Jinsi matapeli wanavyopora mamilioni ya Watanzania mtandaoni
- Uchunguzi wetu wabaini baadhi wamebadili majina ya akaunti zao za mitandao ya kijamii hadi zaidi ya mara 10.
- Huwalazimisha wanunuzi kutuma haraka haraka kiasi chote au nusu ya thamani ya mzigo.
- Hupenda kutumia zaidi WhatsApp na namba zao za kawaida huwa hazipatikani.
- Uchunguzi wawanasa Filber_stores, jumba la pochi na wengineo.
Dar es Salaam, Arusha, Mwanza. Kila siku baadhi ya Watanzania hutuma fedha kwenda kwa wafanyabiashara wanaotangaza biashara kwenye mitandao ya kijamii kwa matumaini ya kuletewa bidhaa walizochagua.
Hata hivyo, baadhi ya wauzaji hao ambao huweka picha zenye mvuto, punguzo kubwa la bei na wenye maelfu ya wafuasi, hupotea bila kuwasilisha hata bidhaa moja.
Nyuma ya miamala hiyo kuna uchumi wa utapeli mtandaoni unaotumia ongezeko la uaminifu kwenye biashara mtandao kuhadaa watu na kunyonya kimyakimya mamilioni ya Shilingi kutoka kwa wanunuzi wa mtandaoni.
Neema Eward anasema akiwa na lengo la kujitafutia kipato cha ziada alishawishika na picha pamoja na video alizoziona katika ukurasa wa Instagram wa mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Filber_Stores, uliodai kuuza bidhaa za kike ikiwemo pochi na viatu.
Uwepo wa bidhaa hizo katika ukurasa huo uliokuwa na wafuasi zaidi ya 19,000 ulimfanya mwanafunzi huyo wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) mkoani Mwanza, kuamini kinaochouzwa na kuona fursa ya biashara ya kuuza bidhaa.
Kwa mikoba ambayo wafanyabiashara wengine huuza kwa Sh45,000 hadi Sh50,000, mfanyabiashara huyo alikuwa akiuza kwa Sh15,000, hadi Sh20,000 ikiwa ni punguzo la takribani mara mbili hadi tatu ya bei ya soko.
Neema anasema alijichanga na kuwasiliana na mfanyabiashara huyo Julai Mosi, 2025 katika mtandao wa WhatsApp kupitia namba 0617 667 687 na baada ya makubaliano ya awali alimtumia Sh350,000 kwa ajili ya malipo ya jozi (pair) 15 za viatu vya kike akiahidiwa kutumiwa mzigo siku iliyofuata.
Baada ya kumtumia pesa kupitia Lipa Namba ya M-Pesa ya mfanyabiashara huyo (67082642) zilipita saa, siku, wiki na miezi bila kupokea bidhaa hizo licha ya Neema kuahidiwa kuwa angefikishiwa mzigo wake stendi kuu ya mabasi Mwanza kutoka Kurasini, jijini Dar es Salaam ilipo stoo ya mfanyabiashara huyo.
“Nilisubiri sana mzigo akawa tu ananiambia atanitumia na baadaye akaniblock (Alizuia nisiwasiliane naye) kabisa hata nikimtafuta kwenye namba nyingine akijua ni mimi anakata simu kisha ananiblock,” anaeleza Neema na kubainisha kuwa utapeli huo umemrudisha nyuma kibiashara.
Neema ni miongoni mwa mamia ya Watanzania, wengi wao wakiwa ni wanawake na vijana wanaoishi mijini, wanaopoteza mamilioni ya fedha kutokana na utapeli unaofanywa na watu wanaowaaminisha wanunuzi kuwa ni wafanyabiashara halali wa mitandaoni.
Ongezeko la utapeli limepita pia na fursa ya kuongezeka kwa matumizi ya mitandao ya kijamii kuuza au kununua bidhaa kutokana na kuongezeka kwa simu janja na upatikanaji wa intaneti.
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) watumiaji wa intaneti nchini wameongeza mara mbili ndani ya miaka mitano kutoka milioni 28 Septemba 2020 hadi milioni 56.3 kufikia Septemba 2025.
Matumizi ya simu janja nayo yamepaa nchini hadi milioni 27 Septemba, 2025 kutoka simu janja milioni 22 Septemba 2024, jambo linalotoa fursa zaidi za kukuza uchumi wa kidijitali ikiwemo uuzaji na ununuzi wa bidhaa mtandaoni.
Ongezeko la ukuaji wa inteneti unawarahisishia wafanyabiashara kupata masoko ya huduma na bidhaa wanazouza kwa njia rahisi na haraka huku wengine wakitumia fursa hiyo kutapeli watu.
Uchunguzi uliofanywa na Nukta Habari kwa zaidi ya miezi minne kuanzia Agosti hadi Desemba, 2025 katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza, umebaini kuwa baadhi ya matapeli wanatumia ongezeko la imani ya wanunuzi kwenye biashara za mitandaoni kuwaibia fedha zao.
Ili kubaini mbinu zinazotumika kutapeli, tulichunguza akaunti nane za watu wanaouza bidhaa kupitia mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na Tiktok ambazo hutumiwa zaidi na baadhi ya matapeli.
Tuliagiza bidhaa 12 kutoka katika akaunti hizo nane huku baadhi tukiagiza bidhaa zaidi ya moja kutokea mikoa tofauti ili kubaini iwapo kulikuwa na utofauti wa uhakika wa kupata bidhaa kwa walio karibu na mfanyabiashara husika na wale walio nje ya mkoa.

Baadhi ya miamala iliyotumwa kwa mfanyabiashara filber store kwa lengo la kujipatia bidhaa lakini badala yake akafanya utapeli
Kati ya wafanyabiashara nane tuliowachunguza kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii ni wafanyabishara watatu pekee waliofikisha bidhaa husika kwa uaminifu huku wafanyabiashara watano wakitutapeli bidhaa tisa na kukata kabisa mawasiliano.
Kurasa hizo zilizofanya utapeli ni pamoja na Jumba la pochi Tanzania, freedelivery 89, filber_stores, na home store store (HOME_KITCHEN_DAR) ambao hutumia mbinu mbalimbali kutapeli watu.
Hata hivyo, baadhi ya majina haya yanabadilishwa mara kwa mara ili kuhadaa wateja wapya.
Jinsi utapeli unavyofanyika
Ili kutapeli, watu hao hutumia mbinu mbalimbali zinazowavuta wanunuaji polepole mwisho kujikuta wametapeliwa ikiwemo kutumia picha na video zenye ubora wa hali ya juu kuvutia wateja, punguzo kubwa la bei kulinganisha na wauzaji wengine pamoja na kutumia majina yanayofanana na akaunti za biashara zinazoaminika.
Mathalani, katika ukurasa wa mfanyabiashara freedelivery89 ameweka samani nzuri za kuvutia kwa bei ndogo huku akionyesha video mbalimbali zinazoonesha akiwapelekea wateja bidhaa zao jambo ambalo linajenga uaminifu kwa wateja.
Baada ya mteja kuvutiwa na bidhaa hutakiwa kutuma pesa ya mzigo angalau nusu bei pamoja na gharama ya usafiri ndipo mzigo wake unaweza kusafirishwa kutoka kwake hadi alipo mnunuaji, huku wengine wakitoa ofa ya usafiri wa bure kwa wakazi wa Dar es Salaam.
Katika mawasiliano na matapeli hao wanakutajia maeneo wanayopatikana, namba za malipo zenye majina yatakayojitokeza wakati wa malipo huku wakikuhakikishia mzigo kufika ndani ya saa moja, au saa tatu kwa wale waliopo maeneo ya karibu.
Ukituma pesa tu, na kuhakikisha kuwa fedha imepokelewa, wafanyabiashara hao hutokomea. Ukijaribu kupiga simu ya mfanyabiashara uliyekuwa unawasiliana nae haipokelewi tena, muda mchache baadae haipatikani, ukijaribu kumtumia ujumbe mfupi katika mitandao ya kijamii uliyokuwa ukiwasiliana nae mwanzo huko nako hajibu au anakuzuia (block).
Wakifanikiwa kutapeli watu kadhaa, wafanyabishara hao hubadili majina ya akaunti zao au kuiga majina ya biashara halali mashuhuri mtandaoni ili kuendeleza mnyororo huo wa utapeli.
Kwa mfano, awali home_store_store alikuwa akijiita home essential store, kisha akabadili na kujiita HOME_KITCHEN_DAR na baadae akabadili na kujiita home _storetz lengo likiwa ni kuwapoteza watu walio watapeli kutokuwafahamu.

Tunachokifahamu kwa waliotutapeli
Miongoni mwa akaunti zinazotuhumiwa zaidi kutapeli watu mtandaoni ni filber_stores iliyopo Instagram inayouza viatu na mikoba. Uchunguzi wetu umebaini akaunti hii ina namba ya utambulisho wa kipekee wa (Instagram User ID) 28146547923 inayosaidia kuitofautisha na akaunti nyingine zenye majina yanayofanana katika mtandao huo hata kama watabadili majina.
Ili kuthibitisha madai ya utapeli ya baadhi ya watu mtandaoni na wale waliotujulisha akiwemo Neema, Novemba 22, 2025 mwandishi wetu aliyepo Dar es Salaam alinunua viatu na mkoba kutoka katika akaunti hiyo na kutakiwa kulipia Sh55,000 siku hiyo hiyo kupitia Lipa Namba ya M-Pesa yenye namba 67082642 na jina la Filbers Sales.
Baada ya kulipia alijulishwa na mhudumu mwenye sauti ya kiume kwa kutumia namba +255 617 667 687 yenye jina la Leila Shaha Simbaliana kuwa mzigo ungefika Manzese baada ya saa 3 siku hiyo hiyo. Lakini hadi Desemba 31, 2025 hakuna mzigo uliomfikia.
Hata baada ya malipo hakupokea tena simu na hata alipopigiwa kupitia namba nyingine kufuatilia alieleza kuwa kuna watu wengi ofisini kwao na kwamba angefuatilia.
Mwandishi wetu mwingine kutoka Arusha aliagiza pochi yenye thamani ya Sh25,000 na kulipia usafiri wa Sh5,000 kwa akaunti hiyo hiyo ya filber_stores na kuhudumiwa na sauti ya mtu yule yule aliyedai wapo wengi. Naye baada ya malipo hakupokea tena simu wala kujibu meseji.
Awali mtu huyo alimweleza mwandishi wetu kwa ujumbe mfupi kuwa hawana duka bali wanatoa mzigo moja kwa moja kwenye ghala lao la mizigo lililopo Bandari ya Dar es Salaam. Ndani ya miezi mitatu wameshabadili eneo lilipo ghala kwenye akaunti yao mara mbili ikiwemo Makumbusho na Kurasini.
Mizigo inapochelewa, baadhi ya wateja hutaka kurejeshewa fedha bila mafanikio.
“Nililipia mzigo baada ya hapo akawa kimya, nikawa namtumia ujumbe hajibu. Baadaye nikamwambia nirudishie pesa yangu kama hakuna mzigo wangu akawa ‘anablue tiki’ tu (ujumbe umefika WhatsApp, unaonyesha umesomwa lakini haujibiwi) meseji zangu,”anaeleza Gladys Mataka, mkazi wa Jiji la Arusha ambaye ni miongoni mwa waliotapeliwa na filber-stores Novemba 16, 2025.
Mwandishi wetu mwingine alipomtafuta mtu anayehudumia biashara ya filber_stores kujibu tuhuma za utapeli, alikiri kupokea madai hayo akibainisha kuwa wameanza kuyafanyia kazi, akisisitiza tufike ofisini kwao Kurasini jijini Dar es Salaam katika ghala namba tano kwa ajili ya maelezo zaidi.
“Nishawahi kusikia na nikahandle (Nikashughulikia), kwa wenye changamoto (za kutapeliwa) nikatatua…Tafuta muda uje godown (ghalani) Januari 3,2026 watakusikiliza na kutatua,” alisema mtu huyo aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Filber na kudai yeye ndiye mmiliki wa biashara husika wakati wa mahojiano kwa njia ya simu.
Hata baada ya mwandishi wetu kufika eneo la geti namba tano la Bandari ya Dar es Salaam, alilotuelekeza kupitia ujumbe mfupi wa WhatsApp, hakukuwa na ofisi yoyote zaidi ya vibanda vya mamantilie. Majirani, walinzi na wafanyabiashara wengine hawalifahamu duka au ghala hilo na wala hawajawahi kumsikia mfanyabiashara huyo.
“Kwanza hapa sijawahi kuona mfanyabiashara mdogo akiwa na ofisi yake hapa na tokea nimekaa hapa sijawahi kusikia hata hilo jina (filber-stores) hakuna,” anaeleza mmoja wa walinzi wa ghala lililopo Kurasini jijini Dar es Salaam inapodaiwa kuwepo ofisi ya Filber-stores, aliyehudumia eneo hilo kwa miaka sita sasa.
Imeandikwa na Fatuma Hussein, Daudi Mbapani, Esau Ng’umbi (Dar es Salaam), Lucy Samson (Arusha), na Mariam John (Mwanza).
Itaendelea kesho
Latest