Vijana na mustakabali wa miundombinu ya kidijitali ya umma Tanzania
- Washiriki kubuni huduma za mtandaoni kutatua changamoto za wananchi.
- Waeleza kinachowazuia kushiriki ujenzi wa miundombinu ya kidijitali ya umma (DPI).
- Serikali, wadau watoa mwelekeo waweka mikakati kuwaweza vijana.
Rachel Emanuel anakumbuka siku ambayo ilibadilisha kila kitu katika maisha yake. Rachel alikuwa akikabiliwa na mgogoro wa ardhi kwa muda mrefu.
Rachel (33), kila alipojaribu kutafuta msaada, alijikuta katika mlolongo mrefu na kutumia pesa nyingi kuwalipa mawakili, jambo ambalo hakulimudu.
Siku moja akiwa nyumbani kwake Bagamoyo mkoani Pwani akiperuzi vitu mtandaoni katika simu yake alikutana na moja ya taarifa kuhusu programu tumishi ya Sheria Kiganjani.
Rachel, mara moja alipakua programu hiyo. Ndani ya dakika chache akaongea na wakili kuhusu jambo lake.
“Sikuamini,” anasema Rachel, mama wa mtoto mmoja. “Kwa mara ya kwanza nilisikia sheria iko upande wangu. Ilikuwa rahisi, inaeleweka na haikunigharimu pesa yoyote kupata mwongozo wa kisheria kushughulikia mgogoro wa ardhi wa kiwanja changu.”
Rachel ni miongoni mwa Watanzania wengi ambao wameanza kuona mabadiliko ya teknolojia yanayochagizwa na vijana wabunifu. Mabadiliko hayo ni zana za kidijitali ambazo zinachangia katika ujenzi wa miundombinu ya kidijitali ya umma (DPI).
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), DPI ni mkusanyiko wa mifumo ya kidijitali inayofanya kazi pamoja, ambayo inaunda msingi imara wa kutoa huduma za umma na binafsi kwa katika ngazi ya jamii.
DPI inawezesha upatikanaji wa huduma kama vitambulisho vya kidijitali, malipo ya kielektroniki, na kubadilishana taarifa kwa uwazi, ubunifu na ufanisi ambao taasisi za umma na binafsi zinarahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Sheria Kiganjani ilitengenezwa na vijana wa Tanzania kwa lengo kuu moja; kuzifanya huduma za kisheria kupatikana kwa kila mtu na sehemu yoyote.
Programu hiyo iliyoanzisha mwaka 2018 inatoa mwongozo wa sheria, fursa za ushauri, na elimu ya haki za msingi kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.
“Watanzania wengi wanakosa haki zao za msingi na huduma za kisheria,” anasema mwanzilishi mwenza wa Sheria Kiganjani, Musa Kisena ambapo wameweza kuwafikia watu zaidi ya milioni 3.5. Kupitia programu hiyo.

Sheria Kiganjani inawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ili kuwapatia msaada wa kisheria kwa njia ya simu za mkononi. Picha | Sheria Kiganjani.
Haki sio eneo pekee ambalo vijana wanaboresha maisha ya Watanzania kwa kutumia ubunifu wa teknolojia unaojengwa juu ya DPI.
Jukwaa lingine linaloundwa na vijana ni M-Kadi. Jukwaa hili mebadilisha namna Watanzania wanavyofurahia maisha. Sherehe za harusi, kuzaliwa, matamasha na hafla ambazo zamani zilitegemea kadi za karatasi zisizodumu, sasa hufanyika kwa kutumia mialiko ya kidijitali.
M-Kadi inawawezesha watumiaji kubuni, kutuma na kufuatilia mialiko, na hata kukusanya michango kwa njia ya kidijitali, jambo linaloongeza ujumuishi wa kifedha wa makundi mbalimbali kwenye jamii wakiwemo vijana na wanawake.
“Tuligundua kuwa kulikuwa na shida ya kusambaza kadi za karatasi na watu walitumia pesa nyingi kuchapisha kadi ambazo hubaki kama uchafu,” anasema mwanzilishi wa jukwaa hilo, Maarufu Muyaga.
Jukwaa hilo limekuwa njia mojawapo ya kupunguza matumizi ya karatasi ili kuokoa mazingira yanayoharibiwa kwa ukataji wa miti.
Hali halisi ya DPI Tanzania
Serikali kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, inachagiza upatikanaji wa intaneti ya uhakika na yenye ubora na kutanua wigo wa huduma mtandao ili kutengeneza mazingira rafiki kwa vijana wabunifu kushiriki kikamilifu katika ujenzi na ukuzaji wa DPI.
Hii inatokana na ongezeko la watumiaji wa intaneti. Kwa mujibu wa Takwimu za Mawasiliano za September 2025 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), idadi ya watumiaji wa intaneti imeongezeka kutoka milioni 41.4 katika robo ya mwaka iliyoishia September 2024 hadi milioni 99.3 kwa robo ya mwaka inayoishia Septemba 2025.
Licha ya ongezeko hilo, bado Watanzania hawajafikiwa kikamilifu na DPI kuwawezesha kupata huduma mbalimbali kwa njia rahisi na ya haraka.

Ripoti ya Ukomavu wa Teknolojia ya Utawala (GovTech Maturity Index) ya mwaka 2022 iliyotolewa na Benki ya Dunia, inaeleza kuwa Watanzania saba kati ya 10 wanahitaji huduma za msingi za Serikali kama Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) lakini upatikanaji wake ni changamoto hasa maeneo ya vijijini.
Pia ushirikishwaji wa viijana ambao ni zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wote katika ujenzi wa DPI bado siyo wa kuridhisha, jambo linalowapunguza kasi yao katika kuvumbua na kubuni teknolojia rahisi kutatua changamoto za Watanzania hasa kijamii na kifedha.
Bado vijana wabunifu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowakwamisha kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa DPI nchini ikiwemo matukio ya kupungua kwa kasi na kuzimwa kwa intaneti kama ilivyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na 2020. Hii imekuwa ikiathiri utoaji wa huduma mtandaoni na kuathiri kipato cha vijana.
Mtaalam wa ulinzi wa kidijitali na intaneti, Alembe Joseph anasema Tanzania imepiga hatua katika eneo la DPI ukilinganisha na nchini nyingine za Africa lakini udhibiti wa baadhi ya majukwaa ya mtandaoni kunapunguza kasi ya vijana kupata taarifa na kubadilishana uzoefu wa kuendeleza huduma na bidhaa wanazobuni.
“Tumeona vizuizi katika matumizi ya mitandao kwa mfano X. TikTok na Instagram Live, hiyo ni sehemu moja ya changamoto ambayo inapelekea utekelezaji wa DPI ionekane inasuasua kwa sababu watu au wanafikiria kwamba ni censorship (udhibiti),“ anasema Joseph ambaye ni Katibu wa Jukwaa la Vijana la Utawala wa Mtandao Tanzania (Youth IGF Tanzania).
Anasema hatua hizo zimekuwa zikisababisha malalamiko kutoka kwa vijana, hasara na kuwakosesha uhuru wa kupata na kuchangia katika utekelezaji wa sera na sheria za Tehama.
Sera ya Taifa ya Tehama ya mwaka 2016, inaiagiza Serikali na wadau wa teknolojia kuweka majukwaa ya ushirikishwaji katika kukuza teknolojia ili kuwarahishia wananchi upatikanaji wa huduma za kijamii na kuchagiza maendeleo ya Taifa.

Ushiriki wa vijana katika ujenzi wa miundombinu ya kidijitali ya umma (DPI) unawawezesha kutoa mchango wao wa ubunifu katika kukuza uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya Watanzania. Picha | Teen In AI Tanzania.
Nini kifanyike kuongeza ushiriki wa vijana?
Joseph anapendekeza uanzishwaji wa masanduku ya ubunifu (innovation sandbox) ambayo kijana watatoa mawazo ya kibunifu ambayo yanatoa suluhu kwa maisha ya Watanzania kupitia DPI zilizopo.
Mtaalam huyo anasema Serikali iendelee kutoa unafuu wa kodi kwa kampuni changa za vijana, kuweka mazingira rafiki ya kuanzisha biashara na kuwapa fursa zaidi ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kupitia majukwaa mbalimbali.
“Vijana waweze kutafuta fursa zingine zilizopo ili kuweza kujielimisha zaidi na zaidi kwa sababu elimu ndio kitu cha msingi ili kuelewa sera na kanuni katika sekta ya teknolojia,” anasema Joseph.
DJ Sma anashauri sheria zinazosimamia teknolojia zijumuishwe pamoja ili kuondoa mkanganyiko wa vijana ambao wanaanzisha kampuni huku Serikali ikiangalia namna ya kuwawezesha kifedha kupata teknolojia rahisi zitakazoimarisha shughuli zao.
“Serikali iwe muwezeshaji, iwaachie watu wafanye ugunduzi. Wakae na wabunifu wajue wanahitaji nini na wawe wepesi kubadilika hasa katika kipindi hiki ambacho akili unde (AI) inaanza ili tusiachwe nyuma,” anasema DJ Sma.

Majukwaa yanayowaleta pamoja vijana katika sekta ya teknolojia ni njia mojawapo ya kubadilishana uzoefu na mawazo yatakayosaidia kubuni bidhaa na huduma zinazoendana na mahitaji ya wananchi na DPI. Picha | Kontenti.
Hatua inazochukua Serikali
Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Mifumo na Huduma za Uzingatiaji wa Sheria, Miongozo na Viwango ya Tehama wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohamed Mashaka anasema Serikali imeanza mchakato wa uandaaji wa Sera ya Taifa ya Kampuni Changa ambayo itaweka msingi wa vijana kushiriki katika ujenzi wa DPI.
‘Lengo ni kuunda mazingira wezeshi, yanayotabirika na yenye msaada kwa ukuaji wa makampuni chipukizi nchini. Sera hii itaanzisha motisha mbalimbali za kuchochea ubunifu na ujasiriamali,” anasema Mashaka.
Pia Serikali inaendelea na jitihada za kuanzisha vituo vya ubunifu (Innovation Hubs) hadi ngazi ya wilaya kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Vituo hivi vitawekewa maabara za kidijitali, maeneo ya mafunzo, na vifaa vya utafiti ili kuvutia vijana wengi wenye ubunifu kuendeleza bunifu zao kwa kutumia teknolojia rahisi ya kidijitali.
“Tutaanzisha Jamii Sandbox (Masanduku ya ubunifu) kama jukwaa maalumu ambapo wabunifu wanaweza kuunda, kujaribu, na kuboresha mawazo yao kabla ya kuyapeleka sokoni,” anasema mtaalam huyo.
Sandbox hiyo itafanya kazi kama daraja muhimu kati ya ubunifu na uanzishaji biashara, na kupunguza hasara na gharama zinazohusiana na kuleta bidhaa na suluhisho jipya sokoni.
Ikiwa mikakati hii ya Serikali na wadau itatekelezwa kikamilifu, itakua fursa muhimu kwa vijana kutumia ujuzi, maarifa na ubunifu kujenga miundombinu imara ya kidijitali ya umma ambayo sio tu itaboresha maisha ya Watanzania bali kukuza uchumi wa nchi.
Latest