Urembo wa ‘filters’ unavyoweza kuangamiza vijana wa Tanzania

November 20, 2020 12:48 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Filters ni teknolojia inayomuwezesha mtumiaji kuhariri picha ama video zake kwa kuweka vikolombwezo kibao.
  • Teknolojia hiyo inaweza kuhatarisha mahusiano ya watu na kusababisha sonona.
  • Watu washauriwa kuwa na kiasi wakati wa kuitumia. 

Baada ya kuona picha yake katika mtandao wa kijamii wa Instagram, alivutiwa naye. Kwa kuwa hakuwa na namba yake ya simu, aliamua kumtumia ujumbe mfupi kupitia mtandao huo mashuhuri kwa picha na video.

Uamuzi wa Makeke kumtumia ujumbe huo mfupi maarufu kama DM binti huyo ulikuja baada ya kufuatilia mwenendo wa picha na comments anazoweka. Hakika alikuwa tofauti na mabinti wengine.

Muda mwingi aliweka picha zake akiwa anaenda au kutoka kanisani. Aliweka picha akiwa nyumbani na marafiki warembo.

Kwa urembo wake katika picha hizo, kila mtu alikuwa akivutiwa kutoa maoni katika ukurasa huo wa Instagram. 

Ukiingia kwenye ukurasa wake hukosi watu 300 waliopenda ama ‘kulike’ alichoposti katika mtandao huo. Hata wanaomfuata si haba. Ni zaidi ya wafuasi 12,000.

Licha ya kutuma ujumbe wake mara kwa mara, haukujibiwa. Siku moja baada ya miezi mitatu alijibiwa na mrembo huyo na kisha baadaye walibadilishana namba za simu.

Jamaa alionekana kuchanganyikiwa. Hakuamini kama jitihada na mipango yake imeanza kuzaa matunda. Kwa wakati huo hakuwa ana sababu ya ‘kuslaidi DM’ tena. Ni mwendo wa kupiga soga Whatsapp. Huko ni picha nawe, video nawe ambazo alikuwa akiziona mwenyewe yaani ‘exclusive’.

Baada ya miezi kama mitatu mingine tangu waanze mawasiliano yao, bwana huyo alifunga safari na kuja Dar es Salaam kuonana na binti. Alijiiba kazini kwake huko Makete mkoani Njombe ili aonane na mtoto.

Alikuwa tayari kuhatarisha kibarua chake akutane na mrembo huyo hata kwa dakika moja. Picha na video alizotumiwa hazikufaa tena. Alitaka kitu mubashara.

Kama kawaida, alifikia nyumbani kwa shemeji yake Mbagala Mission. Walipanga wakutane kituo cha basi cha Makumbusho Jumamosi Saa tisa alasiri ili watafute kwa pamoja pahala pa kukutana na kupata angalau chakula cha jioni.

Kila mtu alikuwa akimsubiria mwenzie waonane kwa hamu. Bwana huyo aitwaye Makeke aliwaza kila aina ya mtindo ambao angetumia kumlaki ‘malkia’ wake mpya. Alipanga baada ya kuonana naye ampatie binti huyo mtaji wa biashara aliokuwa amemuomba.

Jambo ambalo wengi hatufahamu ni kwamba huenda filters zikaharibu mahusiano yetu, kutukosesha kazi ama kutuletea sonona katika maisha yetu.Picha|Najm Consultant.

Ilifika Jumamosi waliyopanga kukutana. Wakati wote akiwa njiani Makeke alikuwa akiwasiliana na mrembo huyo ambaye alikuwa amekaribia sana kufika kituoni kwa kuwa anakaa Boko Basihaya. Binti alikuwa wa kwanza kufika Makumbusho.

Makeke alivyofika alipiga simu kujua mrembo amekaa wapi. Ili kufahamu akamwambia binti amwambie rangi au aina ya nguo alizovaa au anyooshe mkono ili amuone. Wakati akiendelea kuangaza huku na huko alimuona mtu aliyenyoosha mkono akiwa tofauti na yule aliyekuwa akichati naye wakati wote.

Binti wa mtandaoni alikuwa mweupe pee kama theluji wakati yule aliyemuona akimwelekeza alama alikuwa na ngozi nyeusi ambayo hata baada ya kupaka urembo haikuwa imebadilika sana kiasi cha kufikia hata moja ya 10 ya anayeonekana kwenye picha na video.

Makeke alijipa moyo na kumsogelea yule mtu aliyekuwa akiwasiliana naye. Furaha aliyekuwa nayo na mipango ya mitindo ya kumlaki ilipotea ghafla. Alihamaki kidogo. Wewe ndiyo “Nunu”? Makeke aliuliza? Binti akasema ndiye mimi kwa mapozi huku akitia kogo kidogo.

Makeke akijitutumua kidogo. “Mbona upo tofauti na yule wa kwenye mtandao? Kuna mtu kakutuma?” Makeke aliuliza. Nunu alijibu “Ni mimi mwenyewe hausikii sauti yangu?” Makeke alitingisha kichwa kuitikia kana kwamba amekubaliana na Nunu.

“Inakuwaje picha na video unazoposti ama kunitumia zinakuwa tofauti na naniyemuona?” Nunu alitabasamu na kucheka kidogo.

“Babu weee, ni mambo ya ‘filter’ hayo”. Nunu alisema. “Filter?” Makeke alihoji. Tofauti na vijana wengine, Makeke si mtundu wa mitandao ya kijamii na matumizi ya simu janja.


Soma zaidi: 


Ana ujuzi wa msingi tu wa kupiga picha au kuchukua video na kuituma licha ya kuwa ni mtu mwenye shahada ya udaktari wa binadamu. Mara nyingi hupuuza ushauri wa simu janja ambao humtaka kuhariri au kutia mbwembwe kwenye picha ama video zake. Hivyo filter ilikuwa ni mpya kwake.

“Huwa nazihariri picha zangu kwa filter, unaweza ukavaa miwani hata kama hauna. Unaweza hata kujitengeneza kuwa na asili ya Mchina. Hakuna kinachoshindikana kwenye filter,” Nunu alisema akijaribu kumwelewesha Makeke.

Filters ni teknolojia inayomuwezesha mtumiaji kuhariri picha ama video zake kwa kuweka vikolombwezo kibao ikiwemo kuufanya uso kuwa nyororo, kubadili rangi na hata kuweka masikio ya Sungura kwenye kichwa cha mtu.

Makeke alibaki ameduwaa. Dakika 20 zinaenda bado wamesimama Makumbusho. Mipango yao ilianza kuharibika.

“We mwanamke siyo mwaminifu,” Makeke mtoto aliyelelewa kwenye misingi mikali ya kidini alisema kwa sauti yenye mikwaruzo.

Wawili hao walikuwa wamepanga mengi. Makeke alikuwa amemuahidi Nunu kumpatia mtaji wa Sh4 milioni mara baada ya kuonana na kuhakikishiana uchumba. 

Nunu tangu amalize chuo miaka minne iliyopita hakuwahi kupata kazi wala kibarua cha muda mfupi ambacho kingemwingizia kipato. Zaidi aliwahi kupata Sh100,000 baada ya kuposti tangazo kwenye akaunti yake ya Instagram. Mteja huyo hakuwahi kurudi tena.

Aliamini kujitengeneza kwenye mtandao na kuposti kungempa mpunga lakini hadi sasa hali ya maisha inakuwa ngumu kwa kuwa wateja hawapo.

Makeke kwa miezi mitatu ndiyo alikuwa mtu wa karibu aliyekuwa akimsaidia Nunu kukabiliana na kadhia ndogondogo za kifedha nyumbani alikokuwa akiishi na dadake ikiwemo dharura pale alipoumwa kwa kuwa hakuwa na bima ya afya.

“Nitamshawishi vipi Makeke ili anipende na kunikubali kama zamani?” Nunu alijiuliza kimoyo moyo. Makeke alionekana hayupo Makumbusho kabisa. Macho yake yalikuwa yakishangaa shangaa magorofa mapya yanayoendelea kuibuka kama uyoga katika Barabara ya Bagamoyo.

“Naomba niende,” Makeke alisema. “Kwanini unanifanyia hivi?” Nunu alihoji akimshika mkono Makeke ili waendelee na mazungumzo. “Naomba unisamehe,” aliongeza. Ni mambo ya mitandao tu,” alisema kwa sauti ya chini iliyoonekana kuwa na majuto.

“Mipango yote tuliyopanga imeshakufa Nunu. Tuendelee na maisha mengine,” alisema Makeke huku akiangaza angaza bodaboda ili akimbilie Ubungo kukata tiketi ya kurejea Njombe na kisha kwenda Makete. Nunu alimuona Makeke akitokomea taratibu kwenye kundi la watu waliokuwa wakihaha kusaka usafiri.

Alipiga simu mara kadhaa bila mafanikio. Alituma ujumbe karibia bando likate, hakujibiwa. Jasho jembamba lilikuwa likimtoka. Alikuwa na majuto moyoni. Mtaji aliohidiwa na Makeke ambao alikuwa amebakiza kidogo tu kuuweka kibindoni, uliyeyuka. 

Mapenzi yaliyokuwa yameanza kuchanua kupitia mtandao yalitokomea.

Filters zisipotumika vizuri zinaweza kuwa chanzo cha kuharibika kwa mahusiano. Picha| Huffington Post.

Nunu ni miongoni mwa mamia ya wanawake wa Tanzania ambao hutumia teknolojia za mitandao ya kijamii kubadilisha muonekano wao kiasi cha sura au maumbo yao kubadilika kabisa kuliko uhalisia. 

Tamaa ya kuonekana wenye sura na maumbo mazuri au wenye mafanikio inaenda na gharama kama iliyomkuta Nunu na nyingine lukuki za kiafya.  

Wataalamu wa afya na saikolojia wanasema kuwa tabia ya matumizi ya mitandao ya kijamii kupita kiasi na kujibadili mwonekano ina athari kubwa kwa mwanadamu.

“Instagram imekuwa ikihusishwa na dalili za sonona na hali ya wasiwasi au uoga uliopitiliza (anxiety). Wasiwasi huo ama sonona inayohusiana na mwonekano wa mwili huchochea mtu kutoridhika na mwonekano wa mwili wake au kutojikubali kabisa katika maisha yake,” Peace Amadi, mtaalamu wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha California alinukuliwa na jarida la Women Health Magazine la nchini Marekani.

Mtaalamu huyo anasema hali hiyo inazidi kuongezeka kwa sasa kwa kuwa watu wengi wanatumia muda mwingi mtandaoni.

Nimeamua kuwatumia Makeke na Nunu ambao ni wahusika wa kusadikika katika makala ili kuweza kuwakumbusha vijana wenzangu kuwa na kiasi katika matumizi makubwa ya mitandao ambayo ni hatarishi katika shughuli zetu za kikazi, kijamii na kiafya.

Filters zinatumiwa na baadhi ya wanawake na wanaume zinazidi kuwa maarufu hapa Tanzania. Jambo ambalo wengi hatufahamu ni kwamba huenda zikaharibu mahusiano yetu, kutukosesha kazi ama kutuletea sonona katika maisha yetu.

Sitaki kusema kuwa watu wasitumie kabisa filters, la hasha! Bali wafanye kwa kiwango na waache kuaminisha watu kuwa mwonekano unaonekana kwenye picha na video zilizotengenezwa na teknolojia hizo ndiyo wao. 

Filters zenye masikio ya mbwa au mkia wa Simba huenda zisionekane tatizo kwa kuwa mtu anaweza kusema ni utani japo kuna wengine wanaweza kutumia mwanya huo kufanya unyanyasaji mtandaoni.

Uamuzi ni wako.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW