Usafiri, bidhaa za vyakula vyapaisha mfumuko wa bei kwa asilimia 0.8 Tanzania

May 12, 2026 5:14 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Mfumuko wa bei wafikia asilimia 4.0 kwa mwaka unaoishia Aprili, 2026.
  • NBS yasema kiwango hicho ni cha wastani ikitazamia kuongezeka zaidi.
  • Wachambuzi wa uchumi watia neno.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini kwa mwezi Aprili 2026 umefikia asilimia 4.0 kutoka asilimia 3.2 kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2026 ikichangiwa zaidi na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa usafiri na bidhaa za vyakula.

Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2026 imeongezeka kwa asilimia 0.8 ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2026.

Taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei nchini iliyotolewa Mei 8, 2026 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa kiwango cha bei ya usafiri kimeongezeka kwa asilimia 5.2 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja hali iliyochangia kupaa kwa mfumuko huo.

Huenda ongezeko hili limechochewa  na kupaa kwa bei ya mafuta duniani kunakotokana na vita vinavyoendelea kati ya Marekani, Israeli na Iran.

Vita hivyo vilivyoanza mwishoni mwa Februari, 2026 vimesababisha  gharama ya mafuta yanayopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi Aprili kufikia Sh4,115 kwa petroli na dizeli Sh4,248 kwa lita baada ya Serikali kuweka ruzuku ya Sh259 kwa kila lita kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).

Kufuatia ongezeko hilo la mafuta lililoanza Machi, 2026 Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilitangaza bei mpya ya nauli kwa vyombo vya usafiri wa umma ikiwemo daladala iliyoanza kutumika Mei Mosi mwaka huu suala lililowaacha watumiaji wa usafiri huo katika maumivu.

Mara ya mwisho kiwango cha mfumuko wa bei kufikia asilimia 4.0 ilikuwa Mei 2023 na miezi iiyofuatia kiwango hicho kimekuwa kikipanda na kushuka kwa wastani wa kati ya asilimia 3.9 hadi 3.0.

Pamoja na kupaa huko kwa mfumuko wa bei NBS imesema ongezeko hilo bado ni la wastani ikitazamia kuongezeka zaidi.

“Kiwango cha mfumuko wa bei pia umekuwa na mwenendo imara kwa ujumla jambo linaloashiria utulivu wa bei kwa ujumla huku kukiwa na shinikizo la mfumuko wa bei linaloongezeka kwa kiwango cha wastani kuelekea mwisho wa kipindi,” imesema taarifa ya NBS.

Pamoja na usafiri, mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi umeongezeka hadi asilimia 5.7 kutoka asilimia 5.5 iliyorekodiwa kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2026.

Kwa upande mwingine, mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Aprili, 2026 umeongezeka hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 2.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2026.

Wachambuzi wa uchumi watia neno

Mtaalamu wa masuala ya fedha na uchumi kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Abel Kinyondo amesema changamoto kubwa zaidi hutokea pale mfumuko wa bei unapoongezeka wakati ajira na vipato vya wananchi haviongezeki. 

“Bidhaa za chakula zikianza kuwa bei kubwa wakati wewe huwezi ‘ku-afford’(kumudu gharama), inabidi uanze kupunguza aina ya vyakula au hata idadi ya milo,” amesema akieleza hali hiyo inaweza kuongeza umaskini wa chakula na kupunguza uwezo wa wananchi kuweka akiba au kuwekeza.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya uchumi na fedha Paulo Chengula amesema kupanda kwa mfumuko wa bei kunamaanisha moja kwa moja maisha ya Mtanzania wa kawaida yanaathirika kwa sababu fedha nyingi zinaishia kwenye matumizi ya msingi badala ya akiba au maendeleo binafsi. 

“Mwananchi anatakiwa sasa ajiandae na awe na bajeti, aache baadhi ya matumizi ambayo sio ya muhimu,” amesema.

Wachambuzi hao pia wameishauri Serikali kutumia sera za muda mfupi kupunguza makali ya maisha kwa wananchi, ikiwemo kupunguza baadhi ya kodi na kuweka mazingira yatakayochochea uzalishaji wa bidhaa nyingi zaidi sokoni. 

Wamesema hatua hizo zinaweza kusaidia kushusha bei za bidhaa muhimu na kupunguza presha ya mfumuko wa bei katika kipindi hiki cha changamoto za uchumi wa dunia.

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Sin

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Sin

Nukta TV

Mizinga ya heshima, Rais Samia akimpokea Rais wa Singapore, Ikulu Dar es Salaam

Mizinga ya heshima, Rais Samia akimpokea Rais wa Singapore, Ikulu Dar es Salaam

Nukta TV

Mikakati ya Serikali kuhakikisha walimu wa VETA wanapata ajira na mikopo

Mikakati ya Serikali kuhakikisha walimu wa VETA wanapata ajira na mikopo

Nukta TV