BOT, wadau wa fedha kushirikiana kuongeza ujumuishi wa kijinsia, ufikiaji huduma za kifedha Tanzania

March 5, 2025 8:14 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Kupungua kwa pengo la uwiano wa ufikiaji wa huduma za kifedha kutawawezesha wanawake kupunguza umasikini  na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Dar es Salaam. Huenda Tanzania ikashuhudia ongezeko la ufikiaji wa huduma za kifedha kwa wanawake, mara baada ya wadau wa masuala ya fedha ikiwemo benki na taasisi za kimataifa kufanya mkutano wa kujadili mikakati ya kupunguza pengo la ujumuishi wa kijinsia katika ufikiaji wa huduma za kifedha lililopo hivi sasa.

Utafiti wa Finscope wa mwaka 2023 umebainisha kuwa pengo la ujumuishi wa kijinsia nchini Tanzania katika masuala ya kifedha limepungua kutoka asilimia 10 mwaka 2017 hadi asilimia 3 mwaka 2023. 

Hata hivyo, bado kuna upungufu wa ufikiwaji wa huduma za kifedha kwa wanawake kwa asilimia 19.4 ukilinganisha na wanaume ambao pia umepungua kutoka asilimia 30 iliyokuwepo mwaka 2017.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam leo Machi 5, 2025 kuwa mkutano huo utawakutanisha viongozi wa juu wa benki watakaojadiliana namna ya kupunguza pengo lililopo ili kufikia uwiano wa asilimia 50 kwa wanaume na wanawake katika ufikiaji wa huduma za kifedha ifikapo mwaka 2033.

Tutuba ameongeza kuwa pengo la ufikiaji wa huduma za kifedha kwa wanawake hukwamisha kasi ya maendeleo kwa kupunguza ukuaji wa uchumi na uendelevu  kupitia huduma mbalimbali za kifedha ambazo wanawake wangezifanya ikiwemo kukopa, kuweka akiba pamoja na kufanya miamala.

“Mkutano wa leo utajadili fursa zilizopo na namna tunavyoweza kuzitumia kutatua changamoto zitakazondoa tofauti kati ya wanawake na wanaume katika upatikanaji wa huduma za kifedha nchini…Lengo hili limewekwa mpaka kufikia mwaka 2033 limezingatia mazingira tuliyonayo na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 – 2050 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha ,” amesema Tutuba.

Aidha, Gavana Tutuba ameongeza kuwa, kupungua kwa pengo la uwiano wa ufikiaji wa huduma za kifedha kutawawezesha wanawake kupunguza umaskini kwa kuwaongezea vipato kupitia shughuli za kiuchumi jambo litakalochochea maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya  Mabenki Tanzania (TBA) Theobald Sabi amesema taasisi anayoiongoza ina dhamira ya kushughulikia changamoto ya pengo la ujumuishi wa kijinsia katika ufikiaji wa huduma za kifedha kwa wanawake.

Sabi amesema wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa huduma mahususi kwa wanawake kama mikopo, kufungua akaunti maalumu za wanawake na kutoa elimu ya fedha ili wanawake nao wanufaike na upatikanaji wa huduma za kifedha.

“Maendeleo ya biashara zinazomilikiwa au kuongozwa na wanawake yatakuwa na faida mtambuka kwenye uchumi na jamii na kwetu sisi mabenki hiyo ni biashara na hiyo ni kuongeza idadi ya wateja wetu,” amesema Sabi.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...