Utegemezi wapungua kwa asilimia 4.3 Tanzania
- Ni kutokana na kupungua kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18.
- Yatajwa kuwa ni ishara nzuri kwa maendeleo ya nchi.
- Dar es Salaam na Kusini Unguja kuna uwiano mdogo zaidi wa utegemezi huku Kigoma, Simiyu na Katavi uwiano ukiwa juu.
Dar es Salaam.Wakati watoto wenye umri chini ya miaka 18 wakiendelea kupungua Tanzania, uwiano wa umri wa utegemezi nao umepungua jambo linaloashiria ongezeko la nguvukazi muhimu katika ukuaji wa uchumi.
Ripoti ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 iliyozinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwishoni mwa wiki inaeleza kuwa asilimia ya watoto wenye umri chini ya miaka 18 imeendelea kupungua kutoka asilimia 50.1 mwaka 2012 hadi asilimia 49 mwaka 2022 kwa Tanzania Bara.
Kwa upande wa Zanzibar imepungua kutoka asilimia 49 mwaka 2012 hadi asilimia 47 mwaka jana.
Ripoti hiyo ambayo imetolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema pia kuwa uwiano wa umri tegemezi nchini Tanzania umepungua kutoka asilimia 91.5 mwaka 2012 hadi asilimia 87.1 mwaka 2022 kwa Tanzania.
Hiyo ni sawa kusema utegemezi umepungua kwa asilimia 4.3 ndani ya kipindi cha miaka 10.
“Uwiano (wa umri tegemezi) umepungua kutoka asilimia 91.7 hadi asilimia 87.4 katika kipindi hicho kwa Tanzania Bara. Aidha kwa Tanzania Zanzibar, uwiano umepungua kutoka 83 mwaka 2012 hadi 77.7 mwaka 2022,” imebainisha ripoti hiyo.
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa aliyekuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo Aprili 15, 2023 alisema kuwa kupungua kwa hali ya utegemezi kunamaanaisha nchi ina hazina kubwa ya nguvu kazi ambayo iko katika umri huo ambayo ni kichocheo kikubwa cha uchumi.
“Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania wote wako kwenye umri wa miaka 15 hadi 64. Hii ni ishara nzuri katika maendeleo ya nchi kwa kuwa wingi wa watu wenye umri huu una uhusiano wa kupungua wa uwiano umri tegemezi,” alisema Waziri Mkuu.
Nchini Tanzania mtu anapofikisha umri wa miaka 18 hutambulika rasmi kisheria kama mtu mzima na kuwa na uwezo wa kuajiriwa rasmi pamoja na kuwa na uwezo wa kumiliki mali.
Soma zaidi
-
Ahueni, maumivu: Bei za vyakula zikianza kushuka Mwanza
-
Uhaba wa walimu bado wazitesa shule za msingi, sekondari Tanzania
Hivi karibuni Takwimu mpya za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zimeonesha kuwa pato la Taifa la Tanzania kwa bei ya sasa limeongezeka hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 85.42 sawa na Sh200 trilioni mwaka 2023 kutoka Dola za Marekani Bilioni 69.9 sawa na Sh 163.5 trilioni kwa mwaka 2021.
Pamoja na kuwepo kwa sera nzuri za uchumi ambako kunatajwa kuwa sababu ya ongezeko hilo, uwepo wa nguvu kazi ya kutosha unarahisisha utekelezaji wa sera hizo na hii inaweza kuwa sababu ya kiwango cha utegemezi kushuka.
Uwiano wa watu walio katika umri tegemezi ni nini
Kwa mujibu wa ripoti za matokeo ya Sensa, huo ni uwiano kati ya watu walio katika umri tegemezi ambao ni wenye umri chini ya miaka 15 na wale wenye umri wa miaka 65 na zaidi ikilinganishwa na idadi ya watu wenye umri wa kufanya kazi yaani wenye miaka 15 hadi 64.
Uwiano huu hupatikana kwa kujumlisha watu wote wenye umri chini ya miaka 15 na wale wenye umri wa miaka 65 na zaidi na kugawanywa kwa watu wote wenye umri wa miaka 15-64 na kuzidishwa kwa 100.
Mikoa mitano yenye kiwango kikubwa cha umri wa utegemezi
Uwiano wa umri tegemezi ni mkubwa zaidi katika Mkoa wa Simiyu ambao una wastani wa asilimia 119.3. Hiyo ni sawa kusema kwa kila watu 1,000 wa mkoa huo, basi 119 ni tegemezi.
Mkoa wa Simiyu unafuatiwa na mikoa ya Tabora na Katavi yenye uwiano wa takriban asilimia 109.7 kila moja, kisha Kigoma wenye asilimia 109.3 na Rukwa wenye asilimia 108.9.
Aidha, mikoa yenye uwiano mdogo wa umri tegemezi ni Dar es Salaam wenye asilimia 51.3, Kusini Unguja kwa asilimia 67.6 pamoja na Kusini Magharibi wenye asilimia 67.9.
Hali hiyo inatoa tafsiri gani?
Isdory Mgoroka ambaye ni mchambuzi wa masuala ya uchumi nchini Tanzania ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kupungua kwa utegemezi ni matokeo ya mabadiliko ya sera mbalimbali za maendeleo, kurahisisha upatikanaji wa huduma pamoja na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
“Kuna sera nyingi ambazo utekelezaji wake umesaidia kupunguza utegemezi, ikiwemo utoaji wa mikopo kwa vikundi, vile vile kukua kwa teknolojia kumerahisisha mambo mengi, hivi sasa watu wanaweza kufanya kazi na kujiingizia kipato kupitia mifumo ya kidijitali,” amesema Mgoroka.
Licha ya uwiano wa umri wa utegemezi kupungua Mgoroka, amebainisha kuwa kiwango hicho kilichopungua ndani ya miaka 10 si cha kujivunia badala yake Serikali na wananchi wanapaswa kushirikiana ili kupunguza zaidi uwiano wa umri wa utegemezi.
“Kwanza Serikali inapaswa kuziba mianya ya ubadhirifu, huko kuna upotevu mkubwa wa fedha ambazo zingeweza kuongeza tija katika kuboresha uchumi na kuinua maisha ya Watanzania, uchumi hauwezi kukua ikiwa kuna ubadhirifu,” amesisitiza Mgoroka.
Kauli hiyo ya Mgoroka inakuja zikiwa zimepita siku chache tu tangu Ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2021/22 kuonyesha kuna upotevu mkubwa wa pesa katika miradi na mashirika ya umma ambapo uchunguzi umetakiwa kufanyika ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Latest