Mabadiliko ya tabianchi yalivyoathiri unyeshaji mvua za masika Tanzania
- Baadhi ya mikoa yapata mvua chache na vipindi virefu vya ukavu.
- TMA yasema hali hiyo ni mabadiliko ya muda mfupi ya mifumo ya hali ya hewa..
- Vimbunga katika bahari ya Hindi na mabadiliko ya joto vyachangia.
Dar es Salaam. Kufuatia kusuasua kwa unyeshaji wa mvua za masika katika baadhi ya mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka likiwemo jiji la Dar es Salaam, watalaam wa hali ya hewa wamesema hali hiyo imechangiwa na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo vimbunga na joto la bahari.
Msimu wa mvua za masika ni mahususi katika Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Pia mvua hizo hunyesha katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Mvua hizo hunyesha kati ya Machi na Mei.
Mapema mwaka huu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitabiri kuwa maeneo mengi ya mikoa hiyo yangepata mvua za kutosha yaani wstani hadi juu ya wastani, lakini kumetokea mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa ambayo imeathiri unyeshaji wa mvua hizo.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi amesema maeneo ambayo yamepata mvua chache na vipindi virefu vya ukavu hasa mwezi Machi ni mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Dk Kijazi amesema hali hiyo ya vipindi virefu vya ukavu imesababishwa na matukio ya vimbunga katika bahari ya Hindi eneo la Rasi ya Msumbiji kusini.
“Vile vile, yamejitokeza mabadiliko ya muda mfupi ya joto la bahari katika eneo la pwani ya Afrika Mashariki na eneo la mashariki mwa bahari ya Hindi.
“Mabadiliko hayo ya muda mfupi ya joto la bahari ambayo ni nadra kutokea kutokana na tabia ya bahari kutunza joto au baridi kwa muda mrefu yamesabishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dk Kijazi.
Soma zaidi:
- TMA yatahadharisha ujio mvua kubwa
- Watanzania washauriwa kutumia taarifa za hali ya hewa kwenye mipango ya maendeleo
- Ujio mfumo wa taifa wa hali ya hewa kuchochea ujenzi wa viwanda nchini
Mwenendo huo wa vimbunga na mabadiliko katika joto la bahari vimechangia Ukandamvua (ITCZ) kuendelea kusalia katika maeneo ya kusini mwa nchi ambapo kwa kawaida katika kipindi cha mwanzoni mwa mwezi Machi huanza kuelekea maeneo ya kaskazini mwa nchi.
Hali hiyo imesababisha kuvurugika kwa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kuathiri mwenendo wa unyeshaji wa mvua za Masika, 2022.
Ingawa maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani katika msimu huu wa mvua za masika 2022, TMA imesema matukio ya vipindi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza.
Mvua hizo kubwa zinaweza kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu ikiwemo barabara na madaraja, hivyo wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari.