Unayotakiwa kufahamu kuhusu “Boxing Day”
- Ni siku ya mapumziko ambayo watu hutumia kupeana zawadi.
- Wengine hutumia kukamilisha matakwa ya kidini na mapumziko ya Kitaifa.
- Ilianza kuadhimishwa karne ya 19 kwa matajiri kutoa zawadi kwa watu wasiojiweza.
Sikukuu ya Krismas imepita mpaka mwaka ujao tena. Hiyo haimanishi kuwa msimu wa mapumziko ya mwisho wa mwaka nao umemalizika.
Watu bado wanaendelea kusheherekea katika maeneo mbalimbali duniani. Leo pia watu wanasheherekea siku ya “Boxing Day” au siku ya kupeana zawadi ambayo inafanyika siku moja baada ya Krismasi.
Siku hiyo ambayo siyo siku ya kupigana kama jina lenyewe lilivyo, haisherekewi katika nchi zote, isipokuwa watu wengi huitumia kama siku ya mapumziko baada ya Krismasi.
Kwanini “Boxing Day”
Kwa mujibu wa mtandao wa Metro, siku hiyo ilianza kusheherekewa karne ya 19 ambapo matajiri walitumia kama siku ya kufunga zawadi kwenye maboksi na kuwapatia watu wenye uhitaji na wasiojiweza kwenye jamii.
Pia ilikuwa ni siku iliyozoeleka kwa wafanyakazi hasa wa bustani na nyumbani kupokea zawadi kutoka kwa mabosi zao na kuitumia siku hiyo kupumzika na familia zao bila kufanya kazi.
Mtandao huo unaeleza kuwa makanisa nayo yalikuwa na sehemu katika siku hiyo. Yalikuwa yanakusanya fedha kutoka kwa waumini kwa mwaka mzima na kuwapa watu wenye uhitaji hasa waliopo ndani ya kanisa.
Siku hiyo ambayo siyo siku ya kupigana kama jina lenyewe lilivyo, haisherekewi katika nchi zote, isipokuwa watu wengi huitumia kama siku ya mapumziko baada ya Krismasi. Picha|Mtandao.
Nchi zinazosheherekea “Boxing Day”
Inaelezwa kuwa sikukuu ya zawadi ilianza kusheherekewa nchini Uingereza tangu mwaka 1871 na inaendelea kusheherekewa mpaka leo kama sikukuu ya kitaifa.
Watu huingia madukani kununua zawadi ambazo hupata punguzo la bei ili kuwapa ndugu, jamaa na marafiki. Hali hiyo inatafsiriwa kuwa ni ishara ya kuimarisha mahusiano na kuendeleza undugu kwenye jamii.
Kwa Waingereza, kama siku hiyo imeangukia jumamosi basi husogezwa hadi jumatatu inayofuata; na kama imeangukia jumapili husogezwa hadi jumanne. Nchi nyingine zinazosheherekea siku hiyo ni pamoja na Australia, New Zealand, Canada, Nigeria, Trinidad na Tobago.
Zingine ni Singapore, Afrika Kusini, Bermuda na jimbo la Hong Kong lilipo China. Nchi hizi zinasheherekea kwa sababu zilikuwa makoloni ya Uingereza.
Kwa nchi hizo, siku hiyo hujulikana zaidi kama siku ya kufanya manunuzi ya zawadi kwenye maduka kama ilivyo kwa “Black Friday”.
Black Friday ni muda maalumu ambapo maduka hufunguliwa wakati wa jioni na bidhaa huuzwa kwa bei ya chini mno kuliko mteja anavyotarajia. Wamarekani na wamekuwa wakiitumia siku hii kununua bidhaa ambazo zinaashiria kuanza kwa maandalizi ya zawadi za Krismas na kufunga mwaka.
Zinazohusiana:
- Mambo ya kufanya wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka
- Zingatia haya unapofanya manunuzi siku ya “Black Friday”
- Zingatia haya wakati ukifanya manunuzi msimu wa sikukuu
Katika nchi nyingine ni siku ya mapumziko, watu hawafanyi kazi lakini kwao ina umuhimu mkubwa katika shughuli za kidini (religious significance) hasa nchini Romania, Hungary, Germany, Poland, Netherlands, Jamhuri ya Czech na Scandinavia.
Pia inasheherekewa kama siku ya Mtakatifu Stefano kati nchi ya Ireland na mkoa wa Catalan, Uispania ambapo watu hutulia majumbani wakitafakari mateso aliyoyapa Stefano siku za uhai wake.
Moja ya mavazi yanayovaliwa huko Ireland wakati wa sherehe za kumkumbuka Mtakatifu Stefano ambayo pia ni siku ya Boxing Day. Picha|Mtandao.
Kwako, siku hii ina maana gani? Unaitumiaje wewe na familia yako?
Latest
