Usiyoyafahamu ripoti ya matokeo ya sensa mwaka 2022
- Yabainisha kuongezeka nguvukazi, idadi ya wanaojua kusoma na kuandika.
- Watoto chini ya miaka 18 wanedelea kupungua.
- Asilimia 99.5 ya kaya zote za Tanzania zina vyanzo vya maji.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua ripoti za matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 huku akibainisha mambo mbalimbali yaliyopo katika ripoti hiyo ikiwemo kiwango cha Watanzania kujua kusoma na kuandika kuongezeka kwa asilimia 7.1 ndani ya miaka 10.
Majaliwa aliyekuwa akizindua ripoti hizo leo Aprili 15, 2023 visiwani Zanzibar amesema matokeo ya sensa yamebainisha baadhi ya viashiria muhimu kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo wastani wa ongezeko la watu, hali ya upatikanaji wa huduma za kijamii na makazi.
Mtendaji huyo mkuu wa shughuli za Serikali amesema kiwango cha watu wenye umri wa miaka mitano na kuendelea cha kujua kusoma na kuandika kimeongezeka hadi asilimia 79.1 mwaka 2022 kutoka asilimia 72 mwaka 2012.
Hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 7.1 ndani ya miaka 10.
“Kiwango cha jumla cha uandikishaji kwa wanafunzi ngazi za shule za msingi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimefikia asilimia 95.9 kwa mwaka 2022 kutoka asilimia 94.6 mwaka 2012,” amesema Majaliwa huku akibainisha kuwa uboreshaji wa elimu unaofanywa na Serikali umechangia watoto wengi kwenda shule.
Amesema kuongezeka kwa watu walioelimika kuna mchango chanya katika maendeleo ya Taifa kwa sababu watu wanapata stadi muhimu za maisha kuendesha uchumi na kujipatia kipato.
Kwa mujibu wa Majaliwa, ripoti hiyo imebainisha kuwa kiwango cha watu wanaoishi maeneo ya mijini kimeongezeka kutoka asilimia 30 mwaka 2012 hadi asilimia 35 mwaka 2022, japokuwa kasi ya uhamiaji mijini imepungua ikilinganishwa katika kipindi cha mwaka 2002 hadi mwaka 2012.
“Katika kipindi hicho kasi ya uhamiaji ya watu kutoka vijijini kwenda mijini ilikuwa asilimia 5.2 ukilinganisha na kasi ya asilimia 4.8 ya mwaka 2012 hadi mwaka 2022,” amesema Majaliwa.
Amesema matokeo hayo ni uboreshaji wa huduma za kijamii na kiuchumi katika maeneo ya vijijini, jambo linalowafanya watu wasikimbilie zaidi mijini.
#Sensa2022 Wizara za Fedha na Mipango kwa pande zote mbili shirikianeni na Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar kuendelea kutoa mafunzo ya matumizi ya matokeo ya sensa ya mwaka 2022-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pic.twitter.com/N3uJyBYbQI
— Ofisi ya Waziri Mkuu (@TZWaziriMkuu) April 15, 2023
Idadi ya watoto chini ya miaka 18 inapungua
Amesema asilimia ya watoto wenye umri chini ya miaka 18 imeendelea kupungua kutoka asilimia 50.1 mwaka 2012 hadi asilimia 49 mwaka 2022 kwa Tanzania Bara.
Kwa upande wa Zanzibar imepungua kutoka asilimia 49 mwaka 2012 hadi asilimia 47 mwaka jana.
“Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania wote wako kwenye umri wa miaka 15 hadi 64. Hii ni ishara nzuri katika maendeleo ya nchi kwa kuwa wingi wa watu wenye umri huu una uhusiano wa kupungua wa uwiano umri tegemezi,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema hiyo ina tafsiri kuwa nchi yetu ina hazina kubwa ya nguvu kazi ambayo iko katika umri huo ambayo ni kichocheo kikubwa cha uchumi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 99.5 ya kaya zote za Tanzania zina vyanzo vya maji ambapo kati ya vyanzo hivyo, takriban vyanzo saba kati ya 10 vimeboreshwa.
Soma zaidi:
Makazi na mawasiliano nako poa
Majaliwa amesema asilimia 63.3 ya kaya zote zina nyumba yenye kuta bora, asilimia 84.8 zina nyumba zenye paa bora huku zaidi ya nusu (asilimia 56.9) zina sakafu bora.
Kuhusu mawasiliano, amesema yameimarika ambapo asilimia 97.5 ya vitongoji, mitaa na shehia za Zanzibar na Tanzania Bara zimefikiwa na mitandao ya simu.
“Takwimu hizi zinaonyesha maendeleo wezeshi ya kutekeleza uchumi wa kidijitali nchini,” amesema Majaliwa huku akiwataka Watanzania kutumia vizuri fursa hiyo kukuza uchumi kwa kufanya biashara na kuimarisha mahusiano na mawasiliano.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar Hemed Suleiman Abdulah wakizindua Ripoti ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi 2022, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)- Tunguu. Picha | Ofisi ya Waziri Mkuu.
Atoa maagizo
Mara baada ya kubainisha baadhi ya matokeo muhimu yanayopatikana katika ripoti za sensa, Waziri Mkuu ameagiza wadau na wananchi kutumia kikamilifu matokeo ya sensa kufanya maamuzi sahihi katika shughuli zao za maendeleo.
Pia watendaji wa Serikali wanaohusika na mipango kutumia takwimu za sensa katika shughuli zao za kila siku ili kuongeza ufanisi katika kuwahudumia Watanzania kupitia huduma za kijamii katika maeneo yao.
Amesema elimu na kampeni ya matokeo ya sensa ziendelee ili kuwasaidia Watanzania kupanua uelewa na matumizi ya takwimu za sensa huku akiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kushirikiana na wadau wengine kupanga mipango miji ili kuondoa makazi holela nchini.
“Serikali ya Tanzania iko katika hatua za mwisho za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya mwaka 2025 sambamba kuandaa dira nyingine ya mwaka 2050. Matokeo ya Sensa ya mwaka 2022 ni muhimu sana kwani yatatumika kufanya tathmini ya utekelezaji wa mipango ambayo imeainishwa kwenye dira ya mwaka 2025 na kupitia taarifa hizo tunaweza kujipima, kujitathmini tulikotoka, tulipo na tunakoelekea,” amesema Majaliwa.
Uzinduzi wa ripoti hizo utafuatiwa na matukio mengine yatakayofanyika awamu kwa awamu kulingana na ratiba ya utoaji wa matokeo ya sensa.