Utegemezi wa kifedha waongezeka Tanzania
- Waongezeka kwa asilimia tano ndani ya miaka sita.
- Watu 2,280 kati ya 9,915 walioshiriki katika utafiti huo nchini Tanzania ni tegemezi.
Dar es Salaam. Wakati dunia ikiendelea kupambana na changamoto ya ukosefu wa ajira, ripoti ya mpya ya Finscope inaonyesha hali ya utegemezi kifedha kwa mtu mmoja mmoja imeongezekaa nchini.
Ripoti hiyo iliyotolewa Julai 10, 2023 na Mfuko wa Kuendeleza Huduma za Fedha Tanzania (FSDT) inasema utegemezi umeongezeka kwa asilimia tano ndani ya miaka sita.
FinScope ni utafiti unaofanyika katika nchi 13 za Afrika ukitoa maarifa kuhusu mahitaji ya kifedha, na tabia za watumiaji kuanzia umri wa miaka 16 na kuendelea.
Utafiti huu pia hutoa taarifa za kuaminika na mienendo ya ujumuishi wa kifedha Tanzania bara na Zanzibar.
Mwaka 2017 nchini Tanzania Utafiti huo ulibaini kulikuwa na asilimia 18 za utegemezi kifedha zilizoongezeka hadi kufikia asilimia 23 mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo Watanzania 2,280 kati ya 9,915 walioshiriki katika utafiti huo hutegemea fedha za watu wengine ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Utafiti wa FSDT unabainisha kuwa idadi hiyo ya watu ilikusanya Sh2.5 milioni ndani ya kipindi cha miaka sita kutokana na utegemezi wa kifedha.
Mwaka 2017 fedha hizo zilikuwa Sh5 milioni ambayo imeongezeka hadi kufikia Sh7.9 milioni mwaka 2023.
Aidha, ripoti hiyo pia imeonesha kuporomoka kwa idadi ya watu wanaojishughulisha na kilimo na uvuvi, shughuli zinazotajwa kuchangia upatikanaji wa fedha kwa watu wengi nchini.
“Kumekuwa na mabadiliko katika chanzo cha msingi cha mapato kutoka kilimo na uvuvi kuelekea kazi ya kawaida na utegemezi,” imesema ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo Wakulima na wavuvi nchini Tanzania wamepungua kwa asilimia 13 ndani ya miaka 6.
Soma zaidi
-
Utegemezi wapungua kwa asilimia 4.3 Tanzania
-
Uhaba wa walimu bado wazitesa shule za msingi, sekondari Tanzania
Mwaka 2017 kulikuwa na asilimia 42 ya watanzania wanaojishughulisha na kilimo na uvuvi idadi iliyoporomoka hadi kufikia asilimia 28 kati ya wale waliohojiwa katika utafiti huo.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya wizara yake bungeni kwa mwaka 2023/24 amesema jumla ya kaya milioni tano sawa na asilimia 43.6 ya kaya zote Tanzania Bara zinategemea kilimo moja kwa moja.
Hata hivyo, Ripoti ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/ 2020 inaonyesha kuwa kaya zinazojishughulisha na uvuvi nchini Tanzania ni chini ya asilimia moja.
Hiyo ni sawa na kusema kati ya kaya zaidi ya milioni 11.6 zilizopo Tanzania ni kaya 120,078 au pungufu zaidi ya hizo zinayojishugulisha na uvuvi.
Latest