Changamoto ya intaneti inavyowakwamisha wajasiriamali Tanzania

May 14, 2024 5:11 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutokana na kupungua kwa idadi ya wateja wanaopatikana majukwaa ya mtandaoni kupitia intaneti.
  • Huenda ikachukua muda kidogo kutatua changamoto hiyo.
  • Wajasiriamali washauriwa kujielimisha na mbinu za kukabiliana na changamoto za intaneti.

Mbeya. “Siku za nyuma nilikuwa nikiweka ‘status’ napata ‘views’ (watazamaji) 300 hadi 400 lakini tangu juzi napata ‘views’ 40 hadi 60 Kwa kweli hali imekuwa ngumu si kawaida keki nilizotengeneza kubaki,”.

Ni Zamda Mafimbi, mjasiriamali anayejihusisha na utengenezaji wa keki jijini Mbeya, akielezea kwa uchungu namna changamoto ya ukosefu wa intaneti ilivyoharibu biashara yake ambayo kwa kiasi kikubwa hutegemea mtandao.

Mafimbi, ambaye hutangaza keki zake kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram, WhatsApp, na Facebook ameiambia Nukta Habari kuwa katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita amekuwa akishindwa kupakia picha za bidhaa zake huku wakati mwingine akilazimika kusubiri zaidi ya masaa mawili ili kuchapisha picha moja.

Mjasiriamali huyo ameongeza kuwa changamoto ya intaneti imesababisha kupungua kwa idadi ya watu wanaotizama bidhaa zake kupitia kurasa za mitandao ya kijamii jambo lililoathiri  biashara yake ambayo ndio anaitegemea kuendesha maisha.


Soma zaidi:Punda wanavyorahisisha maisha ya wakazi Iziwa, Mbeya


Hitilafu ya mkongo wa baharini ndio chanzo

Wakati Zamda pamoja na wafanyabiashara kama yeye wanaotegemea mtandao kwa kiasi kikubwa ili kuendesha shughuli zao wakionja shubiri ya kukosekana kwa huduma hiyo, huenda upatikanaji wake ukachukua muda mrefu zaidi mara baada ya kubainika kuwa chanzo cha tatizo hilo ni hitilafu kwenye mkongo wa mawasiliano wa baharini.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA leo Mei 13, 2024 imebainisha kuwa taarifa za awali zimeonesha chanzo cha tatizo ni hitilafu katika mkongo wa mawasiliano wa baharini wa Kampuni za SEACOM ba EASY kati ya Afrika Kusini na Msumbiji.

Licha ya kuwa taarifa hiyo imebainisha kuwa tayari hatua za dharula zimechukuliwa na watoa huduma ili kuhakikisha upatikanaji wa intaneti kwa njia ya mbadala unafanyika, bado kumekuwepo na malalamiko kwa baadhi ya watumiaji kutopata huduma hiyo kwa uhakika.

Kwa mujibu wa TCRA changamoto ya intaneti imekuwepo nchini kuanzia jana Mei 12, 2024 saa tano asubuhi.

Maisha yapoje nje ya mtandao?

Tofauti na maumivu anayopitia Zamda, baadhi ya wafanyabishara ambao shughuli zao hazihusiani na mtandao wao wameendelea kutamba.

Anastazia Mwamlima, mfanyabiashara wa mahitaji ya nyumbani eneo la Ilolo jijini Mbeya amewashauri wajasiriamali wenzie kutotegemea mitandao ya kijamii peke yake ili kuendesha shughuli zao jambo litakalowasaidia kipindi zitokeapo dharula za ghafla.

Kwa upande wake Imani Luvanga, Mwandishi wa Habari na mtetezi wa haki za kidigiti ameiambia Nukta habari kuwa changamoto hiyo inawapata watumiaji wa mtandao kutokana na mazoea na kutokujiandaa kukabiliana na hali kama hiyo inapokuwa imejitokeza.

“Ni vyema wajasiriamali wa mtandaoni wakawa na uelewa mpana wa masuala ya inateti ili  hata kama wanakumbana na changamoto hiyo, wanakuwa wafahamu namna ya kukabiliana nayo bila shughuli zao kuathiriwa,” amesema Luvanga.

Makala hii imeandikwa na Samuel Ndoni, mwandishi wa habari aliyepo jijini Mbeya anapatikana kwa nambari za simu 0677202000 au barua pepe samuelndoni@gmail.com

Enable Notifications OK No thanks