Upandaji miti: Kuiokoa Magu na tishio la jangwa
- Ni baada ya sehemu kubwa ya miti ya wilaya hiyo kutoweka.
- Yaathiri shughuli za kilimo na biashara.
- Kampeni ya upandaji miti yaimarishwa wilayani humo.
Mwanza. Licha ya mvua za masika kuanza kunyesha katika mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka, wananchi wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza wanaweza wasipate ahueni katika shughuli zao kutokana na wilaya hiyo kuathiriwa na ukame.
Msimu wa mvua za masika ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).
Maeneo mengine yanayopata aina hizo za mvua ni ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Wakazi wa Wilaya hiyo, wanaeleza kuwamvua zinazoendelea kunyesha siyo za kuridhisha kukidhi mahitaji ya uzalishaji na biashara ya mazao ya kilimo kwa sababu sehemu kubwa ya miti imekatwa.
Hiyo ni sawa kusema sehemu kubwa ya wilaya hiyo inaelekea kuwa “jangwa”.
“Ni ukame, hali ni mbaya kuna wakati hata maji ya kunyweshea mifugo kwenye madimbwi na malambo yanakauka , kiujumla hali si shwari,” anasema Mageta Masalu, mkazi wa Kijiji cha Sagani wilayani humo.
Masalu anasema ukosefu wa mvua za kutosha unaombatana na hali mbaya ya hewa kila mwaka katika wilaya hiyo, kumewafanya wasifaidike kikamilifu na shughuli za kilimo.
“Hatupati mavuno ya kutosha na hata kama mvua zinapokuja, zinakuja mvua mbaya mafuriko au zilizoambatana na upepo mkali,” anasema.
Ukataji miti hovyo husababisha athari kwa mazingira ikiwemo kupungua kwa mvua na kuharibika kwa rotuba ya udongo. Picha| LEAF.
Changamoto ya ukosefu wa mvua za kutosha pia umetajwa kusababisha kukosekana kwa vyanzo vya mapato ambapo wakazi hao wanaeleza kuwa wanalazimika kutegemea misimu ya mvua pekee kwa ajili ya kupanda na si kilimo cha umwagiliaji.
Mwenyekiti wa kijiji cha Sagani, Joseph Sagara anasema misimu ya mvua inapoisha maji yaliyoko kwenye malambo na visima hukauka haraka kutokana na jua kali.
Anasema tatizo la ukame unaosababishwa na kutokuwepo kwa miti linaathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za uzalishaji mali wilayani humo.
“Tuna miaka mingi kila mwaka ni afadhali ya uliopita, maisha ni magumu hata maji ya kutumia nyumbani ni shida kiujumla hali ni mbaya,” anasema Sagara.
Mwongozo wa upandaji na utunzaji wa miti Tanzania uliotolewa na Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA) uliotolewa mwaka 2017, unaeleza kuwa misitu imefunika hekta zaidi ya milioni 48 ya ardhi ya Tanzania.
Eneo hilo la misitu ni zaidi ya jimbo moja la California nchini Marekani.
Lakini ukataji wa miti usiodhibitiwa kwa ajili ya mkaa na kuni zinazotumiwa nyumbani na viwandani unatishia uwepo wa misitu hiyo ambayo ina umuhimu katika kuendelea mifumo ya maisha ya wanyama na mimea, kupunguza mmomonyoko wa udongo na uzalishaji wa hewa ukaa na kutunza vyanzo vya maji.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Taifa ya Takwimu za Mazingira ya mwaka 2017 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kiwango cha ukataji miti kinakadiriwa kuwa ni hekta 372,000 kwa mwaka.
Tatizo juu ya tatizo
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji cha Sagani, Joseph Sagara, kutokana na tatizo la ukame katika wilaya hiyo, watu wamehamishia nguvu zao katika ukataji miti ya asili ili waweze kupata kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia na kuuza kujipatia kipato.
Amesema hali hiyo imechangia miti mingi ya asili kutoweka huku hakuna juhudi za kimakusudi za kunusuru hali hiyo.“Hali ni mbaya, jua la Magu ni kali linatofautiana na jua linalowaka maeneo mengine la huku linaunguza hasa, watu hatuna pesa, hatuna vyakula vya kutosha ndani na hatuzalishi kwa kiwango kizuri kijumla Magu ina rekodi mbaya,” anasema Sagara.
Soma zaidi:
- Teknolojia inavyotumika kuokoa mazingira
- Teknolojia ya kutengeneza matofali kwa taka za plastiki yaingia sokoni
- Taka za kielektroniki zinavyotafuna mazingira ya Tanzania
Ukataji miti pia katika wilaya hiyo ulichangiwa na kuwepo kwa mdudu aina ya mbung’o aliyekuwa akisababisha ugonjwa wa malale kwa binadamu na wanyama ambapo alikuwa akikaa kwenye miti, jambo lilisababisha watu kakata miti ili kumtokomeza.
“Kwa kuwa mdudu huyo mara nyingi alikuwa akikaa kwenye miti, watu walilazimika kukata miti ili wasiendelee kupata maradhi hayo lakini pia hata mifugo yao mingi ilikufa,” anasema Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TSF), Profesa Dos Santos Silayo.
Prof Silayo anasema pamoja na mdudu huyo kudhibitiwa, tayari miti mingi ilikuwa imeharibiwa vibaya na hakukuwa na juhudi za makusudi za kuinusuru.
“Magu ni wilaya mojawapo kwa Mkoa wa Mwanza ambayo miti yake imeharibiwa sana, hali inayosababisha wilaya hiyo kuwa miongoni mwa wilaya zinazonyemelewa na ukame, hivyo kama TFS tumemaua kuanzisha kampeni za upandaji miti ili kunusuru hali hiyo,” anasema Prof Silayo.
Hatua zinazochukuliwa kuinusuru wilaya hiyo
Ili kuiokoa wilaya hiyo na jangwa, Prof Silayo anasema wameanzisha kampeni ya upandaji miti ambayo itasambazwa kwenye taasisi mbalimbali za dini, shule na kaya ili isaidie kurudisha uoto wa asili.
Amesema wana imani endapo kila mwananchi ataweka kipaumbele cha kupanda miti angalau minne na kuitunza vizuri hadi kukua itasaidia kupunguza tatizo la ukame.
“Magu leo ni ukame kwa kuwa hakuna mti ambao unakomaa kwa kiwango kikubwa mingi inakatwa ovyo na kuchomwa, maeneo ya hifadhi za misitu yameharibiwa vibaya hivyo kama TFS tumeona ipo haja ya kuanzisha kitalu hapa ili kunusuru hali hiyo na kurudisha ikolojia,” anaeleza.
Naibu wazir wa Utalii, Mary Masanja akipokea moja ya mti uliooteshwa na mwananchi wilayani Magu kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya upandaji miti kitaifa yaliyofanyika wilayani Magu Machi 21, 2022. Picha|Mariam John.
Upandaji miti utasaidia kupata hewa safi, kuhifadhi vyanzo vya maji, kuhifadhi ardhi yenye rutuba na kuzuia mmomonyoko wa udongo katika wilaya hiyo ya Kanda ya Ziwa.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Magu, tangu uhamasishaji wa zoezi la upandaji miti kwa wananchi lianze mwaka huu, mkoa wa Mwanza umefanikiwa kupanda miche ya aina mbalimbali zaidi ya milioni 3.2.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Marry Masanja akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani hivi karibuni alitoa agizo kwa wananchi wanaoishi mikoa ya Kanda ya Ziwa kuhakikisha wanaendelea na kazi ya kupanda miti na kutunza mazingira kwa ustawi wa maisha ya kila mmoja.
Aliziagiza halmashauri zote nchini kwa kushirikiana na TFS kuanzisha vitalu vya kuoteshea miche itakayotolewa kwa wananchi kwa ajili kupanda ili kuhifadhi Mazingira.
“Kwa kuwa uhitaji wa miche si Magu pekee kuna haja ya kila halmashauri nchini kuanzisha bustani ndogo ndogo katika ngazi za kata na tarafa ili iwe rahisi kwa wananchi waishio vijijini kupata miche hiyo kirahisi na kwenda kuipanda,” alisema Masanja.
Latest