwa na ufanisi duni.
Bajeti juu, ufanisi kidogo
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya bajeti Oran Njeza, bajeti ya kilimo imeongezeka zaidi ya mara nne ndani ya miaka minne kutoka Sh294 bilioni katika mwaka wa fedha 2021/22 hadi Sh1.249 trilioni kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Hata hivyo, Njeza amesema sekta hiyo imekua kwa asilimia 4.1 pekee mwaka 2024, jambo ambalo wabunge wanaliona kama ishara ya ukosefu wa ufanisi wa matumizi ya rasilimali hizo.
Latest



