Ijue historia ya sikukuu ya mwaka mpya

December 31, 2024 9:00 am · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Sherehe za mwaka mpya hapo zamani hazikufanyika Januari 1 kama ilivyozoeleka hii leo.
  • Sherehe za mwaka mpya za kisasa zilianza kufanyika katika karne ya 19 na 20. 

Dar es Salaam. Kila inapofika mwezi Disemba kila mwaka, ulimwenguni kote ni msimu wa sikukuu. 

Watu hufanya matukio mbalimbali ikiwemo sherehe za kufunga mwaka na kuukaribisha mwaka mpya. 

Katika kipindi hiki, familia ambazo huwa zimetengana kwa muda, huungana tena na kusherehekea pamoja. Watu hupeana zawadi kudhihirisha upendo na furaha walizonazo kwa wapendwa wao. 

Sherehe za mwaka mpya zimekuwa alama muhimu ya utamaduni wa binadamu kwa miaka mingi, zikibadilika kulingana na jamii katika kuonyesha imani, matumaini, na matarajio katika kuanza mwanzo mpya. 

Kuanzia mila za kale hadi sasa, jinsi tunavyokaribisha mwaka mpya ni safari ya kuvutia kupitia historia. Wakati ukijiandaa kuupokea mwaka mpya wa 2025, nakurudisha nyuma kufahamu historia na kwa nini unasherehekea sikukuu ya mwaka mpya. 

Mwanzo wa sherehe huko Mesopotamia

Sherehe za mwaka mpya zilianzia huko Mesopotamia ya kale mnamo mwaka 2000 Kabla ya Kristo (KK) . Sherehe za mwaka mpya katika Mesopotamia ya kale hazikufanyika Januari kama ilivyozoeleka hii leo, bali zilifanyika mwezi Machi katika siku ambayo urefu kati ya mchana na usiku huwa sawa (spring equinox).

Sherehe hizi zilikuwa zikifanyika kwa siku 12 zikiashiria kuzaliwa upya na zilijulikana kama Akitu. Sherehe za Akitu zilifanyika kwa kuambatana na matambiko mbalimbali ili kumtukuza Marduk, mungu mkuu wa Babeli, aliyeaminika kudumisha ustawi wa jamii za watu wa Mesopotamia ya kale.

Sherehe za mwaka mpya katika Mesopotamia ya kale zilifanyika kwa kuambatana na matambiko mbalimbali ili kumtukuza Marduk, mungu mkuu wa Babeli. Picha|Altargods.com

Kalenda ya Kirumi na Januari 1

Kadri jamii zilivyoendelea kukua, ndivyo kalenda zilivyoendelea kubadilika. Jamhuri ya Kirumi ilikuwa ikiadhimisha sherehe za mwaka mpya Machi 15. Baada ya marekebisho ya kalenda ya Kaisari Julius mnamo mwaka wa 46 KK, Januari 1 ikawa mwanzo rasmi wa mwaka.

Mabadiliko haya yalikusudia kumheshimu Janus, mungu wa Kirumi mwenye nyuso mbili, ambaye aliweza kuangalia mbele na nyuma kwa wakati mmoja. Warumi kusherehekea siku hiyo kwa kubadilishana zawadi, kupamba nyumba zao kwa matawi ya mzeituni, na kuandaa karamu za kifahari.(Kulingana na Encyclopedia Britannica)

Wakati wa enzi za kati, sherehe za mwaka mpya zilipoteza umaarufu huko barani Ulaya kutokana na mizizi yake ya kipagani. 

Kwa mujibu wa tovuti ya History Today, viongozi wa dini ya Kikristo wakajaribu kuibadilisha sikukuu hii kwa kuanzisha ibada za kidini. Kanisa likasisitiza kusherehekea kuzaliwa kwa Kristu (Krismasi) Desemba 25 na Siku ya Ujio wa Malaika Machi 25 kama siku bora za maadhimisho ya mwanzo mpya.

Mnamo mwaka 1582 kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Gregory XIII alianzisha kalenda ya Gregori, kalenda hii ilirekebisha mwelekeo wa kalenda ya Kaisari Julius na kuthibitisha tena Januari 1 kama siku ya mwaka mpya.

Nchi zilizokuwa zikifuata dini ya Kikatoliki zilipokea haraka marekebisho haya, lakini mikoa ya Kiprotestanti na Kanisa la Orthodox la Mashariki ilichukua karne nyingi kufuata mfano huo. Kwa mfano, Uingereza ilikubali kalenda ya Gregori mnamo mwaka wa 1752.

Kubadilishwa kwa kalenda ya Kaisari Julius hakujafanya kutoweka kwa tofauti za kimila na tamaduni katika kusherehekea mwaka mpya.

Papa Gregory XIII alianzisha kalenda ya Gregori, kalenda hii ilirekebisha mwelekeo wa kalenda ya Kaisari Julius na kuthibitisha tena Januari 1 kama siku ya mwaka mpya. Picha|Pointsincase.com

Mfano,  jamii za watu wa China husherehekea mwaka mpya kati ya Januari 21 na Februari 20. Watu hutumia muda huo kwa mapumziko na kukamilisha shughuli mbalimbali za kijamii.

Nchini India, wana sherehe ya mwaka mpya inayojulikana kama ‘Vishu’ ambayo hufanyika mwezi Aprili, kuashiria mzunguko mpya wa kilimo. 

Mwanzo wa mila za kisasa

Sherehe za mwaka mpya za kisasa zilianza kufanyika katika karne ya 19 na 20. Na Kulingana na gazeti la The New York Times, tukio maarufu la ‘Times Square Ball Drop’ la mwaka 1907 lilifanyika kama mbadala wa mwaka mpya kwa tamaduni za jamii ya watu wa China, ambao ulipigwa marufuku mjini New York. 

Duniani kote, maeneo mbalimbali Januari 1 hutumika kama siku ya mwaka mpya. Usiku wa kuamkia siku hiyo huambatana na shamrashamra mbalimbali ikiwemo kupiga fataki, watu kwenda kwenye nyumba za ibada kutoa shukurani na wengine kukutana katika nyumba za starehe.

Mathalani, Hispania, watu hula zabibu 12 moja kwa kila pigo la saa, usiku wa manane kama mila yao kusheherekea mwaka mpya wakiamini kuwa tendo hilo huleta habari njema.

Nchini Brazil, watu huvaa mavazi meupe na kuruka mawimbi saba wakiamini tendo hilo huleta baraka. Wenzao wao wa Scotland, sherehe ya Hogmanay hujumuisha maonyesho ya mwali wa moto, maandamano yenye mishumaa, na kuimba wimbo wa “Auld Lang Syne.” 

Licha ya mabadiliko yote hayo, kiini cha sherehe za mwaka mpya zinabaki kuwa za kimataifa. Mwaka Mpya ni ishara ya mwanzo mpya, amani, furaha katika maeneo mbalimbali duniani. 

Duniani kote, maeneo mbalimbali Januari 1 hutumika kama siku ya mwaka mpya, huku usiku wa kuamkia siku hiyo ukiambatana na shamra shamra mbalimbali. Picha|Medium.com

Heri ya Mwaka Mpya wa 2025!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks